Mrengo wa kulia watazamia mapinduzi kura ya rais Romania – DW – 24.11.2024

Waromania wanapiga kura Jumapili katika duru ya kwanza ya uchaguzi wa rais katikati mwa mfumuko mkubwa wa bei ambao unaweza kumnufaisha kiongozi wa mrengo wa kulia, George Simion.

Kura hiyo inazindua wiki mbili za uchaguzi nchini Romania, ikiwemo uchaguzi wa bunge na duru ya pili ya uchaguzi wa rais Desemba 8.

Miongoni mwa wagombea 13 wa urais, Waziri Mkuu wa chama cha Social Democratic, Marcel Ciolacu, anaongoza kwa asilimia 25, akifuatiwa na kiongozi wa chama cha AUR, Simion, akiwa na asilimia 15-19.

“Ninaogopa sana tutamaliza na Simion katika duru ya pili,” alisema mfanyakazi wa Tehama Oana Diaconu mwenye umri wa miaka 36, wakati akizungumza na AFP mjini Bucharest, akionesha wasiwasi kuhusu tabia isiyotarajiwa ya kiongozi huyo wa mrengo wa kulia na mashambulizi yake dhidi ya Umoja wa Ulaya.

Simion, mwenye umri wa miaka 38, anadai nafasi katika nchi maskini mwanachama wa NATO huku vyama vya mrengo wa kulia kote Ulaya vikishinda uchaguzi.

Kwa mujibu wa wataalamu, hatari ni kubwa katika kinyang’anyiro cha kumrithi Rais Klaus Iohannis, kiongozi wa mrengo wa kiliberali na mshirika mkubwa wa Ukraine, ambaye ameshikilia nafasi hiyo ambayo ni ya heshima zaidi tangu 2014.

Duru ya kwanza ya uchaguzi wa rais Romania | George Simion
Mgombea wa muungano wa siasa kali za mrengo wa kulia George Simion akizungumza na vyombo vya habari wakati wa duru ya kwanza ya uchaguzi wa rais mjini Bucharest, Romania, Novemba 24, 2024.Picha: Andreea Campeanu/REUTERS

Romania katika nafasi muhimu ya kimkakati kwa NATO

Romania, ambayo inapakana na Ukraine, imekuwa na umuhimu mkubwa tangu Moscow ilipovamia jirani yake mwaka 2022.

Nchi hiyo ya Bahari Nyeusi sasa ina nafasi ya “kimkakati muhimu” kwa NATO — kwa kuwa inahifadhi zaidi ya wanajeshi 5,000 — na ni njia ya usafirishaji wa nafaka za Ukraine, limesema shirika la utafiti la New Strategy Center katika utafiti wake.

“Demokrasia ya Romania iko hatarini kwa mara ya kwanza tangu anguko la ukomunisti mwaka 1989,” alisema mchambuzi wa kisiasa Cristian Pirvulescu alipozungumza na AFP.

Soma pia:Rais wa Romania, Iohannis kuwania uongozi wa juu wa NATO 

Baada ya ushindi wa Donald Trump katika uchaguzi wa rais wa Marekani, “hali imekuwa ngumu zaidi”, aliongeza.

Simion, anayejulikana kwa hotuba zake kali na shabiki wa Trump ambaye wakati mwingine huvaa kofia nyekundu kumuenzi kiongozi wake huyo – anatarajia kuimarishwa na ushindi  wa Trump.

Simioni ambaye anapigania “Romania yenye uzalendo zaidi”, anapinga kutuma msaada wa kijeshi kwa Ukraine na mara kwa mara hukosoa kile anachokiita “kiotoa cha rushwa na ufisadi” huko Brussels.

Romania hadi sasa imekuwa na “wasindikizaji na waoga kama viongozi,” alisema hivi karibuni, na kuongeza kuwa watu “hawakubali tena kutendewa kama raia wa daraja la pili” katika nchi nyingine.

Duru ya kwanza ya uchaguzi wa rais Romania | Marcel Ciolacu
Waziri Mkuu wa Romani na mgombea urais Marcel Ciolacu, akipiga kura yake wakati wa duru ya kwanza ya uchaguzi wa rais mjini Bucharest, Romania, Novemba 24, 2024.Picha: Octav Ganea/Inquam Photos via REUTERS

Simion afaidika na hasira za wapiga kura, Ciolacu aahidi utulivu

Simion ameshudia umaarufu wake ukiongezeka kwa kutumia hasira za wapiga kura juu ya mfumuko wa bei ulioweka rekodi huku akiahidi kutoa nyumba za bei nafuu kwa wote.

Katika juhudi za kupata uungwaji mkono kutoka Waromania wengi walioko nje ya nchi, amesafiri kote Ulaya.

Iwapo atafikia duru ya pili, mchambuzi Pirvulescu anatabiri “athari kubwa” ambayo huenda ikakipa msukumo chama chake cha AUR katika uchaguzi wa bunge wa Desemba.

Kwa ujumla, kampeni imekuwa na mizozo na mashambulizi ya kibinafsi, huku Simion akikabiliwa na tuhuma za kukutana na majasusi wa Urusi — madai ambayo amekana.

Kwa upande mwingine, Ciolacu amekabiliwa na mzozo juu ya matumizi yake ya ndege za kibinafsi.

Soma pia: Romania na Bulgaria zajiunga kwa sehemu katika kanda ya Schengen

Pamoja na viwango vya umaarufu vya chini, anatarajia kuwashawishi wapiga kura kwa ahadi yake ya kuhakikisha “utulivu” nchini Romania.

Kama kiongozi wa Chama cha Social Democratic (PSD), Ciolacu anafurahia kuungwa mkono na chama kikubwa zaidi cha Romania, ambacho kimeunda siasa za nchi hiyo kwa zaidi ya miongo mitatu, na kwa sasa kinatawala kwa ushirikiano na Chama cha Kitaifa cha Kiliberali.

Duru ya kwanza ya uchaguzi wa rais Romania | Elena Lasconi
Kiongozi wa chama cha upinzani cha mrengo wa kati-kulia cha Save Romania Unioni, USR, Elena Lasconi akizungumza na vyombo vya habari siku ya uchaguzi wa duru ya kwanza ya urais, mjini Bucharest, Romania, Novemba 24, 2024.Picha: Andreea Campeanu/REUTERS

Anayeshika nafasi ya tatu ni mwandishi wa habari wa zamani Elena Lasconi, ambaye alikua meya wa mji mdogo wa Campulung na mkuu wa chama cha upinzani cha mrengo wa kulia, ambaye anaweza kutoa mshangao.

“Matarajio yetu ni kuwa kumalizia na Lasconi katika duru ya pili — anaonekana kuwa mgombea mwaminifu zaidi,” alisema mtaalamu wa Tehama Diaconu kabla ya kupanda kwenye tram huko Bucharest.

 

Related Posts