MWAMUZI kutoka Morocco, Samir Guezzaz ndiye atakayechezesha mchezo wa Ligi ya Mabingwa Afrika kati ya Yanga dhidi ya Al Hilal huku rekodi zake zikionekana kuwapa matumaini wenyeji.
Mchezo huo wa kwanza Kundi A kwa timu hizo, utachezwa kesho Jumanne Novemba 26, 2024 kwenye Uwanja wa Benjamin Mkapa, Dar es Salaam kuanzia saa 10:00 jioni, huku Gezzaz akisaidiwa na Zakaria Brinsi na Hicham Ait Abbou, huku Karim Sabry akiwa mwamuzi wa akiba (Fourth Official) ambapo wote ni raia wa Morocco.
Rekodi za mwamuzi huyo zinaonyesha kwamba, kila anapokuwepo uwanjani timu za nyumbani zimekuwa na matokeo mazuri tofauti na za ugenini jambo linaloweza kuipa faida zaidi Yanga kwenye Uwanja wa Benjamin Mkapa.
Samir amechezesha michezo 11 ya kimataifa ambapo kati ya hiyo timu za nyumbani zimeshinda minane, sare miwili huku zile za ugenini zikishinda mechi moja tu, na kati yake ametoa jumla ya kadi 40, za njano 39 na nyekundu moja.
Kama haitoshi, Al Hilal imekuwa na bahati mbaya na mwamuzi huyo kwani kwani timu hiyo kutoka Sudan imekuwa ikipata wakati mgumu pindi anapokuwepo uwanjani.
Rekodi zinaonyesha mwamuzi huyo ameweza kusimamia michezo minne ya Al Hilal na yote timu hiyo imeshindwa kupata matokeo ya ushindi.
Mchezo wa kwanza kuisimamia Al Hilal, Guezzaz alikuwa mwamuzi wa akiba ‘Fourth Official’ ambapo kikosi hicho kilichapwa mabao 3-1 dhidi ya Etoile du Sahel ya Tunisia ukiwa ni wa robo fainali ya kwanza ya Kombe la Shirikisho Afrika. Ulichezwa Aprili 7, 2019.
Pia akaichezesha Al Hilal ilipotoka suluhu na TP Mazembe ya DR Congo katika mchezo wa hatua ya makundi ya Ligi ya Mabingwa Afrika, Februari 24, 2021.
Baada ya hapo akasimamia tena timu hiyo katika raundi ya pili ya mchujo ya Ligi ya Mabingwa Afrika akiwa ni mwamuzi wa akiba ‘Fourth Official’, ambapo Al Hilal ilitoka sare ya kufungana bao 1-1 dhidi ya Rivers United ya Nigeria, Oktoba 17, 2021.
Mchezo wa mwisho kuichezesha Al Hilal ulikuwa wa hatua ya makundi ya Ligi ya Mabingwa Afrika kati ya timu hiyo dhidi ya Petro Atletico ya Angola ambapo kikosi hicho cha Sudan kilichapwa bao 1-0, mechi iliyopigwa Novemba 25, 2023.