Wapinzani wa Yanga yawakuta CAF

SHIRIKISHO la Soka la Afrika (CAF), kupitia Kamati ya Nidhamu, limechukua hatua kali dhidi ya wapinzani wa Yanga kwenye Ligi ya Mabingwa, MC Alger kutokana na vitendo visivyoridhisha vya mashabiki wa timu hiyo wakati wa mechi ya kufuzu hatua ya makundi dhidi ya US Monastir.  

Kwa mujibu wa uamuzi DC23173 uliotolewa Novemba 24, 2024, MC Alger ya nchini Algeria imetozwa adhabu ya kucheza mechi zao nne za nyumbani za michuano ya CAF bila mashabiki, huku kukiwa na masharti ya kutofanya kosa lolote ndani ya miezi 12 ijayo.  

Hii inamaanisha kuwa katika hatua ya makundi ya Ligi ya Mabingwa Afrika, MC Alger iliyopangwa Kundi A itacheza mechi zake za nyumbani bila uwepo wa mashabiki wake uwanjani dhidi ya Yanga (Desemba 7, 2024), Al Hilal (Desemba 14, 2024) na TP Mazembe (Januari 10,2025).

Adhabu hii imekuja baada ya mashabiki wa MC Alger kujihusisha na vitendo visivyo vya kiungwana wakati wa mechi ya marudiano kuwania kufuzu makundi dhidi ya US Monastir Septemba 21, 2024.

Mchezo huo uliomalizika kwa MC Alger kushinda mabao 2-0, uliwawezesha kubadili matokeo ya kipigo cha 1-0 walichopata kwenye mchezo wa kwanza ugenini na kufuzu hatua ya makundi. Hata hivyo, furaha ya ushindi huo iligubikwa na matukio yasiyofaa kutoka kwa mashabiki wa timu hiyo.

Zaidi ya adhabu hiyo, MC Alger pia imetozwa faini ya dola za Marekani 50,000 (Sh132.5 milioni), ambazo inapaswa kulipa ndani ya siku 60 tangu ilipofikishiwa taarifa hiyo.  

Caf imeeleza kuwa hatua hizi zinakusudia kukomesha matukio kama hayo na kuimarisha maadili ya soka safi na heshima katika mashindano ya Afrika. Klabu hiyo imetakiwa kutii maelekezo hayo na kuhakikisha kuwa haivunji tena kanuni za mashindano, ili kuepuka adhabu kali zaidi.  

Pia Caf itafuatilia kwa karibu utekelezaji wa adhabu hizo, huku ikitarajia MC Alger kuboresha mwenendo wake ndani na nje ya uwanja ili kurejesha hadhi yake katika mashindano ya soka barani Afrika.

Related Posts