Kulingana na makadirio ya hivi punde, watoto sasa wanajumuisha hadi nusu ya wanachama wote wa vikundi vyenye silaha, na kuajiriwa kunachochewa na umaskini ulioenea, ukosefu wa elimu na kuporomoka kwa huduma muhimu.
“Watoto nchini Haiti wamenaswa katika mzunguko mbaya – wamesajiliwa katika vikundi vyenye silaha ambavyo vinachochea hali yao ya kukata tamaa, na idadi inaongezeka.,” alisema UNICEF Mkurugenzi Mtendaji Catherine Russell, akibainisha kuwa “machafuko na vitisho vimekuwa sehemu ya maisha ya kila siku”.
Chini ya tishio la mara kwa mara
Hali katika mji mkuu wa nchi hiyo, Port-au-Prince, inatisha kwa kiasi kikubwa, huku watoto milioni 1.2 wakiishi chini ya tishio la mara kwa mara la unyanyasaji wa kutumia silaha. Inakadiriwa kuwa asilimia 25 ya wakimbizi wote wa ndani 703,000 ni watoto, wanaoishi katika hali mbaya na kukabiliwa na vitisho vingi.
Kudorora kwa hali ya usalama kumesababisha kuongezeka kwa kasi kwa ghasia dhidi ya watu walio hatarini zaidi nchini Haiti. Ukatili wa kijinsia na ubakaji umekithiri, huku ripoti kutoka Ofisi ya Mwakilishi Maalum wa Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa kuhusu Watoto na Migogoro ya Kivita zikionyesha ongezeko mara kumi la watoto wanaokabiliwa na ukatili wa kijinsia mwaka huu pekee.
Mwaka huu, UNICEF ilitoa huduma za usaidizi, ikiwa ni pamoja na usaidizi wa kisaikolojia na uhamasishaji wa jamii kwa zaidi ya watu 25,000 walioathiriwa na unyanyasaji wa kingono na kijinsia mwaka 2024.
Juhudi za ulinzi na uokoaji
Katika kukabiliana na mzozo wa ulinzi unaowakabili watoto wanaoandikishwa na makundi yenye silaha au walio katika hatari ya kuajiriwa, UNICEF imetekeleza mipango kadhaa ikiwa ni pamoja na kutoa mafunzo kwa vikosi vya usalama na mashirika ya kiraia kuhusu hatua za ulinzi wa watoto. Pia hutoa huduma kwa wanajeshi watoto wa zamani, pamoja na usaidizi wa kisaikolojia na huduma za kuunganisha familia.
UNICEF inatoa wito kwa pande zote nchini Haiti kutanguliza ulinzi wa watoto, kuunga mkono kuachiliwa mara moja kwa watoto walioajiriwa na kuhakikisha haki zao ni muhimu kwa makubaliano yoyote.
“Watoto katika sehemu nyingi za Haiti hutendewa ukatili ambao mtoto hapaswi kamwe kutendewa,” akasisitiza Bi. Russell, akiongeza kwamba “huwaacha na makovu ya kiakili na kihisia ambayo huenda yakawasumbua maisha yao yote.”