Tarime. Miili ya watu wanane kati ya tisa wa familia moja waliofariki dunia kwa kusombwa na maji imeopolewa, huku jitihada za kuutafuta mwili mwingine zikiendelea.
Watu hao wamefariki dunia baada ya nyumba zao kusombwa na mafuriko yaliyosababishwa na Mto Mori ulio karibu na makazi yao kujaa maji, kufuatia mvua zinazoendelea kunyesha wilayani Tarime.
Tukio hilo limetokea usiku wa kuamkia leo Novemba 25, 2024 katika Mtaa wa Bugosi, Halmashauri ya mji wa Tarime mkoani Mara.
Mkuu wa Wilaya ya Tarime, Edward Gowele amesema juhudi za uokoaji zilianza baada ya tukio hilo na wamefanikiwa kuwaokoa watu wawili wakiwa hai na wanane wamepoteza maisha na mmoja anaendelea kutafutwa.
Amesema mkasa huo umezikumba familia mbili, moja ikiwa na watu tisa ambao wamenusurika na ya pili ina watu 11, wanane wameshafariki dunia mmoja bado hajapatikana na wawili wameokolewa wakiwa hai na wamelazwa Hospitali ya Wilaya ya Tarime kwa matibabu.
“Waliofariki taratibu za maziko zinafanywa na Serikali na maziko yanatarajiwa kufanyika kesho,” amesema Gowele.
Aidha, ametoa wito kwa wakazi waishio mabondeni kuhama ili kuepuka majanga kama hayo nyakati za mvua.
“Tulishatoa tahadhari watu wote waishio maeneo hatarishi wahame hasa kipindi hiki cha mvua kubwa,” amesema mkuu huyo wa wilaya.
Naye Edward Sokoine, baba wa familia iliyonusurika, amesimulia jinsi watoto wake walivyomwamsha baada ya kugundua maji yanakaribia nyumba yao.
“Tulitoka nje wakati maji yalikuwa tayari yameanza kubomoa ukuta wa nyumba. Tulinusurika kwa kupitia kwenye maji yaliyokuwa usawa wa magoti,” amesema Sokoine.
Mkazi mwingine aliyejitambulisha kwa jina la Zakaria Marwa, jirani wa familia zilizoathirika, amesema jitihada za haraka za majirani na vyombo vya usalama, zilisaidia kuwatoa manusura waliokuwa wamejishikilia kwenye mti. “Tulikuwa tunawatia moyo huku tukisubiri msaada wa vyombo vya uokozi vilivyofika kwa haraka,” amesema jirani huyo.
Tukio hili linaendelea kuwa somo kwa jamii kuhusu umuhimu wa kuchukua tahadhari na kuepuka kujenga nyumba za makazi kwenye maeneo hatarishi yakiwamo ya mabondeni.
Akisimulia jinsi mto huo ulivyofurika, Marwa amesema mvua ilinyesha maeneo ya juu ambako kuna chanzo cha mto huo ambao humwaga maji yake ndani ya Ziwa Victoria.
Amesema maji yalipofika maeneo ya kwao kutokana na kasi na wingi, yaliacha njia yake na kusambaa kwenye makazi ya watu na kusababisha baadhi ya nyumba kusombwa na maji.
Diwani wa Nyamisangura, Thobias Ghati amesema mbali na vifo, mafuriko hayo yamesababisha uharibifu na upotevu wa mali za watu wanaoishi pembezoni mwa mto huo.
Amesema miongoni mwa mali zilizoharibiwa na kusombwa ni pamoja na samani za ndani, vyakula na mazao ya mashambani yakiwamo mahindi, migomba na mihogo.
“Bado hatujajua thamani halisi ya mali zilizoharibika na kupotea, tathmini itafanyika baadaye kwa sasa tunahanagika kutafuta miili ya wenzetu waliosombwa na maji,” amesema diwani huyo.
Kaimu Kamanda wa Jeshi la Zimamoto na Uokoaji Mkoa wa Mara, Agostino Magere amewataja waliofariki dunia ni pamoja na Florence Okoth (55), Rebecca Ngari (24), Winfrida Otieno (22), Salome Akinyi (15), Stella Joel (25), Danny Joel (4), Toto Akinyi (12) na Fadhi Ngari (1).
Hata hivyo, mtoto aliyetajwa kwa jina la Ochola Joel (1) bado anatafutwa hajapatikana na miili yote imehifadhiwa Hospitali ya Wilaya Tarime.
Kamanda Magere amesema ujenzi holela usiozingatia utaratibu, ni chanzo cha tukio hilo huku akisema nyumba hizo zilijengwa jirani na mto kinyume cha utaratibu.