Unguja. Wakati ripoti ya sensa ya misitu ya mwaka 2013 ikionyesha kiwango cha ukataji wa mikoko na upotevu wa misitu Zanzibar ni wastani wa asilimia 1.2 (sawa na hekta 1,277) kwa mwaka, inaelezwa sababu inayochangia tatizo hilo ni matumizi ya kuni.
Upatikanaji wa nishati bora ni msingi muhimu wa kukuza uchumi na kuboresha maisha ya jamii katika kila nchi.
Hata hivyo, baadhi ya wananchi wameanza kutambua umuhimu wa kuhifadhi mazingira kwa kushiriki katika upandaji, utunzaji na kumiliki hekta za miti kwa wingi.
Ripoti ya Hali ya Mazingira Zanzibar ya mwaka 2021 inaonyesha zaidi ya asilimia 90 ya wananchi wa vijijini wanategemea kuni kama chanzo cha nishati ya kupikia.
“Huku pembezoni bado tunakabiliwa na changamoto kubwa ya nishati, hivyo wananchi wengi wanategemea kuni na ili upate kuni, lazima ukate misitu,” amesema Asha Abdalla, mkazi wa Mkoa wa Kusini Unguja.
Akizungumza hivi karibuni, mjumbe wa Shehia ya Unguja Ukuu, Ali Hamadi Ali ameziomba taasisi husika kushirikiana nao kwa kuwapatia vitendea kazi na elimu ya ulinzi wa mazingira ili kudhibiti ukataji wa mikoko kwa masilahi ya wananchi na Taifa kwa jumla.
“Ili wananchi waachane na ajira ya ukataji wa mikoko, ambayo ni chanzo cha kuchukua hewa chafu na kusababisha ongezeko la joto, tunahitaji hatua madhubuti,” amesema Ali.
Mkazi mwingine, Hadia Hija amesema wako tayari kutunza mikoko, lakini wameiomba Serikali kuwasaidia vifaa vya kuendeleza shughuli za utalii kwa kutumia rasilimali zilizopo pamoja na kuhakikisha upatikanaji wa nishati mbadala.
Fatma Said Abdalla, mkazi wa eneo hilo, ameongeza kuwa kupitia elimu wanayopewa na wadau wa mazingira, wameanza kuelewa umuhimu wa kuhifadhi misitu, hasa kwa kupanda mikoko ili kurejesha mazingira katika hali yake ya asili.
Utafiti uliofanyika mwaka 2012 kuhusu athari za mabadiliko ya tabianchi kwa uchumi wa Zanzibar, ulibaini changamoto kubwa zinazovikumba visiwa hivyo.
Changamoto hizo ni ongezeko la joto, mabadiliko ya mifumo ya mvua, kuongezeka kwa upepo mkali, kupanda kwa kina cha bahari, mawimbi makali na matukio ya maafa yanayohusishwa na hali ya hewa.
Mkurugenzi wa Idara ya Uhifadhi wa Bahari Zanzibar, Dk Makame Omar Makame amewataka wananchi kuachana na matumizi ya kuni na mkaa unaotokana na ukataji wa mikoko ili kulinda mazingira ya bahari na kuinua uchumi wa buluu unaotegemea rasilimali za baharini. Amesema mikoko ina faida nyingi, ikiwa ni pamoja na kuhifadhi mazingira, kuzuia mmomonyoko wa ardhi na kuimarisha uzalishaji wa samaki, kaa tope na mazao ya bahari.
“Mikoko ni mazalia ya samaki na kaa tope, huchangia shughuli za utalii, na kusaidia nyuki kuzalisha asali. Pia, mikoko inazuia mawimbi ya bahari kuharibu kisiwa na kunyonya hewa ya ukaa, hivyo kupunguza athari za ongezeko la joto duniani,” amesema Dk Makame.
Ametoa wito kwa wananchi kupunguza matumizi ya mkaa na kuni, huku akisisitiza umuhimu wa jitihada za kurejesha maeneo yaliyoharibiwa kwa kupanda mikoko mipya.
Kwa mujibu wa ripoti ya mazingira, kati ya mwaka 2016 na 2021, jumla ya hekta 233.5 za mikoko zimepandwa na kuhifadhiwa Unguja na Pemba kwa ushirikiano na asasi za kiraia.
Idadi ya asasi hizo imeongezeka kutoka 25 mwaka 2016 hadi 60 mwaka 2021, ikijumuisha taasisi kama Zanzibar Women Leadership in Adaptation (ZanzAdapt).
Shaaban Peter, Ofisa wa Teknolojia wa Mradi wa ZanzAdapt, amesema mradi huo unaofadhiliwa na Global Affairs Canada, umetoa elimu kwa wanawake wa Unguja na Pemba kuhusu umuhimu wa uhifadhi wa misitu na mabadiliko ya tabianchi.
Mradi huo unatekelezwa kwa ushirikiano na Shirika la Misitu Duniani (CFI), Chama cha Waandishi wa Habari Wanawake Tanzania (Tamwa) Zanzibar na Jumuiya ya Misitu Pemba (CFP).
“Kwa pamoja, hatua hizi zinaonyesha kuwa juhudi za pamoja za Serikali, wananchi na wadau wa maendeleo zinaweza kufanikisha mapambano dhidi ya athari za mabadiliko ya tabianchi huku zikiimarisha uchumi wa buluu na uhifadhi wa mazingira Zanzibar,” amesema Peter.
Mwanasheria kutoka Ofisi ya Makamu wa Kwanza wa Rais, Saada Said amesema sera hiyo kwa sasa inafanyiwa marekebisho ili kuendana na mahitaji ya sasa.
“Tumeanza mwaka huu, lakini kuna mambo ambayo hayajahusishwa, pamoja na mabadiliko ya mikataba ya kikanda ya mazingira. Hii inahitaji kushughulikiwa. Ingawa marekebisho yalipangwa kukamilika ndani ya mwaka mmoja, changamoto kama rasilimali na ushirikishaji wa wadau zimeathiri kasi ya utekelezaji,” amesema Saada Said.
Makamu wa Kwanza wa Rais wa Zanzibar, Othman Masoud, alipokuwa katika mapitio ya sera hiyo Septemba mwaka huu, alisema Zanzibar kihistoria imebarikiwa mazingira mazuri yenye fukwe za kuvutia, bahari tajiri kwa maliasili, udongo wenye rutuba, pamoja na miti na wanyama wa aina mbalimbali.
Hata hivyo, amebainisha kuwa hali hiyo imeanza kubadilika na changamoto za kimazingira zinazoibuka sasa ni tishio kwa maendeleo endelevu ya Zanzibar.
Aidha, amesisitiza umuhimu wa kuwashirikisha wananchi katika mchakato huu kwa kuwa maliasili ni tegemeo kubwa kwa wananchi, hasa wale wa kipato cha chini.
Mapitio ya sera hiyo yanafanywa na Serikali kwa kushirikiana na taasisi ya Climate Action Network (CAN) Tanzania, ambayo inatoa msaada wa kitaalamu na kifedha kuwezesha kazi hiyo.