Dar es Salaam. Dunia ikianza maadhimisho ya siku ya siku 16 za kupinga ukatili wa kijinsia (GBV) Chama cha Wanahabari Wanawake Tanzania (Tamwa), kimesema matumizi mabaya ya mitandao ya kijamii yameathiri jamii hasa wanawake na watoto.
Tamwa imesema wanawake na wasichana ndio mara nyingi wamekuwa walengwa wa picha zinazowadhalilisha mitandaoni, huku wanawake wanasiasa wakiwa waathirika wa unyanyasaji huo.
Unyanyasaji wa kijinsia (GBV) unarejelea vitisho au vitendo vyenye madhara vinavyoelekezwa kwa mtu binafsi au kikundi kulingana na jinsia yao, kimataifa siku hizo huanzia Novemba 25 hadi Desemba 10.
Kupitia taarifa kwa umma iliyotolewa leo Jumatatu, Novemba 25, 2024 na Mkurugenzi Mtendaji wa Tamwa, Dk Rose Reuben imesema matumizi mabaya ya mitandao ya kijamii yameathiri jamii na kundi hilo liko hatarini.
Pamoja na hayo, amesema wameona wanawake wanasiasa wakidhalilishwa mitandaoni hali inayochagiza kuacha kushiriki katika siasa au kugombea nafasi mbalimbali za uongozi kwenye jamii.
“Tamwa katika kipindi hiki cha siku 16 za kupinga ukatili wa kijinsia, ambacho pia kimeandamana na uchaguzi wa serikali za mitaa wa Novemba 27 mwaka huu, tunakemea udhalilishaji wa wanawake kwa kutumia mitandao ya kijamii.”
“Tunawahimiza wanawake na wasichana wanaogombea nafasi za uongozi katika uchaguzi huu kuwa imara na wastahimilivu ili waweze kutimiza malengo yao, wasiogope kutoa taarifa kwa mamlaka za kiusalama pindi wanapodhalilishwa mitandaoni au kwa namna yoyote ile,” amesema.
Dk Rose amesema katika taarifa hiyo kuwa kauli mbiu ya mwaka huu inalenga kuwakumbusha viongozi, wanaharakati na wadau wa masuala ya ukatili wa kijinsia hasa Serikali, sekta binafsi, kampuni na wananchi kwa ujumla kuungana na kuchukua hatua ili kumaliza ukatili.
Amefafanua kuwa wadau waungane kutokomeza ukatili kulingana na mapendekezo 12 ya mkutano wa Beijing yaliyolenga kutokomeza vitendo vya ukatili wa jinsia na kukuza usawa.
“Tumefanikiwa kupata sheria ya makosa ya kujamiiana ya SOSPA na tumefanikisha kuingizwa kwa kipengele cha rushwa ya ngono katika makosa yaliyo ndani ya sheria ya rushwa, lakini pia nafasi ya mwanamke katika ngazi za maamuzi ikiwemo siasa imeendelea kuongezeka,” amesema.
Siku 16 za kupinga ukatili wa kijinsia zinalenga kuikumbusha jamii kuhusu mienendo na mitazamo inayochagiza vipigo, ukeketaji, ubakaji, ulawiti, mimba za utotoni na rushwa ya ngono katika jamii.
Kadhalika, siku 16 zinatumika kutafakari kwa pamoja ni wapi palipofanikiwa, penye mapengo na ni kwa namna gani yatazibwa katika kupunguza ukatili wa kijinsia.
Kauli mbiu ya maadhimisho haya kwa mwaka huu ni ‘Kuelekea miaka 30+ ya Beijing: Tuungane kumaliza ukatili wa kijinsia kwa wanawake na watoto.’
Takwimu zilizotolewa na Jeshi la Polisi zinaonyesha kesi 29,373 ziliripotiwa Polisi mwaka 2021 ambapo kesi 6,305 sawa na asilimia 21.5 zilikuwa za kubakwa na asilimia 19.5 sawa na watu 5,751 na wanawake 20 walipata mimba za maharimu.
Mpaka Machi 2022 kutoka 2019 kesi 19,726 zilikuwa za ubakaji na GBV zilikuwa 27,838 huku watoto wachanga 443 walitupwa.