Dar es Salaam. Rais wa Tanzania, Samia Suluhu Hassan ametunukiwa Shahada ya Uzamivu ya Heshima ya Uongozi na Chuo Kikuu Mzumbe.
Kabla ya shahada hiyo, mkuu huyo wa nchi alishatunukiwa shahada nyingine tano za udaktari wa heshima katika fani mbalimbali na vyuo vikuu kutoka ndani na nje ya Tanzania.
Ukiachana na tano za awali, shahada aliyotunikiwa na Mzumbe imetokana na kilichoelezwa na Makamu Mkuu wa chuo hicho, Profesa William Mwegoha kuwa, amekuwa kielelezo cha uongozi ndani na nje ya nchi.
Kabla ya hiyo, shahada nyingine alitunukiwa na Chuo Kikuu cha Dar es Salaam (UDSM), Chuo Kikuu cha Zanzibar (SUZA), Chuo Kikuu cha Jawaharlal Nehru nchini India, Chuo Kikuu cha Ankara nchini Uturuki na Chuo Kikuu cha Anga nchini Korea.
Hata hivyo, shahada hiyo ya heshima iliyotolewa leo kwa mujibu wa Profesa Mwegoha, inakuwa ya kwanza kutolewa na chuo hicho tangu kuanzishwa kwake.
Hayo yameelezwa leo Jumapili, Novemba 24, 2024 na Profesa Mwegoha aliposoma risala katika Mahafali ya 23 ya Chuo Kikuu Mzumbe mkoani Morogoro, ambapo Rais Samia alikuwa mgeni maalumu.
Mbali na hotuba ya Profesa Mwegoha, Mkuu wa Kampasi ya Mzumbe Dar es Salaam, Profesa Cyriacus Binamungu amesoma wasifu wa Rais Samia na kueleza kwa upana juu ya sababu ya kumtunuku shahada hiyo.
Hadi wanafikia uamuzi huo, amesema walipitia kwa makini katika muktadha wa misingi ya uanzishwaji wa chuo hicho na kubaini kwa kipindi cha miaka mitatu ya uongozi wa Rais Samia anastahili shahada hiyo.
“Shahada hii ni kielelezo katika kutambua mchango wake (Rais Samia) kwenye jitihada za maendeleo endelevu ya Tanzania na nje ya nchi kwa ujumla,” amesema.
Hata hivyo, amesema mkuu huyo wa nchi ameweka historia ya kuwa Makamu wa Rais wa kwanza mwanamke na baadaye kuwa Rais wa kwanza mwanamke nchini.
Katika uongozi wake, amesema mafanikio mbalimbali yamefikiwa na ndiyo yanayofanya astahili shahada hiyo ya udaktari wa heshima.
Kwa mujibu wa Profesa Binamungu, wameangalia uongozi wa Rais Samia tangu akiwa na nafasi nyingine hadi alipokuwa Rais.
Amesoma wasifu wake akigusia mafanikio ya miaka mitatu ya Serikali chini ya Rais Samia katika sekta za afya, elimu, miundombinu, diplomasia, uchumi na demokrasia.
Katika maelezo yake hayo, amesema ndani ya uongozi wake, Rais Samia ameanzisha falsafa ya 4R iliyojenga msingi wa utawala bora na kuzaa tume ya haki jinai na kikosi kazi.
“Kwa ufupi sana haya ni baadhi ya mambo yaliyotekelezwa na Serikali ya awamu ya sita chini ya Rais Samia Suluhu Hassan.
Hatuna shaka kwamba mtunukiwa wetu amejitanabaisha kwamba yale mafunzo anayatumia vema katika kujenga ustawi wa Watanzania,” amesema Profesa Binamungu.
Awali, akitoa salamu za wizara, Waziri wa Elimu, Sayansi na Teknolojia, Profesa Adolf Mkenda ameipongeza seneti ya chuo hicho kwa uamuzi wa kikanuni wa kutoa shahada hiyo kwa Rais Samia.
Kadhalika, amempongeza Rais Samia kwa kutunukiwa shahada hiyo, akisema anastahili kutokana na uongozi wake wenye maono ya mbali, sahihi na kuwapeleka watu katika njia sahihi.
Amesema katika uongozi wake baada ya kuapishwa alifanya mabadiliko katika baraza la mawaziri na kueleza kila anachotaka katika kila wizara.
Ameeleza katika wizara ya elimu alielekeza mageuzi ya elimu, jambo ambalo mwaka mmoja baadaye dunia ikaanza kuzungumzia mageuzi hayo.
Amesema mwaka huu Umoja wa Afrika (AU) imeutambua kuwa mwaka wa mageuzi ya elimu, hivyo maono ya Rais Samia yalitangulia kabla ya ulimwengu.
Mwenyekiti wa Baraza la Chuo, Profesa Saida Yahya Othman amesema tunuku ya shahada ya heshima ni tukio la kipekee kwa mtunukiwa na mtunuku.
Amesema hiyo ni tunuku ya kwanza kwa chuo hicho, pili inakwenda kwa Rais wa Tanzania, ambaye pia ni muhitimu wa chuo hicho.
Profesa Mwegoha amesema katika mahafali hayo, kuna jumla ya wahitimu 5,012, kati yao wanawake ni 2,354 na wanaume ni 2,358 karibu asilimia 50 kwa 50.
Amesema katika mahafali hayo ya 23 kuna wahitimu 12 wa shahada za uzamivu, ikiwa ni idadi kubwa tangu kuanzishwa kwa chuo hicho.