BAADA ya African Sports kutumia Uwanja wa Jamhuri Morogoro kwa michezo yake ya nyumbani msimu huu, hatimaye kikosi hicho kimerejea kwenye Uwanja wa kituo cha TFF Mnyanjani mjini Tanga, huku Kocha Mkuu, Kessy Abdallah akieleza itawasaidia.
Kessy amezungumza hayo baada ya timu hiyo kupoteza michezo saba kati ya 10 iliyocheza baada ya kushinda miwili na kutoka sare mmoja, jambo linalomfanya kocha huyo kuamini mwenendo huo umesababishwa na kucheza mbali na mashabiki zao wa Tanga.
“Itatusaidia sana kwa sababu mashabiki zetu walikuwa hawana uwezo wa kutufuata Morogoro, tunashukuru tumerudi nyumbani na ni muda sasa kuisapoti timu yao ili ifanye vizuri na kutoka hapa tulipo, naamini kwa umoja huo itawezekana,” alisema.
Kocha huyo aliongeza, bado hakuna balansi nzuri ya kuzuia na kushambulia hivyo anarudi katika uwanja wa mazoezi kufanyia kazi changamoto hiyo, huku akiwaomba mashabiki kukipatia sapoti kikosi hicho akiamini bado ni mapema kuwakatia tamaa.
Timu hiyo ambayo ni mabingwa wa Kombe la Muungano mwaka 1988, imepanda Ligi ya Championship msimu huu baada ya kushuka daraja msimu wa 2022-2023 iliposhika nafasi ya 14 na pointi 23, huku msimu uliopita ikiwa ndio mabingwa wa First League.