Nyumba za kupanga Dar zatajwa kuwa maghala ya dawa za kulevya

Dar es Salaam. Watu saba wanashikiliwa na Jeshi la Polisi kwa tuhuma za kukutwa na kilo 2,207.56 za aina mbalimbali na dawa za kulevya na dawa tiba zenye asili ya kulevya, huku nyumba za kupanga zikitumika kama maghala ya kuhifadhia dawa hizo.

Kufuatia hilo, Mamlaka ya Kudhibiti na Kupambana na Dawa za Kulevya Tanzania (DCEA) imewataka wamiliki wa nyumba kuwa makini na wanaowapangisha, ili kuepusha adhabu wanazoweza kukumbana nazo ikiwemo faini, kifungo au nyumba kutaifishwa.

Kwa mujibu wa Kamishana wa DCEA, Aretas Lyimo watuhumiwa hao walikamatwa katika mikoa ya Tanga na Dar es Salaam na katika dawa zilizokamatwa skanka ni kilo 1,500.6, methamphetamine kilo 687.76, heroin kilo 19.20 na chupa 10 za dawa tiba zenye asili ya kulevya aina ya Fentanyl.

Kupitia operesheni iliyofanikisha ukamataji wa dawa hizo, mamlaka imebaini wahusika wa biashara haramu ya dawa za kulevya hutumia mbinu ya kupanga nyumba ambazo zinageuza kuwa maghala ya kuhifadhi dawa za kulevya, huku wao wakiishi katika maeneo mengine.

“Mamlaka inatoa rai kwa wamiliki wa nyumba kuwa makini wanapopangisha nyumba zao, kwani nyumba inayotumika kwa shughuli za dawa za kulevya ni kinyume cha sheria na inaweza kutaifishwa,” amesema Lyimo, leo Jumatatu, Novemba 25, 2024 alipozungumza na waandishi wa habari jijini hapa.

Kwa mujibu wa Sheria ya Kudhibiti na Kupambana na Dawa za Kulevya, Sura ya 95, imeweka katazo kwa mmiliki au msimamizi wa nyumba, msimamizi wa eneo au chombo cha usafirishaji kuruhusu vitumike kwa lengo la kutengeneza, kuvuta, kujidunga, kuza au kununua dawa za kulevya.

Amesema mmiliki anapojua kuwa kosa linatendeka kwenye eneo lake, ana jukumu la kutoa taarifa kwa mamlaka.

“Kushindwa kufanya hivyo ni kosa la jinai, na akitiwa hatiani adhabu yake inaweza kuwa faini kuanzia Sh5 milioni hadi Sh50 milioni au kifungo cha miaka mitano hadi 30 jela au vyote kwa pamoja,” amesema.

Hii ni mwendelezo wa matukio mbalimbali ya ukamataji wa dawa za kulevya unaofanywa na DCEA ambapo Novemba 12, 2024 walifanikisha kukamatwa kilo 1,066.105 za dawa za kulevya, lita 19,804 za kemikali bashirifu, mililita 447 za dawa tiba zenye asili ya kulevya.

Kupitia operesheni hiyo kipindi cha Oktoba na Novemba, 2024 watuhumiwa 58 walitiwa mbaroni wakiwemo Kimwaga Lazaro (37) na Suleiman Mbaruku (52) anayefahamika kama Nyanda anayetajwa kuwa kinara wa biashara hiyo jijini Dodoma.

Siku hiyo, DCEA ilisema uchunguzi uliofanywa ulibaini wanawake ndio wateja wakubwa wa skanka ikidaiwa huitumia kupunguza msongo wa mawazo na kujistarehesha.

Skanka ni jina la mtaani linaloitambulisha bangi yenye kiwango kikubwa cha sumu (TetraHydroCannabinol – THC) ikilinganishwa na bangi ya kawaida.

Dawa hii ya kulevya hutokana na kilimo cha bangi mseto, asilimia 75 ni bangi aina ya sativa na asilimia 25 ni bangi aina ya indica.

“Katika uchunguzi wetu ambao tulifanya kwenye vijiwe, saluni na maeneo mbalimbali tulibaini watumiaji wakubwa wa skanka ni wanawake. Kuna ambao tulizungumza nao na hata mimi nimezungumza na baadhi ya wanawake wanakiri wanatumia skanka kujiondolea mawazo,” alisema Lyimo.

Katika mkutano wake leo Jumatatu, amesema Novemba, 14, 2024 Jiji la Dar es Salaam wilayani Kigamboni katika mtaa wa Nyangwale, walikamatwa watuhumiwa wawili ambao ni Mohamed Suleiman Bakar (40) na Sullesh Said Mhailoh (36).

Waliokamatwa jijini hapa ni wakazi wa Mabibo, Dar es Salaam na walikuwa na kilo 1,350.4 za dawa za kulevya aina ya skanka.

Dawa zilizokamatwa zilikuwa zimefichwa ndani ya nyumba aliyopanga mtuhumiwa Mohamed, ambayo aliitumia kama ghala la kuhifadhi dawa hizo.

“Dawa nyingine zilipatikana ndani ya gari aina ya Nissan Juke yenye namba za usajili T 534 EJC, zikiwa tayari kwa kusambazwa.

Tarehe hiyohiyo, katika mtaa wa Pweza Sinza E, wilaya ya Ubungo, jijini Dar es Salaam, mtuhumiwa Iddy Mohamed Iddy (46), mkazi wa Chanika Buyuni, alikamatwa akiwa na kilogramu 150.2 za skanka.

Amesema dawa hizo zilizokuwa zimefichwa katika maboksi ya sabuni na baadhi ya dawa hizo na nyingine zilikuwa kwenye boksi lililotengenezwa kwa bati ngumu na kupachikwa kwenye chasis ya gari aina ya Scania lenye namba za usajili wa Arika Kusini LN87XJGP.

Kwa mujibu wa Kamishna gari hilo lilikuwa likitumika kusafisha bidhaa mbalimbali kutoka nje ya nchi.

Mbali na watuhumiwa hao, Novemba 17, 2024, jijini Tanga, watuhumiwa Ally Kassim Ally (52) na Fahad Aly Kassim (56) walikamatwa mtaa wa Mwakibila wakiwa na kilo 706.96 za dawa aina ya heroin na methamphelanine.

Baadhi ya dawa hizo zilipatikana ndani ya gari aina ya Toyota Noah yenye namba za usajili T714 ECX na nyingine zikibainika kufichwa kwenye nyumba aliyopanga mtuhumiwa.

“Pia Novemba 19, 2024, katika Mtaa wa Kipata na Nyamwezi Kariakoo jijini Dar es Salaam, watuhumiwa Michael Dona Mziwanda (28) mkazi wa Tabata Segerea na Tumpale Benard Mwasakila (32) mkazi wa Temeke Mikoroshini, walikamatwa wakiwa na chupa 10 za dawa tiba zenye asili ya kulevya aina ya Fentanyl wakiwa nazo katika duka la kutoa na kuweka pesa,” amesema Lyimo.

Kupitia operesheni hiyo magari matatu na boti moja vilivyohusika katika uhalifu huo vinashikiliwa.

“Pia dawa zilizokamatwa ni nyingi na zingeweza kuwa na madhara makubwa kwa jamii na Taifa ikiwa zingeingia mitaani. Dawa hizi haziathiri tu wale waliokwishaanza matumizi ya dawa za kulevya, bali pia wafanyabiashara hawa hulenga watu wengine ambao hawajaanza matumizi ili kutanua masoko yao,” amesema Lyimo.

Amesema walengwa wapya wanaweza kuwa mtu yeyote katika jamii au familia za Kitanzania. Hivyo, ni dhahiri kuwa jamii nzima inakabiliwa na hatari ya dawa za kulevya.

Related Posts