Dar es Salaam. Rais Samia Suluhu Hassan ametaja mambo sita aliyopitia katika safari yake ya kisiasa, akisema yamemjenga kiuongozi katika kutatua changamoto za wananchi.
Mambo hayo ni pamoja na vurugu za kisiasa Zanzibar mwaka 2001, Bunge Maalaum la Katiba, kupokea taarifa ya kifo cha Rais John Magufuli, janga la Uviko-19, vita vya Russia na Ukraine na kuadimika kwa sarafu ya Dola.
Ameyasema hayo leo Jumapili Novemba 24, 2024 baada ya kutunukiwa shahada ya sita ya heshima katika uongozi na Chuo Kikuu Mzumbe mkoani Morogoro na Mkuu wa chuo hicho, Rais mstaafu wa Zanzibar, Dk Ali Mohamed Shein.
Shahada nyingine alizowahi kutunukiwa ni za Chuo Kikuu cha Dar es Salaam (UDSM), Chuo Kikuu cha Zanzibar (SUZA), Chuo Kikuu cha Jawaharlal Nehru nchini India, Chuo Kikuu cha Ankara nchini Uturuki na Chuo Kikuu cha Anga nchini Korea.
Rais Samia amesema mambo hayo yamemjenga kiuwezo na kumfungulia upeo wa maisha ambayo sasa hivi anayatekeleza.
Kuhusu vurugu za kisiasa zilizotokea Zanzibar mwaka 2001 na kuleta mtafaruku mkubwa uliogharimu maisha ya wananchi, Rais Samia amesema pamoja na kwamba alikuwa mchanga kisasa, aliaminiwa kuwa mmoja wa mawaziri waliopewa jukumu la kuieleza jumuiya ya kimataifa, ilichotokea na hatua zilizochukuliwa kuleta amani.
“Nilikuwa na Dk Shein, akiwa Waziri wa Katiba na Utawala Bora pale Zanzibar na mimi nikiwa (Waziri wa) Kazi, Vijana, Maendeleo, Wanawake na watoto. Tulifanya kazi hii kwa umahiri mkubwa na kuja na suluhusho la kuwa na Serikali ya Umoja wa Kitaifa,” amesema.
Vurugu hizo zilisababishwa na maandamano ya Chama cha Wananchi (CUF), walioandamana jijini Dar es Salaam na visiwani Zanzibar wakipinga matokeo ya uchaguzi mkuu wa 2000.
Kuhusu uwepo wa Bunge la Katiba ambalo alihudumu kama Makamu Mwenyekiti akimsaidia hayati Samuel Sita, amesema nalo lilimpa uzoefu.
“Ikiwa ni mara ya kwanza kwa nchi yetu kuwa na Bunge la Katiba lenye uwakilishi mpana namna ile. Nililazimika kusimamia viko vilivyo na mchanganyiko wa watu wenye uzoefu, weledi na makuzi tofauti.
“Pamoja na kwamba baadhi ya wanasiasa walisusia mchakato ule wakati tunaingia ukingoni wa kazi tuliyopewa, tulifanikiwa kuandika Katiba inayopendekezwa,” amesema.
Ametaja pia tukio la kupokea taarifa ya kifo cha Rais aliyekuwa madarakani, hayati John Magufuli, akisema alilipokea kwa kufaidhaika.
Magufuli alifikwa na mauti jioni ya Machi 17, 2021 katika Hospitali ya Mzena, Dar es Salaam na mwili wake kuzikwa nyumbani kwake, Chato, Mkoa wa Geita.
“Nilikabidhiwa dhamana ya Rais, mkuu wa nchi na Amiri Jeshi Mkuu, katika kipindi ambacho Taifa kwa mara ya kwanza limeondokewa na Rais aliyeko madarakani na ikiwa ni Rais wa kwanza nchini mwenye jinsi ya kike, mambo ambayo kwa miongo sita ya Taifa letu hayakuwahi kufikiriwa wala kutokea,” amesema.
Amesema katika kipindi chake akiwa Rais kuanzia Machi 19, 2024 alipoapishwa, dunia ilikuwa kwenye changamoto ya maambukizi ya Uviko-19.
“Nikiwa bado najipanga na uhalisia wa kuwa mkuu wa nchi na kukabiliana changamoto zinazoambatana na dhamana hiyo, ikazuka vita ya Russia na Ukraine ambayo ikichanganywa na Uviko-19, vilizorotesha sana mnyororo wa usambazaji wa bidhaa mbalimbali duniani zikiwemo zile muhimu hapa kwetu kama ngano, mbolea na vipuri vya viwandani, tulipata shoti (hasara) kubwa sana,” amesema.
Wakati hayo yakiendelea, amesema mabadiliko ya sera za nchi ya Marekani pia yalileta athari ya sarafu ya Dola ambayo ni sarafu kuu katika biashara za kimataifa.
Suala la dola, Rais Samia pia alilizungumzia Novemba 14, 2024, wakati wa kuagwa kwa mwili wa Lawrence Mafuru, aliyekuwa Katibu Mtendaji wa Tume ya Mipango, ambapo alisema kulipotokea changamoto za dola, aliunda kamati ya kushughulikia hilo na Mafuru akiwa miongoni mwa wajumbe.
Alisema kamati hiyo ilimshauri vyema na walipofanyia kazi mapendekezo hayo, tatizo hilo likamalizika.
Akitoa tathmini ya mambo yote hayo mbele ya wahitimu na wageni mbalimbali kwenye mahafali hayo, Rais Samia amesema uongozi hupimwa kwa kuwavusha unaowaongoza kwenye changamoto.
“Ninachoweza kusema kwamba, baharia mzuri hujulikana wakati wa dhoruba, sio wakati bahari ikiwa shwari.
“Unaweza kuwa kiongozi hata kwa miaka 20, lakini ukapata nafasi chache za kuongoza, ikimaanishwa, kudhihirisha kipawa cha uongozi na kuwavusha unaowaongoza katika changamoto zinazohitaji utatuzi,” amesema.
Akieleza mtindo wake wa uongozi, Rais Samia ametaja misingi mikuu mitatu anayoitumia kuwa pamoja na ushirikishwaji, kutumia ushahidi katika kutoa uamuzi na kutanguliza masilahi ya Taifa.
Kuhusu ushirikishwaji, amesema amekuwa akisema Tanzania ni nchi Watanzania wote na kwamba kila Mtanzania ana haki ya kuchangia katika ujenzi wa Taifa.
“Kwa kuzingatia uzoefu nilioupata kwa hali ya kisiasa Zanzibar hasa ya uendeshaji wa Serikali ya Kitaifa, nilipokabidhiwa dhamana ya kuwa Rais, niliona haja ya kuwaunganisha Watanzania wote turudishe hisia ya utaifa na tuishi kama watu wa Taifa moja.
Ametaja falsafa yake ya R4 yenye maneno manne ya Maridhiano, Ustahamilivu, Mageuzi na Kujenga upya TaifA, akisema ina lengo la kuwashirikisha watu.
Katika hilo amesema amerejesha Tume ya Mipango ili kupanga kwa pamoja na kuwa na uratibu mzuri wa mipango.
Kuhusu kufanya uamuzi kwa kuzingatia ushahidi, amesema kikubwa hapa ni masuala ya ufuatiliaji na tahmini ili kupata maridhiano.
“Ili kupata maridhiano, tumeunda kamati kadhaa, vikosi kadhaa na tume kadhaa, vya kutafiti shughuli mbalimbali zinazohusu haki za raia, uhusiano wa kidiplomasia, uendeshaji wa iuchumi, uendeshaji wa taasisi na mageuzi wa sera na uandishi wa Dira ya 2050.”
Amesema uamuzi wa Serikali hufanyika baada ya kupata ushauri wa wataalamu na maoni ya wananchi, huku pia wananchi wakitaka kiongozi aonyeshe njia.
“Mfano mzuri katika hili, ni wakati tumepata janga la Uviko-190, ulikuwa na mjadala watu wachanje au wasichanje, lakini kama mkuu wa nchi nilipojitokeza na kuchanja hadharani na wote waliponiona, wote walifuata njia wakachanja na tukaweza kudhibiti maradhi yale,” amesema.
Kuhusu kuzingatia masilahi ya Taifa ametoa mfano wa uamuzi wa kutumia mkopo uliotolewa na taasisi za kimataifa kwa ajili ya Uviko-19, akisema waliona maelekezo ya matumizi waliyopewa hayakuwa na masilahi ya Taifa.
Maelekezo hayo yalikuwa ni kununua chanjo, kununua barakoa na vitakasa mikono.
“Tukaona lile halina masilahi kwa Taifa letu, tafsiri yetu ya kupambana na Uviko ilikuwa ni kupunguza watoto madarasani,” amesema.
Amesema awali madarasa yalikuwa na wanafunzi 120, hivyo wakasema wapunguze angalau darasa liwe na wanafunzi 50 na ndipo wakajenga madarasa 12,000 ya msingi, sekondari na elimu ya awali.
“Tulisema ili kupambana na Uviko, lazima kuwe na vituo vya vya afya katika maeneo yao, yakitokea majanga wawahiwe kule badala ya kukimbizwa hospitali za wilaya na mikoa,” amesema.
Jambo la tatu walilofanya ni kuhakikisha upatikanaji wa maji safi kwa ajili ya kukabili Uviko-19.
“Hayo mimi na wenzangu tuliona ndio masilahi ya Taifa kuliko kwenda kununua chanjo na viziba mdomo na vitakasa mikono,” amesema.
Katika hilo pia amesema Serikali yake imeimarisha mambo yanayogusa umma zikiwemo sekta za elimu, afya, umeme vijijini na kilimo.
“Bajeti ya kilimo mwaka 2021 tulikuwa na Sh519 bilioni, lakini mwaka huu 2024/25 bajeti ya kilimo ni Sh1.49 trilioni.
“Tumepeleka tukiamini kuwa kilimo ndio ajira, kilimo ndio usalama wa chakula, kilimo tunatengeneza biashara baina ya nchi zetu za Afrika lakini kilimo ndio ajira ya vijana,” amesema.
Akisoma wasifu wa Rais Samia, Mkuu wa Kampasi ya Mzumbe Dar es Salaam, Profesa Cyriacus Binamungu amefafanua sababu za kumpa shahada ya heshima, akisema wamebaini kwa kipindi cha miaka mitatu ya uongozi wa Rais Samia anastahili shahada hiyo.
Amesema mkuu huyo wa nchi ameweka historia ya kuwa Makamu wa Rais wa kwanza mwanamke na baadaye kuwa Rais wa kwanza mwanamke nchini.
Kwa mujibu wa Profesa Binamungu, wameangalia uongozi wa Rais Samia tangu akiwa na nafasi nyingine hadi alipokuwa Rais.
Akizungumza baada ya kuwatunuku shahada wahitimu mbalimbali chuoni hapo, Mkuu wa chuo hicho, Dk Shein amempongeza Rais Samia akisema anastahili.
“Mambo mengine ukielezea utaambiwa unatia chumvi, hatutii chumvi wala pilipili, lakini huo ndio ukweli kwamba anastahisi sifa hii, kwa sababu kaitumikia nchi yake na anaendelea kuitumikia kwa mafanikio makubwa,” amesema.
Kuhusu wahitimu, Dk Shein amesema hakuna njia ya mkato katika maisha, akiwataka watafute elimu kwa bidii.
Awali, akitoa salamu za wizara, Waziri wa Elimu, Sayansi na Teknolojia, Profesa Adolf Mkenda ameipongeza seneti ya chuo hicho kwa uamuzi wa kikanuni wa kutoa shahada hiyo kwa Rais Samia.
Mkuu wa chuo hicho Profesa William Mwegoha amesema katika mahafali hayo, kuna jumla ya wahitimu 5,012, kati yao wanawake ni 2,354 na wanaume ni 2,358 ambayo ni karibu asilimia 50 kwa 50.
Amesema katika mahafali hayo ya 23 kuna wahitimu 12 wa shahada za uzamivu, ikiwa ni idadi kubwa tangu kuanzishwa kwa chuo hicho.