Ushiriki wa Rais Samia G20 wainufaisha Tanzania

Na Mwandishi Wetu, Rio de Janeiro, Brazil

Ushiriki wa Rais Samia Suluhu Hassan katika Mkutano wa G20 uliofanyika hapa Rio de Janeiro, Brazil na kuhusisha nchi tajiri 19 duniani, Umoja wa Ulaya (EU) na Umoja wa Afrika (AU), umekuwa wa manufaa makubwa kwa Tanzania na Bara la Afrika.

Mkutano huu ulitawaliwa na ajenda kuu tatu, ambazo zilihusu kuodoa njaa duniani, matumizi ya nishati safi na utawala bora – wakilenga ushiriki wa nchi za ulimwengu wa tatu katika vyombo vya uamuzi duniani kama Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa zipate kura ya turufu na ujumbe wa kudumu, Benki ya Dunia na vingine.

Akizungumza na wahariri jijini hapa, Rais Samia amesema kitendo cha kualikwa kimempa nafasi ya kusikilizwa uso kwa uso na viongozi wakuu wa nchi hizi 19 ambazo zinashikilia asilimia 85 ya uchumi wa dunia na zinafanya biashara zote kwa asilimia 76.

“Sisi siyo wanachama wa G20, lakini wameona haja ya kutualika kama Tanzania kushiriki mkutano huu. Ushiriki wetu una manufaa makubwa kama Tanzania, lakini kama Afrika. Kwa sababu katika mkutano huu, kama mnavyojua, nchi zote zilizoendelea ndizo zipo katika group la G20. Sasa ukipata nafasi ya kualikwa na ukapewa kijinafasi cha kusema hapo, basi hayo ni mafanikio, kutambulika, kuitwa na kusema mbele ya hao,” amesema.

Moja ya mafanikio ya mkutano huu nchi hizi tajiri duniani zimezindua mikakati miwili endelevu, ambapo G20 wamezindua rasmi Muungano wa Kimataifa Dhidi ya Njaa na Umaskini (GAAHP) na Muungano wa Kimataifa wa Nishati Safi (GCPA), ambao umesimamiwa na nchi za Brazil na Uingereza. Kama sehemu ya mafanikio, Januari mwakani, Tanzania itakuwa na mkutano wa marais wote wa Africa utakaofanyika jijini Dar es Salaam, ukihusu Nishati Safi.

Rais Samia ametumia mkutano huu kusisitiza ajenda ya Nishati Safi ya Kupikia, ambapo kwa Tanzania watu zaidi ya 3,000 hufariki kila mwaka kutokana na kuvuta hewa ya ukaa inayotokana na matumizi ya kuni na mkaa hivyo kuathiri afya zao. Hawa wanakwenda kuokolewa. Tanzania tayari imezindua Mkakati wa Nishati Safi, ambapo kufikia mwaka 2034, asilimia 80 ya Watanzania wanapaswa kuwa wanatumia nishati safi ya kupikia. Nchi hizi za G20 zimeahidi kusaidia utekelezaji wa mpango huu.
.

Mkutano wa G20 wa mwaka 2024 uliofanyika hapa Brazili, ukiwa na kaulimbiu “Kujenga Dunia ya Haki na Sayari Endelevu,” umewakutanisha viongozi wa dunia kujadili masuala muhimu yanayogusa maisha ya kila siku ya watu wengi, wakiwemo Watanzania. Matokeo ya mkutano huu yanalenga kuleta manufaa ya moja kwa moja katika sekta za kilimo, nishati, na utulivu wa kiuchumi nchini. Ushiriki wa Rais Samia Suluhu Hassan umehakikisha kwamba sauti ya Tanzania imesikika katika ngazi za kimataifa, na kuweka msingi wa miradi itakayosaidia wakulima, kaya, na uchumi kwa ujumla.

Moja ya ajenda kuu za mkutano huo ilikuwa kumaliza njaa duniani, suala linaloigusa Tanzania kwani zaidi ya 65% ya watu hutegemea kilimo. Wakulima wa maeneo kama Mbeya, Morogoro, na Kilimanjaro wanakabiliwa na changamoto za ukosefu wa vifaa vya kisasa na hali ya hewa isiyotabirika. Rais Samia amesisitiza msaada wa kimataifa kwa kilimo kidogo, upatikanaji wa mbegu bora, na kukabiliana na mabadiliko ya tabianchi.

Pia, ameweka msisitizo wa nishati safi na endelevu hivyo kuleta matumaini kwa maeneo ya vijijini, ambako familia nyingi bado zinategemea kuni. Rais Samia amesema lengo lililowekwa ni kuwa ifikapo mwaka 2030, Waafrika milioni 300 wawe wamepata umeme. Kwa sasa Waafrika zaidi ya milioni 700 hawana umeme. Amejenga hoja juu ya upatikanaji wa ufadhili wa miradi ya nishati mbadala kama jua na upepo, na viongozi hawa wamemwelewa.

Kimataifa, ametetea mageuzi katika Shirika la Fedha Duniani (IMF) na Beni ya Dunia (WB) kuhakikisha wanaweka masharti bora kwa mikopo ya miradi ya maendeleo. Ushiriki wa mkutano huu unatarajiwa kuinua sekta kama kilimo, nishati, na utalii, ukiboresha maisha ya Watanzania na Afrika kwa ujumla.

Mkutano wa G20 wa mwaka 2024 haukuwa tu jukwaa la viongozi wa kisiasa, bali ulikuwa fursa ya kupata suluhisho za changamoto zinazowakabili Watanzania na Waafrika kila siku. Kutoka kushughulikia njaa hadi kuboresha upatikanaji wa nishati na kutetea mfumo wa haki wa kimataifa, mkutano huu umeweka msingi wa mustakabali mzuri kwa familia, wakulima, na biashara nchini. Matokeo yake yanasisitiza umuhimu wa ushiriki wa Tanzania katika kuunda ajenda ya dunia iliyo jumuishi na endelevu.



Related Posts