Dar es Salaam. Msajili wa Jumuiya za Kidini na Vyama vya Kijamii, Kabidhi Wasihi Mkuu, Mwanasheria Mkuu wa Serikali (AG), Baraza la Kuu la Waislamu Tanzania (Bakwata) na Wadhamini wa Baraza Kuu la Jumuiya na Taasisi za Kiislamu Tanzania, wamewawekea pingamizi baadhi ya Waislamu waliowafungulia kesi ya Kikatiba, baada ya kila mmoja kuiomba Mahakama Kuu Masjala Ndogo Dar es Salaam isiisikilize kesi hiyo.
Baadhi ya Waislamu hao wakiwamo masheikh wamefungua kesi hiyo wakipinga sharti la kutambuliwa Bakwata katika usajili wa taasisi zao.
Waliofungua kesi hiyo ni Sheikh Ayoub Salim Muinge, Sheikh Profesa Hamza Mustafa Njozi, Sheikh Ponda Issa Ponda na wenzao wengine tisa akiwamo mwanamke pekee Riziki Shahari Ngwali.
Katika hati ya madai, wadai wanapinga kitendo cha msajili wa jumuiya na vyama hivyo na Kabidhi Wasihi Mkuu kuwalazimisha kuwa na barua inayowatambulisha kutoka Bakwata katika kusajili taasisi yoyote.
Hata hivyo, wadaiwa hao ikiwamo Bakwata wameibuka na mapingamizi dhidi ya kesi hiyo wakiiomba Mahakama isiisikilize huku wakibainisha sababu mbalimbali za kisheria.
Mapingamizi hayo yamebainishwa na mawakili wa wadaiwa hao, leo Jumanne, Novemba 26, 2024, wakati kesi hiyo inayosikilizwa na Jaji Anold Kirekiano ilipotajwa mahakamani hapo kuangalia kama wadaiwa wameshawasilisha majibu ya madai hayo.
Wadai hao wamewakilishwa na jopo la mawakili wao likiongozwa na Juma Nassoro, Yahya Njama na Ubaidu Hamidu huku AG ikiwakilishwa na Wakili wa Serikali Mwandamizi, Edwin Webiro na Bakwata ikiwakilishwa na Wakili Hassan Fatiu.
Wakili Webiro ameieleza Mahakama kuwa, tayari wameshawasilisha kiapo kinzani kujibu madai hayo sambamba na taarifa ya pingamizi la awali na kwamba tayari wameshawakabidi upande wa wadai.
Katika pingamizi, AG amebainisha hoja tatu, kwanza ikidai wadai hawakupaswa kufungua kesi ya Kikatiba bali walipaswa kutumia njia mbadala kutafuta nafuu wanazoziomba.
Sababu ya pili amedai kuwa wadai hawajaonesha namna walivyoathirika na kauli wanazozilalamikia na kwamba hati ya kiapo kinachounga mkono hati ya madai ina kasoro za kisheria kwa kujumuisha taarifa zizisopaswa kuwamo, kama maoni na hoja.
Kwa upande wa Bakwata, wakili Fatiu pia ameieleza Mahakama kuwa kwa upande wao pia wameshawasilisha kiapo kinzani pamoja na taarifa ya pingamizi la awali.
Hata hivyo, kwa upande wa Baraza la Taasisi na Jumuiya za Kiislamu, Jaji Kirekoano baada ya kuangalia kwenye mfumo amesema wamewasilisha majibu yao (kiapo kinzani) nje ya muda.
Baada ya kujadiliana na mawakili wa pande zote wakakubaliana kuwa hoja ya majibu ya baraza hilo kuwasilishwa nje ya muda itajadiliwa kwa tarehe nyingine ambayo pia ndio Mahakama itapanga tarehe ya kusikiliza mapingamizi hayo.
Hivyo, Jaji Kirekiano ameahirisha kesi hiyo mpaka Desemba 10, 2024 asubuhi kesi hiyo itakapotajwa kwa ajili ya taratibu hizo.
Kwa mujibu wa madai ya wadai katika kesi hiyo sharti hilo linawalazimisha kuwa chini ya Bakwata wakati hakuna sheria inayowalazimisha Waislamu wote kuwa chini ya Bakwata, ambayo yenyewe pia imesajiliwa Wizara ya Mambo ya Ndani na katika Wakala wa Usajili, Udhamini na Ufilisi (Rita).
Wanadai kuwa Bakwata pia imesajiliwa kama taasisi nyingine zilizosajiliwa, haina usajili wa kuwa taasisi ya kuwawakilisha Waislamu wote nchini na kwamba hata Katiba yake hakuna kipingele kinachobainisha ni nani mwanachama wa Bakwata.
Hivyo, wanadai kuwa sharti hilo la kuwalazimisha Waislamu wote kuwa kutambuliwa na Bakwata ni kinyume na Katiba bali wanapaswa waulizwe wao wenyewe kuwa wanataka taasisi gani iwatambue.
Hivyo pamoja na mambo mengine wadai wanaiomba Mahakama hiyo itoe amri na tamko kuwa mwenendo na masharti yaliyowekwa na Msajili wa Jumuiya na wa pili, Kabidhi Wasihi Mkuu, katika usajili wa jumuiya na taasisi ni ukiukwaji wa Katiba.
Wamebainisha kuwa masharti hayo yanakiuka ibara za 13 (1), (2) na (3); 19(1) na (2); 20(1); 29(2) za Katiba ya nchi.