Biharamulo. Yalikuwa mauaji ya kikatili, ndio maelezo pekee unaweza kuyatumia kuelezea kitendo kilichofanywa na Pius Maliseri, cha kumghilibu mtoto Suzana Majaliwa (7) kwa kumnunulia muwa wa Sh200, kumbeba begani na kwenda kumuua.
Mwili wa mtoto huyo uliopatikana Machi 15, 2023 katika kichaka ndani ya Kijiji cha Nyamigere Wilaya ya Biharamulo mkoani Kagera, ulikutwa umekatwa viungo ambavyo ni ulimi, meno, mguu wa kulia na sehemu za siri.
Katika hukumu aliyoitoa Novemba 22, 2024 na nakala yake kupatikana katika tovuti ya mahakama leo Novemba 25,2024, Jaji Ferdnand Kiwonde amemuhukumu Pius Miseri adhabu ya kifo akisisitiza kwa alichokifanya, adhabu hiyo inastahili.
Ushahidi wa mashahidi wa Jamhuri wakiwamo waliomuona mshtakiwa akiwa amemnunulia marehemu muwa wa Sh200 na kumbeba na kuondoka naye, unaonyesha Miseri ndio mtu pekee na wa mwisho kuwa na marehemu.
Katika utetezi wake, mshtakiwa huyo alijitetea kuwa kabla ya tukio hilo, alikuwa akiishi Kijiji cha Kinyanzige Kata ya Kalenge na hakumbuki chochote kuhusiana Machi 15, 2023 ambayo ndio siku aliyomuua mtoto huyo.
Hata hivyo, alieleza kuwa mara ya mwisho kukutana na watoto wa Majaliwa ilikuwa eneo la Akajoli saa 10:00 alasiri na ni kweli aliwanunulia muwa kisha aliondoka na kuelekea eneo la Mwala kwa ajili ya kupata kinywaji.
Alijitetea kuwa alikaa huko hadi saa 1:00 usiku ambapo alirudi nyumbani lakini siku iliyofuata akiwa analima shamba la John Lutambi, alifika Busongoye Kagina na kumweleza miongoni mwa watoto aliowanunulia muwa, mmoja ametoweka.
Alieleza kuwa baada ya kumaliza shughuli za shamba, alirudi nyumbani na kukuta watu wamekusanyika nyumbani kwake ambapo watoto wake walimweleza kuwa watu hao walikuwa wakimtafuta mtoto huyo.
Aliamua kwenda eneo la Rugunzu kwa hofu kuwa watu wale wangemdhuru na siku iliyofuata alirudi nyumbani ambapo mkewe alimshauri akimbilie Kahama, ambapo alikwenda hadi alipokamatwa na Polisi na kurudishwa hadi kijijini.
Alipoulizwa maswali ya dodoso na wakili mwandamizi wa Serikali, Edith Tuka, mshtakiwa huyo alijibu kuwa mtoto Suzana Majaliwa alipotea siku aliyowanunulia muwa na baadaye kukutwa ameuawa, kisha akaomba msamaha.
Shahidi wa kwanza wa Jamhuri, Barnabas Mping’wa ambaye ni Ofisa Tabibu aliyeufanyia uchunguzi mwili wa marehemu, alisema sababu za kifo ni kuvuja damu nyingi kulikosababishwa na viungo muhimu vya mwili kuondolewa.
Kwa upande wake, shahidi wa pili, Isaya Benezeth ambaye ni Mwenyekiti wa Kijiji cha Nyamigere, alieleza kuwa Machi 16,2023, Majaliwa Kagina aliripoti kwake juu ya tukio la kupotea kwa mwanaye Suzan Majaliwa tangu Machi 15,2023.
Shahidi huyo alisema mzazi huyo alimweleza kuwa mwanaye alikuwa amechukuliwa na mshtakiwa huyo, ambapo alimshauri kuripoti suala hilo Polisi, lakini hakupokea ushauri huo akaendelea kumsaka mwanaye.
Badala yake, Machi 19, 2023 aliitisha kikao na wenyeviti wa vitongoji viwili vya Mkuyuni na Kinyanzige kwa lengo la kuweka mikakati ya kumtafuta mwanaye.
Hata hivyo, shahidi huyo alisema Machi 22, 2023, alipewa taarifa kuwa mshtakiwa alionekana eneo la Nyakanazi lakini siku hiyohiyo akaonekana Kahama mkoani Shinyanga ambapo Kazingo Lukaguza alimkamata na kumrejesha kijijini.
Mbali na hilo, shahidi huyo alisema Machi 23,2023 alijulishwa kuwa mwili wa marehemu umepatikana ambapo alikwenda eneo la tukio na aliuona ukiwa hauna ulimi, mguu wa kulia na sehemu za siri pia zikiwa zimekatwa.
Shahidi wa tatu, Yamola Majaliwa, aliieleza mahakama kuwa mara ya mwisho, yeye na marehemu walikuwa wakiangalia televisheni ambapo mshtakiwa alimnunulia Suzan muwa wa Sh200 na kuondoka naye na hakurudi nyumbani.
Mashahidi wengine ambao ni raia walielezea namna taarifa za kupotea kwa mtoto huyo zilivyoanza kusambaa na jina la mshukiwa kutajwa hadi alipokamatwa, huku polisi wao kwa upande wake wakielezea namna upelelezi wa tukio ulivyofanyika.
Baada ya kukamilika kwa ushahidi wa pande zote mbili, Jaji Kiwonde alichambua ushahidi wa Jamhuri na utetezi wa mshtakiwa na kumtia hatiani kwa kosa la mauaji ya mtoto huyo, akisisitiza kifo cha Suzana Majaliwa hakikuwa cha asili.
Jaji alisema kati ya mashahidi wote tisa wa Jamhuri, hakuna aliyeshuhudia mshtakiwa akimuua mtoto huyo, badala yake ulikuwa ushahidi wa mazingira, ambao hukubalika kama ushahidi endapo unakidhi vigezo.
Kulingana na Jaji, mashahidi wote ukimuondoa shahidi wa tatu wa Jamhuri walieleza kuwa mtoto huyo alichukuliwa na mshtakiwa Machi 15, 2023 na ndiye aliyekuwa mtu wa mwisho kuonekana naye kabla ya mwili kupatikana.
Jaji alisema wakati akijitetea, mshtakiwa alidai alikwenda Kahama kwa kuhofia hasira ya wananchi ambao walikuwa wamekusanyika nyumbani kwake, lakini akasema kama alikuwa hana hatia, asingekuwa na sababu yoyote ya kutoroka.
Jaji alisema ushahidi mwingine, ni jibu alilolitoa wakati wa maswali ya dodoso aliyoulizwa na wakili wa Serikali, Edith Tuka ambapo aliomba asamehewe kwa maelezo kuwa ana familia ya watoto watano na mke wanaomtegemea.
“Hii inaonyesha kuwa mshtakiwa aliomba msamaha kwa kosa la jinai alilolitenda. Kwa hiyo utetezi wake alinunua tu muwa akawapa watoto wa Majaliwa na kuondoka, lakini akatorokea Kahama haujatikisha ushahidi wa Jamhuri,”alisema.
Jaji alisema kitendo alichokifanya kilisukumwa na nia ovu kwa sababu baada ya kufanya tukio hilo alitorokea Nyakanazi na baadaye Kahama, kabla ya kukamatwa na mwili wa marehemu haukuwa na ulimi, mguu wa kulia na sehemu za siri.
“Katika maswali ya utetezi ilitaka kuonekana kama viungo hivyo vilikuwa vimeliwa na wanyama wakali, lakini uchunguzi wa baadhi ya viungo tu vya marehemu unanifanya niamini viungo hivi havikuondolewa na wanyama,”alisema Jaji.
Kutokana na ushahidi huo na ushahidi wa Jamhuri kwa ujumla wake, Jaji Kiwonde alimtia hatiani mshtakiwa kwa kosa la mauaji ya kukusudia na kueleza kuwa kwa mujibu wa sheria, adhabu ya kosa hilo ni moja nayo ni kunyongwa hadi kufa.