Arusha. Mtoto wa miaka 16 (jina limehifadhiwa) kutoka wilayani Monduli, Mkoa wa Arusha, amenusurika kifo baada ya kufanyiwa ukatili wa kupigwa na kujeruhiwa sehemu mbalimbali za mwili wake.
Mtoto huyo anadaiwa kuozeshwa na wazazi wake na kukatishwa masomo mwaka jana alipokuwa darasa la sita, katika shule moja eneo la Engaruka.
Kwa mujibu wa taarifa, tukio hilo lilitokea Novemba 19, 2024, mume wake alimfunga kamba kwenye mti na kumpiga kwa madai ya kukwepa majukumu ya ndoa, likiwamo la kubeba ujauzito.
Mtoto huyo alipata majeraha makubwa kabla ya kuokolewa na wasamaria wema kwa kushirikiana na Shirika la Kutetea Wanawake na Watoto (Mimutie).
Tukio hili limeibua mjadala mkubwa kuhusu ukatili wa kijinsia na haki za watoto, hasa wanaokatishwa masomo kwa ajili ya ndoa za utotoni.
Kwa mujibu wa taarifa iliyotolewa leo Jumatatu Novemba 25, 2024 na Waziri wa Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wanawake na Makundi Maalum, Dk Dorothy Gwajima, Serikali inafuatilia kwa karibu suala la matibabu ya mtoto huyo na upatikanaji wa haki yake ya kuishi kwa amani na usalama.
Aidha, Waziri Gwajima amewakumbusha wananchi kuwa ulinzi na usalama wa watoto ni jukumu la kila mmoja, hivyo washirikiane kuwalinda.
“Natoa onyo kali kwa jamii zinazoendeleza ukatili dhidi ya watoto kuwa waache vitendo hivyo kwani ni kinyume na sheria zinaazolinda watoto, hususani Sheria ya Mtoto sura ya 13 inayomlinda mtoto dhidi ya ukatili wa aina yoyote,” imesema taarifa hiyo.
“Na niwaombe wananchi wote kuendelea kutoa taarifa ya viashiria vya vitendo vya ukatili vinavyofanyika katika jamii kwa wakati ili hatua stahiki zichukuliwe. Mtoto huyo amefanyiwa ukatili kwa muda mrefu, lakini taarifa hazikutoka hadi alipolazimika kutafutiwa huduma za kimatibabu,” amesema Dk Gwajima.
Kwa mujibu wa Mkurugenzi wa Shirika la Mimutie, Rose Njilo, mwanafunzi huyo alikatishwa masomo mwaka jana na kulazimishwa kuolewa.
Akimnukuu mama mzazi wa binti huyo, Njilo amesema mtoto huyo alikatishwa masomo tangu mwaka jana baada ya baba yake kupokea mahari na kumuozesha kwa mwanaume huyo.
Amedai awali, binti huyo alikataa shule huku akitaja chanzo kuwa alipelekwa kwa mganga wa kienyeji ili achukie shule.
“Mtoto pia katuambia wazazi wake walimlazimisha kuolewa na mume ambaye amekuwa akimpiga na sababu kuu anasema anakwepa majukumu, eti kwanza alikuwa anakataa kuolewa na kuzaa, ndiyo huyo mume akachukua hatua ya kumfunga kamba kwenye mti.”
“Mtoto amepigwa sana, ameumizwa sana na tunalaani kitendo hiki, katika hizi jamii za pembezoni watoto wa kike wanapitia changamoto kubwa sana,” amesema Njilo.
Kwa upande wake Mkaguzi Msaizidi wa Jeshi la Polisi Kata ya Engaruka, Joseph Wilson amesema kitendo hicho hakikubaliki na wanachukua hatua.
“Jeshi la polisi linachukua hatua kwa sababu tumekuwa tukitoa elimu kwa jamii dhidi ya kuwalinda watoto na msimamo wa Polisi itahakikisha aliyefanya kitendo hiki anafikishwa kwenye vyombo vya sheria,” amesema.
Ofisa Mtendaji wa Kijiji cha Irendei, Josephine Shirima amesema wanaendelea kushirikiana na jamii kuhakikisha anayedaiwa kuhusika na kitendo hicho anakamatwa.
Hata hivyo, kuanzia leo Dunia imeanza kuadhimisha siku 16 za kupinga unyanyasaji wa kijinsia (GBV).
Kimataifa siku hizo huanzia Novemba 25 hadi Desemba 10 ya kila mwaka.
Tayari takwimu zinaonyesha kesi 29,373 ziliripotiwa polisi mwaka 2021 na kesi 6,305 sawa na asilimia 21.5 zilikuwa za kubakwa na asilimia 19.5 sawa na watu 5,751 na wanawake 20 walipata mimba za maharimu.