Mastaa Yanga wampa Ramovic kiburi

Dar es Salaam. Wakati Yanga ikibakiza siku moja kucheza mechi yake ya kwanza ya hatua ya makundi ya Ligi ya Mabingwa Afrika msimu, kocha wa timu hiyo Sead Ramovic amesema licha ya muda mfupi alionao kuelekea mchezo huo wa Jumanne, Novemba 26, 2024 katika Uwanja wa Benjamin Mkapa, Dar es Salaam, amefurahishwa na uzoefu wa wachezaji wake.

Ramovic ambaye mchezo huo dhidi ya Al Hilal ya Sudan utakuwa wa kwanza kwake alisema ana imani kubwa kwamba timu yake itafanya vizuri kutokana na ukomavu wa wachezaji wake ambao wamekuwa na morali kubwa ya kushika mbinu wanazoelekezana katika uwanja wa mazoezi.

Kocha huyo alisema kwa muda ambao amekaa na timu hiyo lakini pia kuwepo kwa mechi za timu za taifa kwa mujibu wa kalenda ya Shirikisho la Soka Duniani (Fifa), hawajapata  muda wa kutosha wa kufanya mabadiliko makubwa lakini anaiamini timu yake.

Yanga itashuka Uwanja wa Benjamin Mkapa Jumanne Novemba 26 ikiwa mwenyeji wa Al Hilal ambapo mabingwa hao watetezi wa Ligi Kuu Tanzania Bara hawajawahi kupata ushindi mbele yao hivi karibuni.

“Ni kweli ni siku chache sana tangu nimeanza kazi lakini sitaki kuchukua hiyo kama kitu kitakachotufanya tusifanye vizuri, naijua timu hii kwa kiasi kikubwa kabla ya kufika hapa.

“Nafurahia kufanya kazi na wachezaji ambao wamekomaa vizuri wanajitambua na wana njaa ya mafanikio kila tunachokifanya unaona kinafanyika kwa ukubwa wake, hii itatupa nafasi ya kubadilika kwa haraka.

“Tunatakiwa kuanza vizuri kwa kucheza nyumbani. Tuna nafasi ya kufanya hivyo kutokana na aina ya wachezaji tulionao ambao wanaonyesha njaa kubwa ya kutaka mafanikio,” alisema Ramovic.

Kikosi hicho Cha Yanga Jana kilihamishia mazoezi yake kutoka Uwanja wao wa AVIC Town Kigamboni na kufanyia katika Uwanja wa Benjamin Mkapa kwa lengo la kuzoea ubora wa Uwanja huo.

Wakati Ramovic akiwa na wachezaji wake pia mkurugenzi wa ufundi wa timu hiyo Abdihamid Moalin alikuwepo nje huku akifanya vikao vifupi na kocha huyo.

Related Posts