Dar es Salaam. Mgombea wa Uenyekiti wa serikali ya mtaa kwa Tumbi Kata ya Tandale kupitia Chama cha Tanzania Labour (TLP), Ruben Peter amewataka wananchi wa eneo hilo wampigie kura nafasi ya uwenyekiti, lakini nafasi za ujumbe wachague kutoka Chadema.
Hayo yamesemwa juzi Novemba 23,2024 na Peter alipokuwa akifanya kampeni hizo katika viwanja vya Mashuka Tandale kwa Tumbo, ambapo alisema wameamua kuungana Ili kutengeneza serikali ya mseto ambapo wananchi hao wanapopiga kura katika nafasi ya uenyekiti achaguliwe mgombea huyo na nafasi za ujumbe wachague wa Chadema.
Peter alisema lengo ni kufanya kazi kwa kushirikiana ili kuwaletea maendeleo wananchi wa mtaa huo.
“Nipeni uenyekiti lakini kwenye nafasi za ujumbe wapeni Chadema tutashirikiana nao huu mseto haushangazi mbona hata majumbani ndiyo tunavyoishi,”alisema Peter
Pia alisema atadumisha amani katika mtaa huo na kuhakikisha maendeleo yanapatikana na huduma za barua za utambulisho zitatolewa bure.
Alisema akichaguliwa atahakikisha suala la usafi wananchi watalipa kwa kaya na siyo kwa kila chumba kama ilivyo sasa.
Hata hivyo alipotafutwa Mwenyekiti Wilaya wa Chama cha Chadema, John Mwende alisema siyo msimamo wa chama chao kuungana na vyama vingine kinachojitokeza ni makubaliano waliojiwekea wagombea wenyewe.
“Hiyo inatokana na wapinzani kukatwa kama hapo Tandale Mtaa wa Tumbi aliyepitishwa na chama chetu kugombea uenyekiti amekatwa, lakini wajumbe wawili wamepitishwa hivyo kwa kuwa upande wa chama cha TLP wana mgombea wa uenyekiti lakini wajumbe wao wamekatwa hivyo wameamua wao wenyewe kuungana kwa pamoja,”alisema Mwende
Naye Katibu Mkuu Taifa wa Chama hicho, Richard Lyimo amewataka wananchi wanapochagua viongozi wa wasichague wasio na uwezo kwa kuwa watakuwa wanatumikishwa na watu wenye uwezo kwa kuwapa rushwa
“Kama mgombea wa chama changu ni mfanyabiashara hatashawishika kupokea rushwa kwa kuwa ana uwezo na ninawaomba mchague mtu msiangalie dini au kabila mtachagua asiyekuwa sahihi,”alisema Lyimo.