Dar es Salaam. “Naifahamu na nimekuwa naitumia, inarahisisha kuandika insha, yaani ukiwa na swali lako unaandika tu kwa haraka inakujibu. Nikipata swali linalonitaka kujielezea wala siumizwi kichwa napata majibu kwa haraka” anasema mmoja wa wanafunzi wa sekondari ambaye jina lake na shule vimehifadhiwa.
Majibu ya mwanafunzi huyu yalikuja baada ya kuulizwa kwamba anafahamu nini kuhusu teknolojia ya Akili Mnemba (Artificial Intelligence- AI).
Alichojibu mwanafunzi huyu hakina tofauti na walichojibu wanafunzi wengine watatu waliolizwa swali kama hilo.
“Nafahamu kuhusu AI na naanza kujifunza ‘coding’, nikifika chuoni nitajikita eneo hilo zaidi kwa sababu ndiyo tunakoelekea. Kwa sasa inanisaidia kujifunza namna ya kujibu maswali na kupata majibu ya maswali ninayokutana nayo,” anasema Leonard Bwire mwanafunzi wa kidato cha sita.
Wakati wanafunzi hao wanasema hivyo teknolojia hii bado ni ngeni kwa baadhi ya walimu, wakiwa hawana wanachokifahamu kuhusu wanafunzi kuitumia kwenye masomo.
Mwalimu wa sekondari ya Kwagunda Omari Badili anasema ana uelewa mdogo kuhusu akili mnemba na hafahamu kama wanafunzi wanaitumia kwenye masomo, ingawa ni shauku yake kuifahamu vyema teknolojia hiyo.
“Binafsi sijawahi kupata mafunzo yoyote kuhusu akili mnemba, ingawa baada ya kunielezea nimegundua kwa namna moja au nyingine huwa naitumia lakini si kwa ajili ya kufundishia.
“Sisi walimu tunaamini mwanafunzi mzuri ni yule anayeweza kutumia akili yake, sikuwa nafahamu kama wanatumia hizo teknolojia kujibu maswali. Halafu kingine bado nashindwa kuelewa mnufaika mzuri wa elimu ni yupi je ni yule anayetumia akili yake au anayetumia teknolojia,”
“Halafu ukiwa mwalimu mzuri utalijua vyema darasa lako na utafahamu uwezo wa wanafunzi wako wote, sasa ikitokea umetoa kazi halafu kuna mwanafunzi anakuja na misamiati mipya lazima ushtuke, tulikuwa tunahisi kuna mtu kamsaidia kumbe sasa ndiyo nagundua huenda akili mnemba inahusika,” anasema.
Wadau wa elimu wanasema ni muhimu kwa walimu kujua kuhusu teknolojia hiyo ili waweze kuboresha ufundishaji wao, kuwasaidia wanafunzi kupata ujuzi muhimu wa teknolojia, na kuhakikisha wanaitumia kwa njia salama na yenye maadili.
Hayo waliyasema walipokuwa wakijadili wakati wa mkutano ulioangazia ubora wa elimu barani Afrika (IQEC), ulioandaliwa na Mtandao wa Elimu Tanzania (TENMET) na kuwakutanisha wadau wa elimu kutoka mataifa zaidi ya 16 ya bara la Afrika.
Wakichangia mada iliyohusu matumizi ya teknolojia ya akili mnemba katika elimu, wadau hao wanaeleza kuwa hakuna namna lazima walimu wawe na uelewa wa kina wa teknolojia hiyo kuwezesha wanafunzi kujua jinsi ya kuitumia katika maisha yao na kazi zao za baadaye, huku wakijua changamoto na faida za teknolojia hii.
Meneja programu wa Shule Direct, Iku Lazaro anasema kuna umuhimu mkubwa wa walimu kuendana na kasi ya maendeleo ya teknolojia ili kujua kila hatua ya ukuaji wake na namna inavyoweza kuwa na athari chanya na hasi kwenye elimu.
Anasema kwa hatua iliyofikia sasa, hakuna namna ya kupambana na maendeleo hayo hivyo ni muhimu kutafuta njia za kuendana nayo hivyo ni muhimu kwa uwekezaji kufanyika katika eneo hilo kuhakikisha walimu hawabaki nyuma.
“Walimu wakiwa vyuoni wanapaswa kufundishwa kuhusu teknolojia na maendeleo yake, sasa hivi teknolojia ni zaidi ya kujua kutumia kompyuta. Walimu wanatakiwa kuwa vinara wa kufahamu maarifa yote ambayo yanaweza kupatikana kupitia teknolojia.
“Hii ni kama ukuta hatuwezi kupambana nao, tunachotakiwa ni kutafuta namna ya kwenda nayo kwa sababu hakuna namna tunaweza kuyakwepa maendeleo ya teknolojia,”anasema Iku.
Mkurugenzi Mtendaji wa Sahara Ventures Jumanne Mtambalike anasema mabadiliko ya dunia yanafanya matumizi ya akili mnemba kuchukua nafasi kubwa, hivyo walimu wanapokuwa na uelewa wa wanaweza kuwasaidia wanafunzi kujiandaa kwa ajili ya ajira na fursa za kazi zinazohusiana na teknolojia.
Mtambalike anasema kwa sasa hakuna namna wanafunzi wanaweza kuzuiwa kutumia akili mnemba bali kinachotakiwa ni kutafuta mbinu kuendana na maendeleo haya ya teknolojia.
“Kupitia maendeleo ya teknolojia ikiwamo matumizi ya akili mnemba siku hizi mwalimu sio mtu pekee mwenye maarifa darasani, wanafunzi wana uwezo, wanajua zaidi ya kile anachofahamu mwalimu kwa sababu zipo njia za kufanya hivyo na wanazifahamu.
“Ili kukabiliana na hili walimu nao wanapaswa kuendana na maendeleo ya teknolojia hususani hii akili mnemba ambayo inatumika zaidi kwa sasa. Ni wakati kwa walimu kujifunza mambo mapya na kuachana na mambo ya zamani, dunia inabadilika hivyo ni muhimu kuendana na mabadiliko hayo ikiwemo maendeleo ya teknolojia,”anafafanua.
Mbali na kuwa na uelewa, Mtambalike anasema walimu pia wanaweza kutumia akili mnemba katika utendaji wao wa kila siku ikiwemo maandalizi ya somo.
Mwalimu atumie vipi akili mnemba?
Mhadhiri wa Chuo Kikuu cha Dar es Salaam Dk Faraja Kristomus anasema akili mnemba ni sehemu ya teknolojia inayoendelea kukua kwa kasi, na wanafunzi wanahitaji kuwa na ujuzi wa kutumia zana na mifumo hii ili waweze kuingia kwenye ushindani.
Anasema endapo walimu watakuwa na uelewa wa kina wa teknolojia hiyo watasaida kuhamasisha wanafunzi kuwa na ufahamu kuhusu matumizi bora ya akili mnemba.
Mbali na hilo, mhadhiri huyo anasema walimu wanaweza kutumia akili mnemba kufanya tafiti za kielimu kwa njia mpya.
“Kwa mfano, AI inaweza kusaidia kuchanganua makundi makubwa ya data, kutoa michango ya kitaalamu kwa ufundishaji, na kusaidia kubaini njia bora za kuboresha mbinu za ufundishaji. AI pia inaweza kutumika kama zana ya kufanya tathmini na tathmini ya mbinu mpya za kufundisha”anasema Dk Kristomus.
Faida nyingine ya akili mnemba mhadhiri huyo anasema mwalimu anaweza kuitumia kama nyenzo ya kufuatilia maendeleo ya wanafunzi kwa njia inayohusisha data na kuchanganua mitindo ya mafanikio.
“Hii inaruhusu walimu kujua ni maeneo gani mwanafunzi anahitaji msaada zaidi, na pia inaweza kusaidia katika utambuzi wa changamoto za kujifunza mapema.Walimu wanaweza kutumia taarifa hizi kwa lengo la kubinafsisha mikakati ya ufundishaji na kuhakikisha wanafunzi wanapata matokeo bora”.
Dk Kristomus anasema mwalimu anayejua matumizi ya akili mnemba atawasimamia wanafunzi wake waweze kuitumia vyema kwa kuzingatia maadili.
“AI inahitaji usimamizi wa maadili. Walimu wanapokuwa na uelewa kuhusu masuala kama vile faragha, usalama wa data, na ubunifu, wanaweza kuwafundisha wanafunzi kuhusu matumizi bora na salama ya teknolojia hii.
“Pia, walimu wanaweza kuwaongoza wanafunzi katika majadiliano ya maadili na athari za AI kwenye jamii, na kujenga uelewa wa kijamii kuhusu akili mnemba inavyoweza kuathiri maisha yao.
Mtalaam wa Tehama, Leocadia Swai anasema zana za teknolojia hiyo kama ChatGPT, hurahisisha wanafunzi kupata habari na kujifunza, kwani wanaweza kuuliza maswali kwa haraka na kwa urahisi na kupokea majibu na huweza pia kumsaidia mtu kujisomea mwenyewe.
“Utumiaji wa programu za akili bandia husaidia pia kuokoa muda na nyenzo kwa walimu na wanafunzi. Kingine mtu anapata majibu wakati wowote anaohitaji bila kusubiri uwepo wa mwalimu. Hii inaweza kuwa ya manufaa hasa kwa wanafunzi ambao wana ratiba nyingi au wanaoishi katika maeneo ya mbali,”
Hata hivyo mtaalam huyo alitahadharisha kuwa matumizi ya zana zinazoendeshwa na akili bandia katika elimu, yanaweza kusababisha ukosefu wa mwingiliano wa kibinadamu, kwani wanafunzi wanaweza kuingiliana zaidi na teknolojia kuliko na walimu na wenzao.
Matokeo ya hilo ni kusababisha kupungua kwa ujuzi wa kijamii na akili ya kihisia, ambayo pia ni muhimu kwa mafanikio katika maeneo mengi ya maisha.
Hoja hiyo inaungwa mkono na Neema Urasa ambaye kitaaluma ni mtafiti, yeye anaeleza matumizi ya programu za aina hii huwafanya wanafunzi kutoshughulisha ubongo kufikiri, na matokeo yake kila wanapokutana na swali wanakimbilia kutafuta msaada wa teknolojia.