Kundi la Hezbollah larusha mkururo wa roketi Israel – DW – 25.11.2024

Mashambulizi hayo yamefanywa baada ya jeshi la Israel kuushambulia mji wa Beirut na kusababisha vifo vya makumi ya watu mwishoni siku moja kabla.

Jeshi la Israel limesema kundi la Hezbollah lilifanya mashambulizi ya mfululizo wa roketi kuelekea Israel jana Jumapili. Limeongeza kuwa nyumba kadhaa ziliharibiwa au kuteketea kwa moto wakati wa mashambulizi hayo yayonatajwa kuwa ni kisasi baada ya Israel kufanya mashambulizi yaliyosababisha watu 29 kuuwawa mjini Beirut huko Lebanon. 

Polisi nchini Israel imesema maeneo kadhaaa yameathiriwa na mashambulizi hayo kwenye eneo la Petah Tikvah, mashariki mwa Tel Aviv, na watu wanne wamepata majeraha. Kwa mujibu wa jeshi la Israel, kundi la Hezbollah lilishambulia kwa kutumia roketi 250 ambapo nyingi zilizuiwa.

Kundi la Hezbollah, ambalo awali liliapa kuyajibu mashambulizi ya Israel lenyewe limesema lilirusha makombora katika kambi mbili za jeshi mjini Tel Aviv na katika eneo jirani.

Mkuu wa sera za kigeni wa EU ziarani Lebanon

Hayo yanaendelea wakati Mkuu wa sera za Kigeni wa Umoja wa Ulaya Josep Borell akiwa ziarani katika mji Mkuu wa Lebanon, Beirut. Katika ziara hiyo, ambako amekutana na kufanya mazungumzo na Waziri Mkuu wa muda wa Lebanon Najib Mikati, Borell ametoa wito wa kuzishinikiza zaidi Israel na kundi la Hezbollah kufikia makubaliano ya usitishaji vita.

Amelalamikia kukwama kwa upatikanaji wa makubaliano hayo licha ya suluhisho kuonekana kukaribia kufikiwa mara kadhaa.

Borrell amesema kuwa, “Sijui ni upande upi unakuwa kizuizi, lakini sidhani kama kuna kitu kinachoweza kuhalalisha vita kuendelea hata kwa siku moja zaidi. Sioni sababu ya kuhalalisha maumivu kwa siku moja zaidi, na ninatumaini kwamba watu wasio na nia ya amani, na wanaoendeleza vita watawajibika kwa kile wanachokifanya.”

Libanon Josep Borrell in Beirut
Mkuu wa Sera za Kigeni wa EU, Josep Borrell akiwa na Waziri Mkuu wa muda wa Lebanon Najib Mikati mjini BeirutPicha: Mohamed Azakir/REUTERS

Hayo yanajiri wakati  balozi wa Israeli nchini Marekani Mike Herzog akisema kuwa, huenda makubaliano ya kusitisha vita yakafikiwa ndani ya siku kadhaa. Balozi huyo ameiambia redio ya jeshi la Israel kuwa vipengele kadhaa vimesalia ili kuhitimisha suala hilo na kuwa makubaliano yoyote yanahitaji idhini ya serikali.

Katika hatua nyingine, kiongozi wa ngazi ya juu wa Iran Ayatollah Ali Khamenei amesema kuwa viongozi wa Israel wanapaswa kupewa adhabu ya kifo na si waranti wa kuwakamata. Khamenei ameitoa kauli akizungumzia uamuzi wa  Mahakama ya Uhalifu wa Kivita ya ICC wa kutoa waranti wa kukamatwa kwa Waziri Mkuu wa Israel Benjamin Netanyahu, Waziri wa zamani wa Ulinzi wa Israel Yoav Gallant na Kiongozi wa Hamas Ibrahim Al-Masri.

 

Related Posts