Wasomi wasema janga la Kariakoo ni somo

Dar es Salaam. Ingawa tukio la kuporomoka kwa jengo la ghorofa Kariakoo limeacha maumivu, wanazuoni wamesema ni somo kwa Taifa hasa kwa kuzingatia taratibu za kitaalamu na kisheria kabla, wakati na baada ya ujenzi.

Wakizungumza kwa nyakati tofauti na Mwananchi, wamesema tukio hilo liwe kumbukumbu mbaya kwa nchi ili kuondoa mtindo wa kufanya kila kitu kwa mazoea badala yake ifuatwe michakato sahihi.

Jengo hilo liliporomoka asubuhi ya Novemba 16, mwaka 2024 katika Mtaa wa Mchikichi, Kariakoo na kusababisha vifo 20, zaidi ya 80 wakijeruhiwa na uharibifu wa mali ya mamilioni.

Kutokana na tukio hilo, Rais Samia Suluhu Hassan alimtaka Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa kuongoza kamati ya uchunguzi.

 Tayari Majaliwa ameshaunda kamati hiyo yenye wajumbe 19 na ameizindua huku akiitaka ikatende haki kwa mujibu wa sheria.

Hata hivyo, Rais Samia alishaweka wazi Serikali haitasita kubomoa majengo yote sokoni hapo, iwapo ripoti ya tume hiyo itaelekeza ifanyike hivyo.

Pia, alisema iwapo tume hiyo itashauri majengo yote sokoni hapo yavunjwe, hatasita kufanya hivyo.

“Sasa tume imeona nini, imesema nini, imetushauri nini, kama tume itatushauri tuendelee kubomoa majengo yasiyokuwa na sifa hatutasika kufanya hivyo. Kwa hiyo hatua zote ambazo tume itatushauri hatutasika kufanya hivyo,” alisema Rais Samia.

Pia, alisema anatambua uwepo wa ripoti za tume mbalimbali ikiwamo ya mwaka 2013, akisema uchunguzi unaofanywa utazingatia mapendekezo ya tume hiyo.

Tume ya mwaka 2013, iliundwa baada ya jengo la ghorofa 16 katika makutano ya barabara za Zanaki na Indira Ghandi kuanguka na kupoteza uhai wa watu 36.

Hatua hiyo ilisababisha Kampuni ya Design Plus Architects (DPA) kupewa zabuni ya kukagua majengo Manispaa ya Ilala kujua usalama wake na Novemba 5, 2013, ilitoa ripoti yake.

Katika ripoti hiyo, DPA iliweka wazi kuwa, kati ya maghorofa 90 yaliyokaguliwa, 67 yalijengwa kinyume cha sheria.

Akizungumza na Mwananchi,  mwanazuoni aliyebobea katika Udhibiti wa Maafa, Dk Egidius Kamanyi amesema umakini ndiyo jambo muhimu ambalo Tanzania inapaswa kujifunza baada ya janga hilo.

Dk Kamanyi amesema umakini huo ni kuacha kufanya vitu kiholela, badala yake kila kinachofanywa kizingatiwe taratibu za kitaalamu na kisheria.

Ameeleza katika ujenzi wa ghorofa kuna michakato ya kihandisi inayohusisha upimaji udongo na utaalamu wa ujenzi wenyewe.

Dk Kamanyi amesema mchakato huo wa ujenzi pia, unahusisha utekelezwaji wa sheria zikiwamo zinazoelekeza kufanywa tathmini mbalimbali kabla ya utekelezaji wa ujenzi.

Amesema baada ya ujenzi pia kuna sheria zinazopaswa kutekelezwa na mamlaka mbalimbali ikiwamo ukaguzi wa jengo na kuangalia usalama wa watumiaji.

“Katika yote hayo, tunachopaswa kujiuliza kwamba michakato yote hii inafuatwa kabla ya utekelezwaji wa miradi kama hii ya ujenzi? Au tunajenga bila kuzingatia taratibu za kitaalamu na kisheria kwa sababu tumezoea kufanya hivyo,” amehoji Dk Kamanyi.

Amesema kilichotokea Kariakoo ingawa bado sababu haijawekwa wazi, lakini kinaweza kuhusiana na ukiukwaji na taratibu za kitaalamu na kisheria.

Katika yote hayo, Dk Kamanyi amesema kuna taasisi zenye mamlaka ya kuyatekeleza, hivyo zinapaswa kutimiza wajibu wao.

Dk Kamanyi amesema kila taasisi yenye mamlaka ya kukagua, kusimamia na kutathmini kabla ya ujenzi, ifanye hivyo kwa ustawi wa uhai wa Watanzania.

“Tuzingatie kanuni na taratibu za kitaalamu na kisheria kabla, wakati na baada ya ujenzi,” amesema Dk Kamanyi.

Mtaalamu wa Uhandisi wa Miundo na Ujenzi wa Chuo Kikuu cha Dar es Salaam (UDSM), Dk Daudi Augustino amesema cha kujifunza ni kuzingatia kanuni za ujenzi.

Miongoni mwa kanuni hizo, amesema ni kuhakikisha kabla ya ujenzi wa ghorofa utafiti wa udongo unaanza kufanywa.

Amesema utafiti huo unawezesha kujua aina ya udongo wa eneo husika na uwezo wake wa kuhimili mzigo kwa maana ya jengo.

Dk Augustino amesema udongo ndiyo unaoamua ni ghorofa ngapi zijengwe katika eneo husika.

“Ukiwa na udongo mzuri unaweza kujenga hata ghorofa 50, lakini kabla ya kujenga ghorofa lazima utafiti wa udongo ifanyike,” amesema Dk Augustino.

Amesema hatua hiyo, inafuatiwa na jukumu la mhandisi wa miundo kujiridhisha ni aina gani ya nyumba itajengwa kulingana na udongo husika.

Dk Augustino amesema mhandisi huyo anapaswa kusikiliza mahitaji ya mteja, kisha amshauri kutokana na uhalisia wa udongo husika.

Pia, amesema umbali kutoka nyumba moja ya ghorofa hadi nyingine pia unapaswa kuzingatia aina ya msingi uliojengwa katika nyumba ya jirani.

“Kama msingi wa jirani yako ni ‘Isolated Parts’ lazima uzingatie wakati unachimba wa kwako, vinginevyo utasababisha kupoteza ubora wa jirani yako au wa kwako,” amesema Dk Augustino.

Katika hilo, amesema ndipo watu wa mipango miji wanapoingia kwa ajili ya kushauri kutokana na uhalisia wa msingi wa jirani zako.

Dk Augustino amesisitiza hizo ndizo njia zinazopaswa kufuatwa katika ujenzi wa jengo lolote la ghorofa na mamlaka zinazohusika zinapaswa kuhakikisha inafuatwa bila kupuuzwa chochote.

Wito wa kuzingatiwa kwa taaluma na kufuatwa kwa taratibu za ujenzi, unatolewa pia na Mhandisi wa Ujenzi na Miundo, Dk Emmanuel Moshi akisema katika kila kazi inayofanywa, taaluma zinapaswa kupewa nafasi na kuheshimiwa.

“Ikitokea unajenga, kuwe na usimamizi wa mtaalamu na Serikali imlazimishe mwenye nyumba atumie wataalamu sio ilimradi mjenzi,” amesema Dk Moshi.

Pia, amesisitiza zinapozingatiwa taaluma, inakuwa rahisi kupata pa kuanzia litakapotokea janga lolote kama la jengo la Kariakoo.

Kufuatia jengo hilo kuporomoka, aliyewahi kuwa Waziri wa Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi na mkurugenzi wa Shirika la Makazi la Umoja wa Mataifa (UN-Habitat), Profesa Anna Tibaijuka, kupitia mtandao wa kijamii wa X (zamani Twitter) aliandika:

“Kwa sheria za mipango miji ilitakiwa viwanja vinne vya ‘high density’ viunganishwe mbele na nyuma kipatikane kiwanja kimoja kikubwa cha kujenga ghorofa imara yenye ‘basement’ kubwa kupaki magari.

“Ghorofa inayofunguka kwenye mtaa wa mbele na nyuma awali katika awamu ya tatu ushauri huo wa wataalamu wa mipango miji ulishapuuzwa na viongozi kwa presha ya wawekezaji, kwa hiyo maghorofa Kariakoo na kwingineko yanajengwa kiholela kwenye viwanja visivyokidhi vigezo.

“Pamoja na madhaifu ya usimamizi wa ujenzi kiuhandisi ni vigumu majengo kuwa imara bila kuwa na eneo la kutosha kujenga kitako yaani ‘base foundation’ stahiki. Naendelea kuhimiza kurekebisha kosa hilo.

“Sasa tunavuna hasara kubwa ya upotevu wa mali, maisha na fursa za ajira na aibu ya kushindwa kusimamia viwango vya ujenzi miaka 63 baada ya uhuru. Naendelea kushauri viwango vya ‘vertical development’ vizingatiwe kuanzia sasa. Tujisahihishe.”

Related Posts