Watanzania mguu sawa gofu Morocco

TIMU  ya Taifa ya gofu ya Wanawake imeanza rasmi mazoezi ya kuvisoma viwanja vya Klabu ya Taghazout , mjini Agadir kutakapofanyika michuano ya Afrika inayoanza kesho , Morocco.

Timu hiyo iliyoondoka nchini mwishoni mwa juma, imewasili salama kwa michuano hiyo inayochezwa mjini Agadir kuanzia leo hadi hadi Novemba 30.

Rais wa Chama cha Gofu ya Wanawake nchini, TLGU, Queen Siraki alisema ratiba ya michuano, wachezaji nyota kutoka mataifa yote ya Afrika watafanya mazoezi ya siku tatu, Jumatatu, Jumanne na Jumatano kabla ya kuingia vitani rasmi Alhamisi, Ijumaa na Jumamosi.

“Ni mashindano yatakayoshirikisha mashimo 54 na kila siku timu itacheza mashimo 18. Alama bora kutoka kwa wachezaji wawili ndizo zitahesabiwa wakati mchezaji wa tatu atakuwa ni wa akiba,” alifafanua Siraki.

Chini ya uongozi wa nahodha Hawa Wanyeche kutoka Dar es Salaam,  wachezaji wengine ni Madina Iddi na Neema Olomi kutoka Arusha, wakati viongozi walioandamana na timu ni katibu wa TLGU, Yasimin Challi na Ayne Magombe ambaye ni ndiye Meneja wa timu.

 “TLGU inaamini wachezaji wetu watatumia vizuri  siku tatu za mazoezi ili kuvifahamu vyema viwanja vyote 18  na changamoto zake ili waweze kupeperusha vyema bendera ya Tanzania nchini Morocco,” alisema Siraki.

Related Posts