Mbili bado hakijaeleweka Championship | Mwanaspoti

WAKATI Ligi ya Championship ikifika raundi ya 10 hadi sasa, ni timu mbili pekee za Transit Camp na Kiluvya United hazijaonja ladha ya ushindi kati ya 16 zinazoshiriki, huku makocha wa vikosi hivyo wakifunguka sababu za kuanza vibaya.

Transit iliyopo nafasi ya 15, imeshacheza michezo 10 hadi sasa ikitoka sare mitatu na kupoteza saba huku kwa upande wa Kiluvya United iliyopanda daraja msimu huu ikiburuza mkia baada ya kutoka sare mchezo mmoja tu na kupoteza tisa.

Akizungumzia mwenendo huo, Kocha wa Transit Camp, Ally Ally alisema changamoto kubwa kwao ni kwenye eneo la umaliziaji tu huku, akiwataka wachezaji wa timu hiyo kuonyesha mabadiliko ya haraka ili kuendana na ushindani wa Ligi ya Championship.

“Hadi hapa tulipo tuko nje ya malengo yetu kwa sababu michezo 10 ni mingi na hatujapata kile tulichokusudia, tumekuwa na changamoto nyingi za umaliziaji wa nafasi, hivyo tuna kazi kubwa ya kurekebisha hilo ili kuendana na ushindani ulivyo.”

Kwa upande wa kocha wa Kiluvya United, Zulkifri Iddi ‘Mahdi’ alisema licha ya ugeni wake katika timu hiyo, kumekuwa na mwenendo mzuri wa kiuchezaji tofauti na mwanzo, huku akiomba muda zaidi kutengeneza kikosi imara kwa ajili ya mechi zijazo.

Related Posts