Polisi yawasaka waliomjeruhi mtoto aliyekatishwa masomo

Arusha. Polisi mkoani Arusha wameanza msako wa kuwatafuta watuhumiwa waliohusika na tukio la kumshambulia na kumjeruhi mtoto wa kike wa miaka 16.

Mtoto huyo ambaye ni mkazi wa Kijiji cha Nadaale, Kata ya Ilorienito, wilayani Longido, Mkoa wa Arusha, alinusurika kifo baada ya kufanyiwa ukatili huo uliosababisha majeraha sehemu mbalimbali za mwili wake.

Kwa mujibu wa taarifa iliyotolewa na Kamanda wa Polisi Mkoa wa Arusha, Justine Masejo leo Jumanne Novemba 26, 2024 uchunguzi wa awali umeonesha mtoto huyo alikuwa mwanafunzi wa darasa la sita katika Shule ya Msingi Kitumbeine, wilayani Longido.

“Lakini aliachishwa masomo na kuozeshwa kwa mwanamume aitwaye Mungure Arkaswai mkazi wa Kata ya Engaruka, Wilaya ya Monduli,” amesema kamanda huyo.

Amesema polisi inakemea vikali tabia ya baadhi ya wanaofanya vitendo vya ukatili na unyanyasaji ikiwamo wa kuwaozesha watoto.

“Tutawakamata na kuchukua hatua za kisheria dhidi yao na tunaomba wananchi na taasisi mbalimbali kuendelea kushirikiana na polisi kutoa elimu ya kupinga ukatili,” amesema Kamanda Masejo.

Mwenyekiti wa Umoja wa Wazazi wa Chama cha Mapinduzi (CCM) Mkoa wa Arusha, Hezron Mbise amekemea kitendo cha kikatili alichofanyiwa mtoto huyo ambaye wazazi wake walitaka kukatisha ndoto zake za kupata elimu.

“Jumuiya ya wazazi tunaalani kitendo hiki cha kikatili dhidi ya mwanafunzi huyo. Niwaombe wazazi na walezi kuzingatia maadili ya malezi ikiwa ni pamoja na kuwapa watoto wao haki ya kupata elimu ambayo inatolewa na serikali bila gharama yeyote,” amesema Mbise.

Tukio hilo lilitokea Novemba 19, 2024 huku ikidaiwa kuwa mume wake alimfanyia ukatili huo akimtuhumu mtoto huyo kukwepa majukumu ya kuolewa ikiwamo kubeba ujauzito.

Mtoto huyo aliokolewa na wasamaria wema kwa kushirikiana na Shirika la Kutetea Wanawake na Watoto (Mimute).

Mkurugenzi wa shirika hilo, Rose Njilo, amesema mtoto huyo alikatishwa masomo mwaka jana na kulazimishwa kuolewa.

Ofisa Mtendaji wa Kijiji cha Irendei, Josephine Shirima amesema wanaendelea kushirikiana na jamii kuhakikisha anayedaiwa kuhusika na kitendo hicho anakamatwa kwa ajili ya hatua zaidi.

Aidha, kwa mujibu wa taarifa iliyotolewa jana Jumatatu Novemba 25, 2024 na Waziri wa Maendeleo ya Jamii,Jinsia,Wanawake na Makundi Maalum, Dk Dorothy Gwajima, Serikali inafuatilia kwa karibu suala la matibabu ya mtoto huyo na upatikanajai wa haki yake ya kuishia kwa amani na usalama.

Aidha, amewakumbusha wananchi kuwa ulinzi na usalama wa watoto ni jukumu la kila mmoja hivyo washirikiane kuwalinda watoto.

Related Posts