Vigogo wajitosa kampeni uchaguzi serikali za mitaa

Dar es Salaam. Wakati kampeni za uchaguzi wa serikali za mitaa zikiingia siku ya tano leo, vigogo wa vyama mbalimbali vya siasa vikiwemo vya upinzani wamejitosa kushiriki na kuongeza nguvu.

Hatua ya viongozi hao imekuja ikiwa zimebaki siku mbili kufanyika uchaguzi huo.

Uchaguzi huo wa vijiji, vitongoji na mitaa utafanyika Jumatano ya Novemba 27, 2024. Ambayo imeshatangazwa kuwa ni siku ya mapumziko ili kutoa fursa kwa wananchi kushiriki kikamilifu kuchagua viongozi wao.

Sababu za kuibuka kwa vigogo hao zimetajwa na wachambuzi wa siasa na jamii waliozungumza na Mwananchi kuwa ni kuimarisha vyama vyao, kusaka kura kwa wagombea wao, kuleta hamasa kwa wananchi kushiriki chaguzi na kusahau yaliyojitokeza katika uchaguzi kama huo mwaka 2019.

Wakati wachambuzi wakibainisha hayo, Waziri mwenye dhamana ya uchaguzi huo wa Ofisi ya Rais-Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (Tamisemi), Mohamed Mchengerwa anasema,”umekuwa uchaguzi wa kupekee sana, wenye hamasa kubwa kila sehemu, ndio maana unaoana viongozi wakuu wa vyama wanafanya kampeni kila kona.”

Waziri Mchengerwa anasema hamasa ya mwaka huu haijawahi kutokea, “hii imechagizwa na maandalizi kuwa shirikishi.”

Baadhi ya vigogo hao ni  wajumbe wa Halmashauri Kuu ya Chama cha Mapinduzi (NEC), January Makamba na Nape Nnauye, Zitto Kabwe (kiongozi mstaafu wa ACT-Wazalendo), Juma Duni Haji (mwenyekiti mstaafu wa ACT-Wazalendo) na Freeman Mbowe (Mwenyekiti wa Chadema), ambao wanatumia majukwaa katika maenei mbalimbali kumwaga sera ili kusaka ushindi kwa vyama vyao.

Nape ambaye ni Mbunge wa Mtama mkoani Lindi aliyekuwa kimya kwa muda baada ya kuondolewa nafasi ya uwaziri Julai mwaka huu, aliibukia kwenye uzinduzi wa kampeni za uchaguzi huo mkoani Rukwa.

Waziri huyo wa zamani wa Wizara ya Habari, Mawasiliano na Teknolojia ya Habari, alipangiwa na CCM kuzindua kampeni mkoani humo, ambapo alisema chama hicho kimejipanga kushika dola kwa kishindo kwa kufanya kampeni kwa lengo la kunadi sera zao.

Wakati Nape akiibukia Rukwa, Makamba ambaye ni waziri wa zamani wa Wizara  Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Kimataifa, alijikita katika jimbo lake la Bumbuli mkoani Tanga akitaja sababu mbalimbali zitakazowezesha CCM kuibuka kidedea.

Katika maelezo yake, Makamba alisema sera, ubora wa wagombea na  wa chama na rekodi ndio yanayoibeba CCM kuibuka kidedea katika maeneo mengi ambayo chama hicho kimesimamisha wagombea.

Licha ya kutangaza kustaafu uongozi ndani ya ACT – Wazalendo, Zitto amekuwa akionekana kwa nyakati tofauti kwenye majukwaa, lakini safari hii uchaguzi wa serikali za mitaa ameamua kuuvalia njuga kwa kufanya mikutano 10 hadi 11 kwa siku ili kunadi sera za chama chake.

Akiwahutubia wananchi wa Muhambwe mkoani Kigoma, Zitto amewataka kuyatumia mamlaka hayo kupiga kura ya hapana katika maeneo yenye mgombea mmoja wa CCM, baada ya upinzani kuenguliwa.

Sio Zitto tu, bali hata Babu Duni ambaye ni mwanasiasa mkongwe kwa muda mrefu alikuwa kimya tangu atangaze kustaafu Septemba 2024, lakini ameibukia kwenye kampeni za uchaguzi wa serikali za mitaa, akipangiwa na chama chake kuwanadi wagombea wa Dar es Salaam.

Akiwanadi wa wagombea wa uenyekiti wa mitaa ya Idrissa na Mwinyimkuu, Magomeni jijini hapa, Babu Duni amesema, “wewe ndiye unayekwenda kupiga kura, wewe ndiye unayesema siitaki CCM, ni wewe.”

“Sasa nyinyi mmeachiwa mitaa miwili, itakuwa miujiza msishinde, itakuwa miujiza kura mzipoteze, itakuwa miujiza msiende kupiga kura, kwa maana miaka ijayo itakuwa migumu kwenu CCM akishinda,” amesema Duni. 

Kwa upande wake, Mbowe alianza kuwanadi wagombea wa chama chake ikiwa ni  katika kampeni za uchaguzi wa serikali za mitaa katika mikoa ya Songwe na Mbeya.

Akiwa katika mikoa hiyo, Mbowe ambaye ni kiongozi wa zamani wa Kambi ya Rasmi ya Upinzani bungeni (KUB) amewataka wananchi Songwe na Mbeya kufanya uamuzi sahihi wa kukichagua Chadema katika nafasi zote za uenyekiti wa mitaa, vijiji na vitongoji.

Mchambuzi wa siasa na jamii, Ramadhani Manyeko anasema uchaguzi ni uchaguzi huwezi kusema chama fulani kinashinda pasipo kufanya maandalizi ikiwemo kampeni za kusaka kura.

“Moja ya dhamira ya chama cha siasa ni kushika dola, unashikaje dola? Lazima uanzie ngazi ya chini ya mitaa, vijiji na vitongoji,” anasema Manyeko.

Manyeko anadai morali ya wananchi kushiriki uchaguzi bado ipo licha ya  yaliyojitokeza katika mchakato wa uchaguzi kama huo mwaka 2019/ 2020, ambapo wagombea wengi hasa wa upinzani walienguliwa kwa sababu mbalimbali.

Mwaka 2019 CCM ilibuka kidedea katika hatua ya ngazi ya uteuzi, baada ya kushinda vijiji, vitongoji na mitaa kwa zaidi ya asilimia 90. Kutokana na hilo, baadhi ya vyama kikiwemo Chadema vilisusia.

Pia, mchakato huo ulilalamikiwa na wadau wa demokrasia waliodai haki haikutendeka, wakieleza iliwekwa rekodi ya wagombea wa upinzani kuenguliwa kuliko chaguzi za aina hiyo zilizopita.

Mbali na hilo, Manyeko anasema uchaguzi wa mwaka 2024 umekuwa na malalamiko mbalimbali kuanzia uandikishaji hadi uteuzi, ambapo wagombea wa vyama upinzani walienguliwa kwa sababu tofauti ikiwemo kukosea majina, herufi na muhuri.

Hatua hiyo ilisababisha CCM kuingilia kati kwa kuiomba Ofisi ya Rais (Tamisemi), kuyapuuza makosa madogo yaliyojitokeza wakati wa ujazaji wa fomu na  kuwarejesha walioenguliwa, ili kuleta ushindani katika uchaguzi huo utakaofanyika Novemba 27,2024).

Ombi hilo lilifanyiwa kazi na Waziri wa Tamisemi, Mohamed Mchengerwa aliyeongeza siku mbili za wa uwasilishaji wa rufaa akizitaka kamati  za wilaya kuitisha fomu za wagombea wote walioenguliwa/hawakuteuliwa, ili kufanya mapitio na kujiridhisha.

Katika maelezo yake, Manyeko amesema kuna maeneo yamefanya vizuri uchukuaji na urejeshaji wa fomu, akisema sintofahamu hiyo inasababishwa na baadhi ya wananchi kukosa elimu ya uraia.

“Sasa vyama lazima vitoke vikawakumbushe wananchi elimu ya uraia, wajibu wao na namna ya kupiga kura, shida tulionayo wanakosa elimu ya uraia na hawaoni faida ya uchaguzi, sasa bila viongozi kutoka na kuwajenge uwezo itakuwa ngumu.

“Nimefanya utafiti wangu kama mchambuzi hata mikutano ya hadhara ya kampeni baadhi ina hamasa sio yote na wananchi sio wengi kwa kiasi hicho, kwa hiyo lazima vigogo watoke kuona namna vyama vyao vinavyoungwa mkono,” anasema Manyeko.

Manyeko anasema kwa miaka sita vyama vya siasa havikufanya shughuli za kisiasa kwa ufanisi, kwa hiyo inahitajika nguvu kubwa na kurejesha hali ndio maana vigogo hao wanatoka au wanatumia fursa ya uchaguzi wa serikali mitaa kuviimarisha vyama vyao.

Mchambuzi mwingine wa siasa, Kiama Mwaimu anasema kuna mambo mawili yaliyosababisha vigogo hasa wa upinzani kujitokeza katika kuwapigia kampeni wagombea wao wa maeneo mbalimbali.

Miongoni mwa mambo hayo, Mwaimu anasema ni kuhakikishiwa uchaguzi wa mwaka huu, utakuwa huru na haki tofauti na mchakato uliopita wa mwaka 2019/20.

Kwa nyakati tofauti, Rais Samia Suluhu Hassan, amekuwa akiwahakikishia wadau wa demokrasia, wanasiasa na Watanzania kwamba uchaguzi utakuwa huru na haki, atakayeshinda atatangazwa.

“Chaguzi zilizopita zilikuwa na matatizo yake, lakini safari hii ilishatamkwa mapema uchaguzi utakuwa huru na haki, sasa watu wanataka kuthibitisha nadharia hiyo, kweli kutakuwa na usawa kwa wote katika uchaguzi huu? Ndio maana unaona vigogo wanajitokeza.

“Ili likitokea la kutokea wapate cha kusema kwamba mchakato haukuwa na demokrasia, ndio maana viongozi wakubwa wa upinzani wameshawishika kujitokeza mstari mbele kushiriki,” anasema Mwaimu.

Kuhusu kujitokeza kwa Makamba na Nape, Mwaimu anasema kuna lengo la kuhakikisha wanatoa usaidizi kwa chama chao ili kiibuke na ushindi katika mchakato huo.

“Walikuwa kimya kwa muda kidogo, sasa huu uchaguzi unahusisha watu wengi, lazima waongeze nguvu zao ili kukihakikishia ushindi CCM, kuliko kukaa kimya, lakini uwepo wao jamii inaona uchaguzi huu sio lelemama,” anasema Mwaimu.

Related Posts