Starkie aibukia Harborough Town | Mwanaspoti

UNAMKUMBUKA Ben Starkie yule mwamba aliyekiwasha kwenye kikosi cha timu ya taifa ‘Taifa Stars’, jamaa yuko zake Harborough Town FC ya England.

Starkie kabla ya kujiunga na timu hiyo, alichezea klabu mbalimbali ikiwemo Leicester City ya vijana, Wilhelmshaven, Shepshed Dynamo, Spalding United, Basford United, Alfreton Town na Ilkeston Town.

Mara ya mwisho kiungo huyo kuonekana uwanjani ni June 02 akiwa na Stars akiingia kutokea benchi kwenye mechi ya kimataifa ya kirafiki dhidi ya Indonesia ikitoa suluhu.

Tangu hapo hakuwa na timu baada ya kumaliza mkataba na Ilkeston na hakuitwa kwenye kikosi cha Stars kilichofuzu kucheza Afcon mwakani nchini Morocco.

Mwezi uliopita alijiunga na Harborough akicheza mchezo wake wa kwanza Novemba 02 kwa dakika zote 90 dhidi ya Tonbridge, timu yake ikiondoka na ushindi wa mabao 4-1.

Timu hiyo ikiwa imecheza mechi 17 ipo nafasi ya 14 kati ya 19 zinazoshiriki ligi hiyo ikishinda mechi tano, sare tano na kupoteza saba.

Harborough Town FC inayopatikana Market Harborough, Leicestershire, England, inashiriki Ligi Daraja la Tatu ‘Southern League Premier Division Central’, ambayo ni sehemu ya ngazi ya tatu katika mfumo wa National League System.

Timu yao inatumia uwanja wa Bowden Park na ni maarufu kwa kukuza vipaji vya ndani kupitia programu zake za vijana.

Ilianzishwa mwaka 1975 kama timu ya vijana ikiitwa Harborough Town Juniors na mwaka 2008 ilirekebishwa kuwa klabu ya kisasa na kuunganishwa timu ya watu wazima, Spencer United.

Spencer United ilijiunga na Daraja la Tano la Leicester & District Mutual League mwaka 1976 na kushinda ubingwa wa ligi hiyo msimu wa 1977–78, wakapandishwa hadi Daraja la Pili.

Msimu uliofuata iliwawezesha kupanda hadi Daraja la Kwanza ingawa walishushwa daraja kurudi Daraja la Pili baada ya misimu mitatu, walikuwa washindi wa pili wa Daraja la Pili msimu wa 1987–88 na wakapandishwa hadi Ligi Kuu.

Related Posts