Kesi ya mauaji: Daktari akana ripoti ya awali, Jaji na mshtakiwa wang’aka

Dar es Salaam. Daktari bingwa wa magonjwa ya akili na ubongo, Sadiki Mandari amewasilisha ripoti kuhusu afya ya akili ya mshtakiwa Hamisi Luwongo anayekabiliwa na kesi ya mauaji ya mkewe Naomi Marijani katika Mahakama Kuu Masjala Ndogo Dar es Salaam huku akiikana ile ya awali.

Ripoti iliyoikana na ile iliyowasilishwa awali mahakamani hapo kutoka Hospitali ya Taifa ya Afya ya Akili Mirembe na kusainiwa na Dk Mandari inaonesha wakati mshtakiwa huyo anatenda kosa analotuhumiwa, alikuwa na tatizo la kiakili.

Dk Mandari (33) amewasilisha ripoti hiyo leo Jumatatu, Novemba 25, 2024 wakati akihojiwa na Jaji Hamidu Mwanga na jopo la waendesha mashtaka linaloongozwa na Wakili wa Serikali Mkuu, Yasinta Peter na wa utetezi, Hilda Mushi baada ya kuitwa kama shahidi wa Mahakama.

Mshitakiwa Hamisi Luogo (katikati). Picha na Maktaba

Akihojiwa kuhusiana na ripoti hiyo, Dk Mandari ambaye ni Mkurugenzi wa Huduma za Tiba ameieleza Mahakama ndiye aliyemfanyia uchunguzi mshtakiwa huyo.

Hata hivyo, amedai ripoti ya awali haitambui badala yake amewasilisha ripoti nyingine inayoeleza wakati mshtakiwa akitenda kosa hilo hakuwa na tatizo la kiakili bali alikuwa na akili timamu jambo lililomuudhi Jaji Mwanga.

“Kwa nini unaleta ripoti mbili tofauti? Kesi hii ni serious (nyeti), hapa kuna uhai wa mtu umepotea,” amehoji Jaji Mwanga na kueleza.

“Mimi hii (iliyowasilishwa mahakamani awali) sikuileta,” amedai Dk Mandari na alipozidi kubanwa kwa maswali akasema kuna mmoja wa ndugu wa mshtakiwa alimpigia aje aitetee ripoti iliyoko mahakamani.

Alipoulizwa na Jaji kama alimweleza huyo ndugu wa mshtakiwa kuwa anakwenda na ripoti nyingine alijibu hakumwambia na Jaji Mwanga alipomuuliza huyo ndugu wa mshtakiwa alijuaje kama anakwenda na ripoti nyingine alijibu kuwa hajui.

“Wewe ni daktari bingwa tena ni mkurugenzi halafu unafanya vitu kama hivi. Mahakama ikifanya uamuzi mnasema Mahakama haitendi haki,” amesema Jaji Mwanga kabla ya shahidi huyo kuendelea kuhojiwa na wakili Mushi.

Baada ya shahidi huyo kumaliza kuhojiwa mshtakiwa Luwongo alinyoosha mkono na akaomba nafasi ya kuongea akidai alikuwa na jambo la kusema na Mahakama ikampa nafasi hiyo.

“Mheshimiwa, kwanza nasikitika na ni aibu kubwa kwa taasisi inayoaminika na Serikali na nchi mzima kutoa taarifa mbili. Ya kwamba iliwasilishwa mahakamani kwa njia ya mtandao, siyo kwamba ilichukuliwa na askari magereza akatembea nayo mfukoni,” amesema mshtakiwa Luwongo.

“Na daktari bingwa amesema aliyokuwa nayo ndio bora zaidi. Nimemsikia daktari bingwa alipoulizwa na wakili Ashura (mwendesha mashtaka), kama aliona postmortem (ripoti ya uchunguzi wa chanzo cha kifo), kwenye file (jalada) langu akasema ndio. Lakini mheshimiwa hakuna ripoti ya uchunguzi maana maiti hakuna.”

Amesema ripoti iliyokuwa inatarajiwa kuthibitisha kifo cha mkewe ni ya mkemia lakini naye alishindwa na kwamba ana shaka kuwa upande wa mashtaka unaweza kwenda tena kwa mkemia akawasilisha taarifa nyingine kuwa majivu aliyofanyia uchunguzi ni ya Naomi.

Hata hivyo, Jaji Mwanga alimtoa wasiwasi kuwa hilo haliwezi kutokea.

Jaji Mwanga aliamuru mawakili wa pande zote kuwasilisha majumuisho ya hoja iwapo mshtakiwa ana hatia au la kufikia Desemba 10, na akapanga kutaja kesi hiyo Desemba 11, 2024 kwa ajili ya kupanga tarehe ya hukumu.

Katika kesi hiyo ya jinai namba 44/2023, Hamisi, mkazi wa Gezaulole, wilayani Kigamboni, jijini Dar es Salaam anakabiliwa na shtaka la mauaji ya mkewe Naomi Marijani kinyume cha kifungu cha 196 na 197 cha Sheria ya Kanuni ya Adhabu, kama ilivyorejewa mwaka 2019.

Anadaiwa alimuua mkewe huyo Mei 15, 2019 nyumbani kwao kisha akauchoma mwili wake kwa moto kwa kutumia magunia mawili ya mkaa ndani ya banda la kuku kisha akaenda kuyazika masalia ya mwili huo na majivu shambani kwake na kupanda migomba juu yake.

Novemba 18, 2024 baada ya upande wa mashtaka kufunga ushahidi wake kwa kuwaita mashahidi 14 na kuwasilisha vielelezo tisa, Mahakama hiyo ilimuona mshtakiwa kuwa ana kesi ya kujibu na hivyo kutakiwa kujitetea.

Wakili wake, Mushi aliijulisha Mahakama kuwa kuna amri ya Mahakama ya mshtakiwa kufanyiwa uchunguzi wa akili, ambayo ripoti yake ilisomwa mbele ya Mahakama Novemba 4 na ikawa sehemu ya mwenendo wa kesi hiyo na kwamba mshtakiwa ataitumia katika utetezi wake.

Baada ya mshtakiwa kufunga utetezi wake, wakili Yasinta aliiomba Mahakama iamuru daktari huyo aliyemfanyia uchunguzi wa akili mshtakiwa aitwe mahakamani ili wapate fursa ya kumfanyia mahojiano kuhusiana na ripoti yake hiyo na Mahakama iliridhia ombi hilo, ikaelekeza daktari huyo afike mahakamani jana.

Mshtakiwa katika utetezi alikana kumuua mkewe akidai kuwa mkewe hajafa bali alitoroka na kwamba taarifa alizowaeleza Polisi kuwa alimuua na kuchoma moto kisha hazikuwa za kweli.

Alidai kuwa aliwadanganya ili kujinusuru na mateso ya kipigo kutoka kwa askari polisi waliokuwa wakimtaka awaoneshe iliko maiti ya mkewe na kwamba masalia ya mifupa aliyokwenda kuwaonesha polisi shambani kwake si ya mkewe.

Alidai kuwa ilisalia kwenye kaburi lililohamishwa kwenye shamba lake lingine alilolinunua, huko Mwongozo Kigamboni na kwamba ndio maana hata uchunguzi wa kisayansi uliofanywa na Mkemia matokeo yake hayakutoa uthibitisho kuwa ni ya mkewe Naomi.

Related Posts