Pamba Jiji yaanza na Yondani

PAMBA Jiji imeanza mchakato wa kuboresha kikosi chake kuelekea usajili wa dirisha dogo la usajili linalotarajiwa kufunguliwa Desemba 15 mwaka huu.

Inaelezwa kwamba, uongozi wa timu hiyo katika kuboresha kikosi ili kujinasua nafasi za chini kwenye msimamo, imekamilisha usajili wa beki mkongwe, Kelvin Yondani.

Taarifa za ndani ya timu hiyo zinasema Yondani amesaini mkataba wa mwaka mmoja akiwa mchezaji huru kwani tangu alipoachana na Geita Gold ulipomalizika msimu uliopita hakuwa na timu.

Pamba Jiji iliyopanda daraja msimu huu baada ya kupita takribani miaka 23, ipo nafasi ya 15 kwenye msimamo wa Ligi Kuu Bara, katika mechi 12 imeshinda moja, sare tano na kupoteza sita ikivuna pointi nane.

“Ukiachana na Yondani, tunafanya mazungumzo na wachezaji kutoka Simba na Yanga ambao tunawaomba kwa mkopo, bado tupo kwenye mazungumzo nao, hatujafikia mwafaka,” kilisema chanzo hicho.

Mwanaspoti linafahamu kwamba uongozi huo, umeanza kufanya mazungumzo na Yanga kwa ajili ya kumchukua mshambuliaji Jean Baleke kwa mkopo, wakiamini kwa aina ya uchezaji wake atawasaidia kufunga mabao.

Yanga ilimsajili Baleke msimu huu akitokea Al-Ittihad ya Libya alipokuwa akicheza kwa mkopo akiwa ni mchezaji wa TP Mazembe, pia amewahi kuitumikia Simba akiingia dirisha dogo msimu wa 2022-23 na kuondoka dirisha dogo msimu wa 2023-2024.

Related Posts