Zaidi ya wagonjwa 600 wahitaji kupandikizwa ini Muhimbili

Dar es Salaam. Zaidi ya wagonjwa 600 wanahitaji kupata huduma ya upandikizaji wa ini katika Hospitali ya Taifa Muhimbili (MNH), huku ikitarajia kuanza kutoa huduma hiyo mwishoni mwa mwaka 2025.

Mpaka sasa, Muhimbili inatoa rufaa ya matibabu hayo nje ya nchi na gharama za upandikizaji wa ogani hiyo ni kati ya Sh66.4 milioni hadi Sh71.7 milioni kwa mgonjwa mmoja.

Imeelezwa kuna ongezeko kubwa la wagonjwa wenye matatizo ya ini nchini huku takwimu zikionyesha kati ya wagonjwa wanaolazwa katika kitengo cha magonjwa ya mfumo wa chakula na ini Muhimbili, asilimia 60 wanaugua ini na hufika hospitali katika hatua za mwisho za ugonjwa.

Daktari bingwa mbobezi wa upasuaji wa magonjwa ya mfumo wa chakula na ini na bingwa wa upasuaji kupitia tundu dogo, Kitembo Salumu amesema mpaka sasa takwimu za hospitali zinaonyesha kuna zaidi ya wagonjwa 5,000 wenye shida kwenye ini.

Amesema kati yao 2,333 wana uvimbe kwenye ini na 607 wamegungulika kuwa na tatizo la saratani ya ini, wengine maini yamesinyaa hivyo wote wanahitaji huduma ya kupandikizwa ambao gharama yake nje ya nchi ni kubwa.

Dk Kitembo amesema matibabu pekee kwa waliogundulika na saratani ya ini pamoja na ini kusinyaa ni upandikizaji.

“Ingawaje wagonjwa wenye uvimbe na wale wenye changamoto zingine wanaweza kutibiwa kwa tiba zingine wakapona,” amesema daktari huyo.

Hata hivyo, Tanzania ipo mbioni kuongeza bidhaa nyingine katika utalii wa matibabu kwa kuanzisha huduma za kibingwa za upandikizaji ogani hiyo, baada ya kufanikiwa katika upandikizaji figo kuanzia mwaka 2017, vifaa vya usikivu, uloto, mimba kwa njia ya IVF na huduma nyinginezo.

Akizungumza leo Novemba 24, 2024 jijini Dar es Salaam, Mkurugenzi Mtendaji wa MNH, Profesa Mohamed Janabi amesema tayari wameanza matayarisho kuelekea upandikizaji wa ini, ikiwa ni hatua ya utekelezaji wa azma ya Serikali ya kutoa huduma za ubingwa bobezi ili kusogeza huduma.

“Gharama ya upandikizaji ini nje ya nchi ni kati ya Dola za Marekani 25,000 hadi 27,000 (Sh66.4 milioni hadi Sh71.7 milioni) na fedha hizi zinajumuisha upandikizaji wa ini, kukaa hospitali na matibabu yote kwa mgonjwa na anayechangia ini,” amesema hata hivyo hakutaja gharama halisi kwa upandikizaji wa ndani.

Profesa Janabi amesema hospitali imeingia makubaliano na hospitali mbalimbali duniani zenye ujuzi huo ili kuanza matayarisho kwa kushirikiana na wataalamu wazalendo kuhakikisha ifikapo mwishoni mwa mwaka 2025, Tanzania inaanza kutoa huduma hiyo kwa kuwa miundombinu stahiki ipo na vifaa tiba vya uchunguzi.

“Wiki hii tumeshirikiana na watalaamu kutoka Hospitali ya Fortis ya nchini India ambao wamekuwa na madaktari wetu, kwa siku tatu wameona wagonjwa zaidi ya 100 wenye changamoto mbalimbali za magonjwa ya ini na kuthamini hali ya upatikanaji wa dawa, miundombinu ya maabara na ICU ambayo inakidhi mahitaji ya huduma hiyo,” amesisitiza Profesa Janabi.

Mwaka 2017 Muhimbili ilipeleka wataalamu saba nchini India kwa ajili ya mafunzo hayo, ambao tayari walirudi nchini na kuongeza ufanisi katika tiba ya magonjwa ya ini kwa kutoa mawe, kuzibua mifereji ya nyongo na kongosho iliyozibwa na uvimbe.

Miongoni mwa maswali mengi kutoka kwa watu ni mgonjwa yupi anayeugua ini anapaswa kupandikizwa, swali lililojibiwa na daktari bingwa wa magonjwa ya mfumo wa chakula na ini, John Rwegasha.

“Kupandikiza ini si kwa hatua za mwisho bali kwa hatua za awali za ugonjwa na kuzuia uharibifu wa ini zaidi kwa kuwafanyia upasuaji au kupandikiza ini,” amesema.

Daktari bingwa wa magonjwa ya mfumo wa chakula na ini Muhimbili, Swalehe Pazi amesema matibabu ya kawaida kwa mgonjwa yakishindikana, upandikizaji ni hatua inayofuata.

“Kupandikiza ini lazima kuna vigezo vinaangaliwa vikifikiwa tunafanya uchunguzi kwa anayetajiwa kuchangia ini kwa mgonjwa, kuna tiba za awali anapewa ili kuandaa mwili na ini husika.

“Kinachofanyika baada ya uchunguzi kwamba kipande cha ini kitakachotolewa kwa mchangiaji, kitakwenda kwa anayepewa bila kumletea madhara na afya yake iko vizuri, damu na vinasaba wameendana,” alisema Dk Pazi na kuongeza;

Magonjwa ya ini yana vyanzo mbalimbali ambavyo asilimia kubwa yanatokana na mitindo ya maisha katika matumizi ya vyakula, vinywaji au bidhaa zenye kemikali (sumu).

Matumizi makubwa ya vilevi na sigara, dawa zenye kemikali, virusi aina ya hepatitis A, hepatitis B, na hepatitis C, unene na uzito uliopitiliza, kurithi, kutokula au kunywa vitoa sumu mwilini kama maji pamoja na tatoo au kutoboa mwili.

Ikiwa ini litaharibika, utahitaji upandikizaji na ikiwa utapata mchangiaji ndugu gharama za upandikizaji hutegemea na hospitali na huanzia Dola 25,000 (Sh69.9 milioni) na iwapo utanunua katika soko la viungo thamani yake inafikia Dola 557,000 (Sh1.4 bilioni).

Hata hivyo, bado nchini utungwaji wa sheria ya uvunaji, usimamizi na utunzaji wa viungo vya ndani vya binadamu likiwamo ini unatarajiwa kusaidia kuanzishwa kwa benki za viungo nchini, hivyo kuboresha matibabu ya kibingwa.

Aina nyingi za magonjwa ya ini hazionyeshi dalili au dalili katika hatua za mwanzo. Dalili huonekana wakati ini tayari limeharibiwa au lina makovu.

Mgonjwa hujisikia uchovu wa kudumu, kupungua kwa hamu ya kula, kubadilika kwa rangi ya mkojo, rahisi kuvunjika hasa mifupa, kuvimba kwa mguu na kifundo cha mguu.

Nyingine ni kutapika, ngozi inayowaka au kung’aa sana, kuvimba na maumivu ndani ya tumbo, kinyesi kuwa na rangi ya lami au kama udongo, rangi ya njano ya macho na ngozi.

Related Posts