Nashindwa hata nianzie wapi, ninakosa raha kila inapoitwa leo kwani wenzangu walikuwa wakinong’ona kuwa mtoto wangu amefanana na mfanyakazi mwenzangu hadi sasa wananiambia wazi na wengine kunicheka.
Jambo la kushangaza mke wangu hamjui huyo mtu na nina uhakika hawajawahi kuonana, kwani hata huo ujauzito wa mtoto wetu nilimpa tukiwa mkoani nilikokwenda kikazi.
Kila nikiangalia mazingira kuwa mke wangu alifanya jambo tofauti na huyu mfanyakazi mwenzangu hakuna dalili wala chembe ya shaka. Ila ninakosa raha, nishauri nifanye nini.
Usichanganyikiwe, tulia na utafakari, maisha hayajawahi kuishiwa vitu vya kushangaza. Muhimu ni kuwa unaamini mkeo hajuani na huyo mfanyakazi mwenzako na huoni dalili ya wao kukucheza shere.
Ingawa kama binadamu ninaelewa wanavyosema wanaumiza hisia zako. Kwani mtoto hata akifanana na watu wa karibu na familia siku hizi kunaleta hisia tofauti, hali inakuwa mbaya zaidi anapofanana na mtu wa nje ya familia.
Kwanza, ni muhimu kutambua hisia zako na jinsi hali hii inavyokuathiri. Ni kawaida kuhisi wasiwasi kutokana na hali hiyo, hata kama kuna sababu za kuweka mtazamo sahihi kuhusu mke wako.
Kukabiliana na wasiwasi huo ni hatua ya kwanza kutatua tatizo. Pia mtu kufanana na mwingine ni uumbaji wa Mungu, kwani unaweza kukutana na mtu nchi nyingine kabisa, lakini kafanana na mtu unayemjua kwenye familia au jirani nchini mwako, hivyo hilo lisikupe shida sana.
Mweleze mkeo kuhusu hali unayokutana nayo ili umsikie atasema nini, pengine maneno yake yakawa faraja kwako kuliko kukaa nalo moyoni peke yako.
Kujenga uaminifu na mawasiliano ni nguzo muhimu katika mahusiano. Kwa mazungumzo mazuri, utapata nafasi ya kuelezea hisia zako na kusikia mtazamo wa mke wako, jambo litakalosaidia kuondoa mashaka uliyonayo.
Aidha, ni muhimu kutafuta njia za kuimarisha heshima na furaha katika familia yako.
Badala ya kujikatia tamaa kwa msongo wa mawazo, unaweza kushiriki katika shughuli zinazofanya familia iwe na umoja.
Pia usiruhusu mtu wa nje ya familia yako kuijadili tena katika eneo la kazi, jenga mipaka ya majadiliano hayo na utakayemsikia kakuambia au kasema pembeni hakikisha unamshikisha adabu kwa kushirikisha uongozi wa mahali unakofanyia kazi ili iwe fundisho kwa wengine.
Fanya hili kwa dhati, litasaidia kuondoa huu mjadala kuhusu mtoto wako ambaye akikua akasikia atajisikia vibaya na kupata mawazo kuwa labda wewe siyo baba yake. Pia usijenge chuki na huyo mfanyakazi aliyefanana na mwanao, kwani hana hatia na pengine hajui chochote kama unavyosema hata hawajawahi kuonana.
Usiache kazi, mapenzi huisha
Nimepata mpenzi mwekezaji, kwa kweli ananipenda na kunitimizia mahitaji yangu na ya familia. Ila kuna jambo amenishirikisha huu sasa ni mwezi nashindwa kufanya maamuzi.
Nimeajiriwa serikalini kwenye ajira zenye mshahara wa kawaida, hivyo ananiambia niache kazi akaniajiri kwenye moja ya kampuni zake iliyopo mkoani Mtwara. Amenionyesha hadi mshahara nitakaolipwa, ni mara mbili ya huu wa sasa na marupurupu kibao.
Kwa kweli ameahidi kubadili maisha yangu kabisa akishaniajiri. Nimewashirikisha ndugu zangu wote wamenikatisha tamaa, nachanganyikiwa hata sijui nifanyeje. Naomba nishauri.
Pole kwa kuchanganyikiwa, ila nami naungana na ndugu zako kuwa usikurupuke kuacha kazi.
Huyu anakuajiri kwa sababu ya mapenzi na umesema ni mwekezaji, huna uhakika huo mradi au miradi itadumu kwa muda gani na je, mapenzi yakiisha utaendelea kuwa mfanyakazi wake? Najua utashangaa kusema mapenzi yakiisha.
Narudia tena, mapenzi huwa yanaisha kabisa, tena mengine huisha vibaya kwa visasi na kununiana, hapo ndiyo itakuwa shida.
Kwa kuwa ameonyesha nia ya kukusaidia uachane na masuala ya kuajiriwa, mwambie akufungulie biashara kubwa ambayo utaiendesha ukiwa kazini, ikisimama unaweza kuamua vinginevyo kwa sababu utakuwa na uhakika na biashara ni yako hata mapenzi yakiisha utaendelea kuiendesha.
Zingatia, kumbuka usije kufanya maamuzi yanayoletwa kwako kwa nguvu ya mapenzi, hata kama ni mumeo kuna vitu unapaswa kuviamua kwa umakini sana, kwani hata ndoa huvunjika.
Kipimo cha utu ni kazi na kazi ndiyo msingi wa maisha, ukiacha halafu ukaachwa utakuwa mgeni wa nani. Siombei uachwe ila hutokea watu wakaachana.