Wakati zikisalia saa chache kabla ya Yanga kushuka Uwanja wa Benjamin Mkapa kupambana na Al Hilal ya Sudan, kocha wa Waarabu hao Florent Ibenge amemvuta mjini kocha mmoja aliyewatibulia wenyeji wake.
Ibenge amemuita jijini Dar es Salaam haraka kocha Anicet Kiazmak ambaye ni kocha wa Tabora United iliyoichapa Yanga wiki chache zilizopita kwenye mchezo wa Ligi.
Ibenge alifanya kazi na Kiazmak pamoja wakiwa Al Hilal ambapo taarifa ambazo Mwanaspoti imezipata ni kwamba kocha huyo anatakiwa kuja kufanya uchambuzi wa mwisho wa kiufundi kuelekea mchezo wa timu hizo mbili utakaoanza saa 10:00 alasiri.
Tayari Kiazmak ameshatua jijiji Dar es Salaam asubuhi hii kwa treni akitokea Tabora akipitiw Dodoma tayari kwa kikao hicho na bosi wake wa zamani.
Ibenge anamuamini Kiazmak kwenye eneo la kuwachambua wapinzani ambapo Wakongomani hao wawili watajifungia kwa lengo Moja la kuwatafutia dawa wenyeji
Hata hivyo utata pekee ambao watakutana nao makocha hao ni kwamba Yanga ipo chini ya kocha mpya Sead Ramovic ambaye ameshathibitisha kwamba Kuna baadhi ya mabadiliko yataanza kuonekana kwenye kikosi chake.