Sababu za kuimarika kwa shilingi dhidi ya dola

Dar es Salaam. Shilingi ya Tanzania imeimarika dhidi ya dola ya Marekani katika wiki za hivi karibuni hatua ambayo ni habari njema kwa wazalishaji wa viwandani, waagizaji wa magari na watumiaji wa mafuta, miongoni mwa wengine.

Takwimu rasmi kutoka Benki Kuu ya Tanzania (BoT) zinaonyesha kuwa, sarafu ya ndani imepanda thamani kwa karibu asilimia tatu katika kipindi cha mwezi mmoja uliopita.

Oktoba 25, 2024, BoT ilinukuu dola moja ikibadilishwa kwa Sh2,703.6/ Sh2,730.64; lakini hadi jana, thamani ya shilingi ilikuwa imeongezeka hadi Sh2,652.84/Sh2,652.1.

Kiwango cha wastani cha kubadilisha fedha kiliimarika kutoka Sh2,717.122 Oktoba 25 hadi Sh2,638.97 kufikia jana.

Kuimarika kwa shilingi kunatarajiwa kuleta utulivu au kupunguza gharama za bidhaa kubwa zinazoagizwa, ikiwa ni pamoja na bidhaa za mafuta, magari na vipuri vyake, sukari kwa matumizi ya viwandani, bidhaa za dawa, chuma na vyuma, pamoja na vitu vyote hivi, kwa kawaida huchangia sehemu kubwa ya gharama za uagizaji Tanzania.

Wachambuzi wanasema kuwa, sarafu imara ya ndani inaleta faida zaidi kuliko hasara kwa uchumi unaotegemea uagizaji kama wa Tanzania.

Takwimu rasmi zinaonyesha kuwa jumla ya uagizaji wa bidhaa na huduma za Tanzania ulifikia Dola 16.454 bilioni kwa mwaka uliomalizika Septemba 2024, kutoka Dola 16.103 bilioni mwaka uliopita. Ongezeko hili lilichangiwa zaidi na uagizaji wa mafuta yaliyosafishwa.

Kwa upande mwingine, mauzo ya bidhaa na huduma nje ya nchi yaliongezeka hadi Dola 15.353 bilioni katika kipindi hicho, ongezeko la asilimia 13.4 kutoka Dola 13.543 bilioni mwaka 2023.

Hii ilitokana zaidi na ongezeko la mapato ya huduma, hasa kutokana na utalii na mauzo ya dhahabu, tumbaku, korosho na bidhaa za kilimo cha bustani.

Profesa Semboja Haji kutoka Chuo Kikuu cha Dar es Salaam (UDSM) amebainisha kuwa mara nyingi shilingi huimarika dhidi ya dola ya Marekani baada ya mwaka wa kifedha kutulia.

Ameeleza kuwa misimu ya mauzo ya mazao makubwa ya kilimo na kipindi cha kilele cha utalii ni mambo muhimu yaliyosaidia kuimarika kwa mapato ya fedha za kigeni ya Tanzania, hivyo kuimarisha shilingi.

“Changamoto kwa uchumi wetu, kama ilivyo kwa mataifa mengine ya Afrika, ni kwamba kile tunachozalisha hakihitajiki sana na majirani zetu,” amesema Profesa Semboja.

“Hata hivyo, mambo ya msimu kama mauzo ya mazao ya kilimo na utalii yanaweza kusaidia kuimarisha sarafu ya ndani.”

BoT inatarajia mwenendo huu kuendelea, na matarajio ya kupungua kwa mahitaji ya dola ya Marekani, hali itakayoimarisha zaidi shilingi ya Tanzania kuelekea mwaka mpya wa 2025.

Kwa sasa, nchi ina akiba kubwa ya dola, na akiba hiyo inaendelea kukua.

 Kufikia Septemba 2024, akiba ya fedha za kigeni ya Tanzania ilikuwa Dola 5.414, bilioni kiasi kinachotosha kugharamia miezi 4.4 ya uagizaji wa bidhaa na huduma juu ya kiwango cha kitaifa cha miezi minne.

Gavana wa BoT, Emmanuel Tutuba, jana ameliambia gazeti dada la The Citizen kuwa mazingira ya kiuchumi ya kimataifa yamechangia nguvu ya shilingi hivi karibuni.

“Utulivu wa uchumi wa Marekani umesababisha kushuka kwa viwango vya riba, hali ambayo imehamasisha wawekezaji kutafuta fursa sehemu nyingine, hivyo kuongeza usambazaji wa dola duniani, ikiwamo Tanzania,” amesema.

Aidha, ameongeza kuwa, watu waliokuwa wakihifadhi kiasi kikubwa cha dola sasa wanazibadilisha kuwa shilingi za Kitanzania kwa ajili ya miamala ya ndani, hali inayoongeza usambazaji wa sarafu ya ndani.

Kwa jumla, kuimarika kwa hivi karibuni kwa shilingi ya Kitanzania kunatarajiwa kuongeza ushindani wa biashara za ndani, kuleta utulivu wa bei za bidhaa muhimu zinazoagizwa kutoka nje na kuimarisha ustahimilivu wa kiuchumi wa jumla wakati Tanzania ikiendelea kuhimili mabadiliko ya kifedha duniani.

Ripoti ya ziada na Rosemary Mirondo

Related Posts