Dar es Salaam. Afrika imetajwa kuwa na nafasi ya kufanya vema katika uchumi wa kidijitali iwapo itaunganisha nguvu katika uzalishaji wa simu janja, kwa ajili ya soko lake na kwingine.
Hayo yamebainishwa hivi karibuni na Mkurugenzi Mkuu wa Tume ya Tehama Tanzania (ICTC), Dk Nkundwe Mwasaga katika kilele cha kongamano la simu za mkononi kwa ajili ya Afrika lililolenga kuelekezea umuhimu wa kuongeza uzalishaji wa simu za kisasa za mkononi ndani ya Afrika.
Kongamano hilo liliandaliwa na Qhala, GSMA, Smart Africa na eneo la Biashara Huru la Afrika (AfCFTA) kwa ufadhili wa Taasisi za Bill & Melinda Gate lilifanyika Novemba 21 hadi 22, 2024 jijini Nairobi nchini Kenya.
Kilele cha kongamano hilo kiliwaleta pamoja wadau muhimu kutoka barani Afrika ikiwa ni pamoja na maofisa wa Serikali, viongozi wa biashara, waendeshaji wa mitandao ya simu, watengenezaji wa ndani na washirika wa maendeleo ya Kimataifa.
Akizungumza katika kongamano hilo, Dk Mwasaga amesema uzalishaji wa simu ndani ya Afrika licha ya kuwezesha wananchi wengi kuzimiliki skutokana na unafuu wa gharama pia utafungua fursa nyingi za ajira, kupaisha uchumi wa kidijitali ikiwemo kustawisha mapato ya Taifa.
Amesema kwa sasa, inakadiriwa chini ya asilimia 44 ya Waafrika wanamiliki simu za mkononi, jambo ambalo linadhihirisha ukosefu wa ufikiaji wa huduma za kidijitali, fursa za kiuchumi na maendeleo ya kijamii na kiuchumi.
“Vikwazo kama vile gharama za juu za uzalishaji, changamoto za kikodi na uwezo mdogo wa uzalishaji vinazuia simu za mkononi kuwa za gharama nafuu na kupatikana kirahisi,” amesema.
Amesema kuna haja ya kushughulikia changamoto kama vile za uchumi wa kiwango cha chini na vikwazo vya biashara katika kanda.
Aidha AfCFTA na itifaki zinasubiri kuleta mabadiliko katika mazingira ya kiuchumi ya Afrika kwa kukuza soko la kidijitali lililo na umoja.
Vilevile kuunganisha mifumo ya kisheria na kukuza ushirikiano wa mipaka kupitia AfCFTA, kunaweza kuhamasisha maendeleo ya vituo vya uzalishaji katika kanda na kupunguza gharama za uzalishaji wa simu za mkononi barani Afrika.
“Kupitia ushirikiano, ufumbuzi bunifu, na ushirikiano imara, kilele hiki kinakusudia kuweka msingi wa sekta ya uzalishaji wa simu za mkononi za ndani itakayokuwa na tija ya ukuaji wa kidijitali na kiuchumi wa Afrika kwa miaka ijayo.”
Malengo ya kongamano hilo
Miongoni mwa malengo ya kongamano hilo ilikuwa ni kuchunguza mikakati ya kuongeza uzalishaji wa simu za mkononi za ndani kote Afrika, kwa kushughulikia vikwazo vikiwamo gharama za juu za uzalishaji, vikwazo vya kisheria na upatikanaji mdogo wa vifaa.
Vilevile, kuwezesha ushirikiano wa kikanda katika uzalishaji wa simu za mkononi, usambazaji, vumbuzi, kuunda vituo vya kikanda na kukuza ushirikiano wa mipaka.
Malengo mengine ni kusaidia mafunzo kutoka nchi zinazopiga hatua katika mabadiliko ya kidijitali, kama vile Rwanda na Misri.
Nchi hizo zimeanzisha sera za kisasa za ushirikiano wa umma na binafsi ili kuimarisha uzalishaji wa ndani na ukuaji wa kidijitali.
Sambamba na kuunganisha sera na mifumo ya kisheria kati ya mataifa ya Afrika ili kupunguza vikwazo vya biashara, kurahisisha taratibu za forodha na kuwezesha biashara ya mpakani kwa simu za mkononi zilizotengenezwa ndani.