Wafanyabiashara wa Kariakoo wafikiria kuhama, wengine wakilia ukata

Dar es Salaam. Baada ya kuporomoka kwa jengo eneo la Kariakoo, baadhi ya wafanyabiashara wakubwa wanafikiria kuhama eneo hilo kwenda sehemu nyingine,  ili kulinda uendelevu wa biashara na uhai wa mitaji yao.

Miongoni mwa sababu za kuhama kwao ni hofu ya usalama wao na mali zao wakisema miundombinu katika eneo hilo, hairidhishi na majengo mengi hayana bima jambo ambalo ni hatari inapotokea changamoto.

Baadhi ya wafanyabiashara waliozungumza na Mwananchi wanaeleza kuwa eneo wanaloweza kuhamia sasa ni Sinza, Kinondoni na Makumbusho huku wakijipa moyo umaarufu walioujenga kwa muda mrefu utawabeba.

Wafanyabiashara hao wanaonyesha nia hiyo katika kipindi ambacho shughuli za uondoaji kifusi kwenye ghorofa lililoporomoka Novemba 16 mwaka huu na kusababisha vifo vya watu 20 na majeruhi karibu 100, zikiendelea huku eneo hilo likiwa chini ya ulinzi.

“Wafanyabiashara wakubwa wanakuwa na mawazo ya kufikiria kuhama kuliko wadogowadogo, fikiria kama mtu alikuwa na stoo ya mzigo katika jengo lililoanguka wote umepotea,” amesema Emmanuel Lameck

Lameck ambaye ni mfanyabiashara wa eneo hilo amesema majengo mengi hayajakatiwa bima na ikitokea changamoto hajui atairudishaje.

“Miundombinu kama ya uokozi mathalani ikitokea ajali ya moto au maafa ya kuporomoka jengo inakuwa ngumu. Sasa jengo lililoporomoka lilikuwa ghorofa tatu na waliokufa ni wengi sasa lingekuwa refu ingekuwaje,” amesema

Amesema licha ya eneo hilo kuwa na tija lakini tukio hilo limewashtua wafanyabiashara wengi wenye mitaji mikubwa.

“Mfanyabiashara mkubwa anaangalia sehemu yenye usalama wa mtaji wake kama miundombinu mibovu hawezi kukaa bora akafanye shughuli zake hata Ubungo kwakuwa ameshajenga jina wateja watakuja,” amesema.

Hoja hiyo  iliungwa mkono na Chacha Abedaus aliyesema kuna wanaofikiria kuhama kwenda kufanya mazingira mengine kuepuka changamoto zinazojitokeza hasa za kufungwa kwa baadhi ya mitaa.

“Kiuhalisia biashara zimesimama kwa sasa kwa eneo kama la Kariakoo kinachotegemewa zaidi ni mzunguko wa watu sasa kunapokuwa na vizuizi kila kona inaumiza wengi,” amesema.

Abedaus anayefanya biashara ya simu mtaa wa Msimbazi, amesema kuna baadhi wameanza kukimbilia Sinza na Kinondoni ili kujaribu kurudisha uhai wa biashara zao.

“Mfanyabiashara siku zote anajali shughuli zake kufanya kazi siku zote bila changamoto hata Serikali inaposema itakagua majengo kiusalama,  ni sawa lakini unaposema utavunja majengo inakuwa hofu kwao,” amesema.

Amesema kipindi hiki cha mwisho wa mwaka kwa hali inayoendelea kutokea ni hasara kubwa kuna watu walioagiza mizigo ya mamilioni ya fedha na  yeye alijipanga kuuza msimu wa sikukuu lakini amesimamishwa baada ya ajali hiyo.

“Madhara yake hayawezi kuonekana sasa lakini ukweli ni kwamba kuanzia Januari hadi Februari hawawezi kuwa na nguvu ya kufanya kazi hasara, itakuwa kubwa,” alisema.

Hata hivyo,  maoni hayo yalitofautiana na Mussa Ligwa ambaye ni mfanyabiashara wa eneo hilo, aliyesema watu hawawezi kuhama kutokana na umuhimu wa kuwa na wateja wengi muda wote.

“Hivi sasa wengi hasa tunaotoka mitaa iliyofungwa tupo nyumbani,  hatufikirii kuhama tunasubiri waokoaji wamalize shughuli zao na tutarejea katika maeneo yetu na kufanya kazi kama kawaida,” alisema.

Ligwa amesema kazi yoyote kukutana na changamoto ni kawaida,  lakini huwa wanaangalia itakula muda kiasi gani.

Mfanyabiashara mwingine, Vicent Mzomboki alisema kutokana ukubwa wa biashara Kariakoo,  ni vigumu mfanyabiashara kufikiria kwenda kufanya shughuli zake sehemu zingine.

“Haiwezekani kwenda kutafuta riziki sehemu nyingine na haitakuja kutokea kwa sababu faida ya Kariakoo ni kubwa kuliko hasara. Kariakoo ina wepesi wa kila kitu ikiwemo kupata wateja,” alisema.

 “Kariakoo kumechangamka tangu nchi kupata uhuru,  ni vigumu kubadilisha utamaduni huo. Wengi wanaofungua Sinza na Makumbusho  wanajifunza Kariakoo,” alisema.

Alisema kuna majengo ambayo yamechoka ambayo hayafiki 50 hata ukiangalia kwa macho yanajulikana yanatikiwa yapishe ujenzi mpya na hata mabadiliko hayo yakitokea hayawezi kuathiri chochote.

“Kariakoo lazima ulipe kodi kuanzia mwaka wa kwanza na wengi wanaangalia sehemu salama ya kuwekeza na kodi inaanzia Sh2 milioni na jengo likiwa hatarishi wengi hawawezi kuingia,” amesema.

Mwananchi jana ilishuhudia shughuli ya uondoaji wa vifusi vya udongo katika ghorofa lililoporomoka  ikiendelea na baadhi ya maeneo wafanyabiashara walikuwa wakiendelea na kazi zao.

Kufuatia ajali ya Novemba 16, 2024, Serikali ililiweka eneo la jengo na makutano ya kuelekea mtaa huo chini ya ulinzi kwa kuvikabidhi vyombo vya usalama kusimamia kupisha shughuli za uokoaji, ili kuangalia hadi chini kama iwapo kutakuwa na mwili uliobakia.

Mwananchi imefika eneo hilo na kushuhudia magari yakipishana yanayoingia na kutoka na kifusi lakini katika eneo hilo hakuna raia wa kawaida anayeruhusiwa kuingia kwa kuvuka maeneo yote yaliyozungushiwa utepe.

Katika maeneo yote yaliyozungushiwa utepe,  huo kuna askari polisi pamoja na wanajeshi na ukiangalia kwa mbali kuna magari yao na watumishi wengine waliovalia mavazi ya uokoaji wakiwa kwenye pilikapilika za hapa na pale.

Nje ya maeneo yaliyozungushiwa utepe biashara zinaendelea kama kawaida kwa wafanyabiashara kuuza bidhaa mbalimbali kwa wateja wanaohitaji mahitaji.

Mfanyabiashara wa nguo za watoto Ally Mustafa, amesema biashara zinaendelea lakini si kwa kiwango walichokizoea.

“Unajua tukio hili la kuporomoka jengo limesababisha wateja kwa kiwango kikubwa kupungua hapa Kariakoo, hasa wakisikia baadhi ya maeneo yamefungwa,” alisema.

Ally anajipa moyo kuwa shughuli ya uondoaji kifusi kwa eneo lililozuiliwa inaendelea kwa kasi, akiamini shughuli zitarejea kwa kasi yake.

“Ingawa si haba walau sisi tunaendelea na biashara lakini wenzetu walio jirani na mtaa uliofungwa hali si nzuri, maana hakuna biashara inayofanyika katika eneo hilo,” alisema

Mfanyabiashara mwingine, Jerome Sanga alisema biashara yake ya nguo huwa anawauzia zaidi watu wanaotoka mikoani na nje ya nchi,  lakini baada ya kutokea maafa wateja wake hawaji.

“Wanaamini hakuna biashara inayoendelea na kama unavyojua watu tuna hofu wengi wanasubiri shughuli ya uokoaji iishe ndipo waje,” alisema .

Wakati wakieleza hayo, Salim Abdallaha kwake mambo ni tofauti alisema tangu aingize mzigo wake wa nguo  kutoka nje ya nchi hajafungua wala kuuona.

“Mzigo wangu uliingia Novemba 15, jioni na shughuli zangu nafanyia mtaa huo uliofungwa sijaufungua wala kuangalia. Najitahidi kuomba kwa askari niingie lakini masharti yamekuwa mengi,” alisema.

Baadhi ya wateja wamesema kwa sasa bado hawana uhuru baada ya kufungwa mtaa huo.

“Natokea Mvomero Morogoro nina wiki sasa nilikuja kufunga mzigo na duka ninalochukua lipo katika mtaa uliofungwa na shughuli hazifanyiki imekuwa shida nimekuja hapa asubuhi nilidhani patafunguliwa lakini mambo kama unavyoona,” alisema.

Naye Sophia Mashaka alisema shughuli zinaendelea lakini kufungwa  kwa mtaa huo,  wanapata usumbufu kupata mahitaji.

Related Posts