Musoma. Hospitali ya Rufaa ya Mkoa wa Mara ya Kumbukumbu ya Mwalimu Nyerere inakabiliwa na upungufu wa magari mawili ya kubebea wagonjwa hali inayokwamisha utoaji wa huduma kwa wagonjwa.
Kauli hiyo imetolewa mjini Musoma jana Jumatatu Novemba 25, 2024 na Mganga mfawidhi wa hospitali hiyo, Osmumd Dyegura alipokuwa akipokea gari la kubeba wagonjwa lililokabidhiwa hospitalini hapo na mbunge wa Musoma Mjini (CCM), Vedastus Mathayo.
Dk Dyegura amesema hospitali hiyo ina jumla ya magari matano ya wagonjwa ambayo hayakidhi mahitaji.
Amesema wastani wa wagonjwa watano kila siku hupewa rufaa mkoani humo na ili kukidhi mahitaji hospitali hiyo inahitaji magari saba.
“Suala hili tumeliwasilisha wizarani na tumeahidiwa magari hayo mawili yanayotarajiwa kununuliwa muda wowote lengo likiwa ni kuboresha huduma na kwenda sambamba na mahitaji yaliyopo,” amesema Dk Dyegura.
Amesema magari yaliyopo yamezidiwa kutokana na kutumiwa na halmshauri za mkoa pale inapohitajika na kwamba uwepo wa huduma ya M- mama ni moja ya sababu inayochangia uhitaji wa magari zaidi.
Akikabidhi gari hilo, mbunge Mathayo amesema Serikali imedhamiria kuboresha huduma za afya ili zikidhi mahitaji ya wananchi.
Mathayo amesema awali hospitali hiyo ya rufaa ilikuwa ikikabiliwa na changamoto ya ukosefu wa vifaa tiba lakini jitihada zimefanyika, na sasa ina vifaa vingi hali iliyosababisha kuanza kutolewa kwa huduma bora ikiwamo baadhi ya huduma za kibingwa.
“Serikali iliahidi na tayari imeanza kutekelezwa tena kwa kiwango kikubwa mfano hapa tayari tuna mashine ya CT- Scan, mashine kwaajili ya usafishaji wa figo, vifaa tiba vya kisasa kwa ajili ya kinywa na meno na huduma nyingine nyingi ambazo awali zilikuwa hazipatikani katika hospitali yetu, wagonjwa walikuwa wakilazimika kwenda hospitali ya rufaa ya kanda na walikuwa wanatumia gharama kubwa na muda mwingi kufuata huduma kule,” amesema.
Baadhi ya wakazi wa Musoma wamesema uwepo wa hospitali hiyo umesaidia kwa kiasi kikubwa kuwapunguzia adha waliyokuwa wakikutana ikiwamo kwenda Hospitali ya Rufaa ya Kanda ya Bugando kwa ajili ya matibabu.
Hata hivyo, wameomba kuharakishwa kwa ujenzi ambao bado unaendelea ili kutoa nafasi kwa huduma nyingi kutolewa hospitalini hapo hasa za kibingwa.
“Kuna ahadi ya huduma za kibingwa za mifupa, hili ni tatizo ni kubwa tunaomba ujenzi unaoendelea ukamilike kwa haraka ili huduma hizo zitolewe hapa hapa,” amesema Lucas Manjebe.