KIRAKA wa Kagera Sugar, Nassoro Kapama amesema anatamani kucheza na Debora Fernandes, Awesu Awesu na Abdulrazak Hamza wa Simba kwani ni wachezaji wanaomvutia sana.
Nyota huyo aliyesajiliwa Simba lakini hakupata nafasi ya kudumu na kuondoka, alisema wachezaji hao ni kati ya wanaomvutia sana Ligi Kuu Bara.
Alisema kutokana na uwezo wake wa kucheza nafasi tofauti, anaamini angepata nafasi ya kucheza na mastaa hao, wangetengeza kombinesheni ambayo ingekuwa mwiba kwa timu pinzani.
“Japokuwa sipo Simba kwa sasa, ila wachezaji hatuna timu za kudumu tunaweza tukakutana popote na tukacheza pamoja na nikatimiza ninachokiwaza, ila nawakubali sana Debora Fernandez Awesu Awesu na Hamza kwa kile wanachokionyesha uwanjani.
“Kuhusu kiwango cha Simba, naiona msimu huu imejipanga na itafanya vizuri katika michuano ya CAF na Ligi Kuu Bara, imesajili vijana wengi ambao ni wapambanaji na tayari wameshaanza kuonyesha makali yao.”
Kuhusu malengo yake ya msimu huu, alisema anatamani kuona kiwango chake kinaisaidia Kagera Sugar na anaamini hilo litatimia kwa kujituma na kufanya mazoezi kwa bidii.
“Natamani kuisaidia timu iwe nafasi za juu kwenye msimamo wa Ligi Kuu, hilo ni kama deni kwangu na wachezaji wote kwa jumla,” alisema.