Nabi, Senzo waongeza mzuka Yanga

Dar es Salaam. Yanga imepokea salamu za kheri kwenye mchezo wake wa kwanza wa Ligi ya Mabingwa Afrika hatua ya makundi kutoka kwa viongozi wao wawili wa zamani kocha Nasreddine Nabi na Mtendaji Mkuu Senzo Mazingisa.

Akizungumza akiwa nchini Afrika Kusini Nabi amesema anaamini Yanga itafanya vizuri kwenye mchezo huu wa kwanza wa makundi dhidi ya Al Hilal.

Nabi amesema licha ya kuwa na kikosi imara pia anamuamini kocha mpya Sead Ramovic ambaye ataiongoza timu hiyo kwenye mchezo wa kwanza tangu atangazwe kuwa bosi wa benchi la ufundi la mabingwa hao wa soka Tanzania.

“Sina wasiwasi na Yanga, inakutana na timu ngumu Al Hilal lakini naamini watapata matokeo mazuri, wana kikosi kizuri kinachoweza kushindana na timu yoyote Afrika,”amesema Nabi ambaye aliifundisha Yanga kwa mafanikio makubwa.

“Hata kocha wao Sead (Ramovic) ni kocha mzuri, nimeona watu wana wasiwasi na uzoefu wake kwenye mashindano ya Afrika, kwangu mimi sio kitu muhimu hata wenye uzoefu walinzia hapa anapoanzia.”

Wakati Nabi anayeifundisha Kaizer Chiefs akiyasema hayo, pia Senzo amesema ingawa mchezo huo utakuwa mgumu lakini ana imani timu yao itafanya vizuri.

“Ni mchezo mgumu kwa timu zote lakini nina imani na timu ya wananchi wenzangu, imekuwa pamoja kwa muda mrefu uzoefu wao utawasaidia kushinda leo.”

Related Posts