Waliofanya vizuri Swalle cup kupelekwa na wizara kufanya majaribio timu za Championship waziri Dkt.Ndumbaro aeleza

Waziri wa Utamaduni,Sanaa na Michezo Dkt.Damas Ndumbaro amesema wizara kwa kushirikiana na mbunge wa jimbo la Lupembe mkoani Njombe Edwirn Swalle inakwenda kutoa fursa kwa vijana wenye vipaji kwenda kufanya majaribio katika timu zinazoshiriki ligi ya championship kwa lengo la kukuza zaidi vipaji vyao na kujipatia ajira.

Dkt.Ndumbaro ameeleza hayo mara baada ya kutazama na kuridhishwa na vipaji vya vijana wakati akifunga michuano ya Swalle Cup Jimbo la Lupembe inayodhaminiwa na mbunge wa jimbo la Lupembe Edwirn Swalle,michuano ambayo imefungwa katika kata ya Kidegembye wilayani Njombe.

“Wizara yenye dhamana ya utamaduni tunasema wale wachezaji watakaopata tuzo tutawapeleka katika timu za Championship wakafanye majaribio,tutashirikiana na Mh Swalle kuwapatia fursa vijana hawa ili waende wakafanye majaribio”amesema Dkt.Ndumbaro

Dkt.Ndumbaro ameongeza kuwa “Micheo sio tu afya bali pia ni ajira kupitia michezo hii wengi mtapata ajira na pongezi mhimu sana zimuendee mbunge Edwirn Swalle kwa kuandaa michezo miaka minne lakini kwa kuandaa zawadi nzuri”

Kwa upande wake mbunge wa Lupembe Edwirn Swalle ameishukuru Wizara kwa kuona umuhimu wa michezo mpaka vijijini jambo ambalo wananchi wa Lupembe wameona ushirikiano uliopo baina ya mbunge wao na serikali kwa kuendelea kutekeleza ilani ya Chama cha Mapinduzi (CCM)

“Mh Waziri umetupa heshima sana watu wa Lupembe na kipekee umewapa hewshima wana michezo walioko hapa kwa kuja kushuhudia vijana wako lakini kipekee pia umeniheshimu mimi Mbunge wenzako”amesema Swalle

Israel Mhada ni katibu wa mbunge wa jimbo la Lupembe amesema michuano ya Swalle Cup imeendelea kupiga hatua tangu ilipoanza mwaka 2021ambapo kwa sasa imefikia msimu wa nne huku ikiwa na mafanikio makubwa ikiwemo kuimarisha umoja na mshkamano wa jamii ya watu wa Lupembe pamoja na kuzalisha ajira za muda mfupi,huku pia akiongeza kuwa bingwa wa michuano hiyo msimu wa 2024 ameweza kujinyakulia kitita cha shilingi laki tano na Ng’ombe mwenye thamani ya Milioni moja na laki tano,Jezi ,kombe,medali na mpira wa viwango vya Fifa.

Katika michuano hiyo kwenye fainali iliyozikutanisha timu ya Ikuna FC pamoja na Matembwe FC,dakika tisini zimekamilika kwa timu ya Ikuna fc kuibamiza mabao mawili kwa sifuri na kutawazwa kuwa bingwa michuano ya Swalle Cup msimu wa 2024.

Related Posts