Mwenyekiti Chadema Kilimanjaro aachiwa kwa dhamana

Moshi. Mwenyekiti wa Chama cha Demokrasia na maendeleo (Chadema) Mkoa wa Kilimanjaro, Gervas Mgonja ameachiwa kwa dhamana.

Mgonja alikamatwa na Jeshi la Polisi Mkoa wa Kilimanjaro jana Jumatatu Novemba 25, 2024  kwa tuhuma za kutoa kauli za kuhamasisha wananchi kuvamia makazi ya wasimamizi wa uchaguzi wa Serikali za mitaa 2024, mkoani humo.

Kwa mujibu wa taarifa iliyotolewa jana usiku na Kamanda wa Polisi Mkoa wa Kilimanjaro, Simon Maigwa, mwenyekiti huyo alikamatwa baada ya kuonekana kwenye video mjongeo iliyosambaa katika mitandao ya kijamii, akiwa anawahamasisha wananchi wafanye uhalifu huo kesho Jumatano Novemba 27, 2024.

Akizungumza leo Jumanne Novemba 26, 2024, Mgonja amesema ameachiliwa kwa dhamana na kutakiwa kuripoti polisi Alhamisi, Novemba 28, 2024 na hakuwa anahamasisha uchochezi.

“Nimepata changamoto ndani ya hizi siku mbili na kama mnavyojua tupo kwenye kampeni za uchaguzi wa Serikali za mitaa na mimi kama mwenyekiti wa mkoa, wajibu wangu ni kuzunguka kwenye baadhi ya majimbo ambayo tuna wagombea ili kuwanadi na juzi nilikuwa Rombo nikafanya mkutano pale Tarakea,” amesema Mgonja.

“Nikazungumza na wananchi wa Rombo nikawaambia kwa sababu tumeenguliwa wagombea wengi na tumekata rufaa nyingi na hakuna kilichobadilika kwenye rufaa zile, wagombea wetu wametupwa takribani 2,000 Mkoa mzima wa Kilimanjaro, nikawaambia hawa wachache tuliobaki nao tuwalinde.”

Hata hivyo, amesisitiza kuwa kwa sasa anaenda kuendelea na kampeni za kuwanadi wagombea wao na kufunga kampeni.

Related Posts