BAADA ya ushindi wa bao 1-0 dhidi ya Tanzania Prisons, Kocha Mkuu wa JKT Tanzania, Ahmed Ally amefurahishwa na safu yake ya ushambuliaji kuanza kutengeneza nafasi nyingi huku akiamini kwamba ipo siku timu pinzani zitafungwa mabao mengi.
Licha ya kupachika bao moja katika mchezo huo wa Ligi Kuu Bara uliochezwa juzi kwenye Uwanja wa Meja Jenerali Isamuhyo, Dar es Salaam, kocha huyo ameliambia Mwanaspoti kuwa ni mwanzo nzuri kwao kwani timu imeashaanza kutengeneza nafasi nyingi tofauti na mechi zilizopita.
“Nawapongeza wachezaji wangu kwa kuonyesha mabadiliko makubwa, ni kweli tumeshinda bao moja licha ya kutengeneza nafasi nyingi haikuwa rahisi kutokana na ugumu kutoka kwa wapinzani,” alisema na kuongeza:
“Safari moja huanzisha nyingine, ushindi huu mwembamba tulioupata una picha mbili kwangu, kwanza washambuliaji wamenionyesha kuwa wanaelewa kile ninachokifundisha, pili kuhusu kutumia nafasi ni zoezi ambalo litakuwa endelevu.”
Ahmed alisema timu yake ilitengeneza nafasi zaidi ya nane lakini ilitumia moja ambayo Hassan Kapalata alifunga bao pekee dakika ya pili, hivyo kwake sio mbaya akiamini kwamba itafika wakati kila nafasi watakayotengeneza itakuwa bao.
Akizungumzia mchezo kwa ujumla, alisema haukuwa rahisi kutokana na kukutana na timu ambayo inacheza mpira wa aina moja na timu yake hivyo mbinu binafsi ndio zimeamua matokeo hayo.
“Ulikuwa mchezo mgumu na wa ushindani timu zote zinacheza mchezo wa nguvu na kasi hivyo kila upande ulijaribu kutafuta pointi tatu muhimu sisi tulikuwa bora zaidi na ndio maana tulipata pointi hizo tatu muhimu,” alisema.