Kamati kuchunguza sakata la wanafunzi 15 wanaodaiwa kuchoma moto shule Siha

Moshi. Timu inayochunguza tukio la wanafunzi 15 wa Shule ya Sekondari Sanya Day, Wilaya ya Siha, Mkoa wa Kilimanjaro waliokamatwa kwa madai ya kufanya vurugu, imeanza uchunguzi wake huku wanafunzi hao wakiwa wamesimamishwa masomo.

Novemba 20, 2024  mkuu wa wilaya hiyo, Dk Christopher Timbuka alithibitisha kukamatwa kwa wanafunzi hao na kueleza kuwa, vurugu hizo zilifanyika Novemba 17, 2024.

Amebainisha kuwa,  chanzo cha vurugu kilitokana na mmoja wa wanafunzi wa kidato hicho kukamatwa na simu na walinzi wa shule, waliotoa taarifa kwa mmoja wa walimu.

“Wanafunzi hao walichukizwa na kitendo cha walinzi kutoa taarifa kwa mwalimu hali iliyosababisha wao kuwarushia walinzi mawe. Baadaye usiku huo, walikusanyika na kujaribu kuchoma moto nyumba ya mwalimu,” amesema Dk Timbuka.

Amesema moto huo ulisababisha uharibifu mdogo kwenye mlango wa nyumba hiyo kabla ya kudhibitiwa.

Akizungumzia hatua zilizochukuliwa leo Jumanne Novemba 26, 2024, Dk Timbuka amesema wanafunzi hao wamesimamishwa masomo na wanatakiwa kufika shuleni wakiwa na wazazi wao.

“Baada ya polisi kukamilisha taratibu za awali, tuliwakabidhi bodi ya shule kwa hatua zaidi. Shule imewasimamisha masomo wakati uchunguzi ukiendelea na wanapaswa kuja na wazazi wao,” amesema Dk Timbuka.

Mkurugenzi wa halmashauri hiyo, Dk Haji Mnasi amesema tayari ametuma timu shuleni hapo kufanya uchunguzi wa tukio hilo.

“Uchunguzi unaendelea na nasubiri taarifa rasmi kutoka kwa timu niliyoituma pamoja na bodi ya shule. Nitatoa maelezo baada ya kupata mrejesho,” amesema.

Mwenyekiti wa bodi ya shule hiyo, Ernest Fatael amesema bado wanasubiri mrejesho kutoka Jeshi la Polisi kabla ya kufanya uamuzi kuhusu suala hilo.

“Kesi bado iko polisi na walituambia tusubiri. Hatujatoa hitimisho kuhusu wanafunzi hawa,” amesema.

Related Posts