Dar es Salaam. Wakati kesho Jumatano Novemba 27, 2024 Watanzania wakitarajiwa kupiga kura kuwachagua viongozi wa Serikali za mitaa, vijiji na vitongoji, Rais Samia Suluhu Hassan amesema ni muhimu kuheshimu uamuzi wa wapigakura.
Amesema demokrasia yenye nguvu inajengwa kwa misingi ya heshima na mshikamano, akiwataka wananchi wote waliojiandikisha katika mchakato huo, kujitokeza kupiga kura.
Pia, amewataka kujiepusha na vitendo vya vurugu, uchochezi na uvunjifu wa amani.
“Niwasihi wasimamizi wa uchaguzi na wanaohusika, kuhakikisha uchaguzi unafanyika kwa haki, uwazi kwa kuzingatia taratibu zilizokubaliwa na wadau. Matumaini yangu mtaendelea kutekeleza majukumu yenu kwa weledi, kulinda haki za wananchi na kudumisha utulivu tunapoelekea mwisho wa mchakato huu,” amesema.
Rais Samia ameeleza hayo leo Jumanne Novemba 26, 2024 alipohutubia Taifa Ikulu jijini Dodoma, kuhusu mchakato wa uchaguzi.
Amesema dhamira ya Serikali ni kuhakikisha uchaguzi unafanyika kwa uwazi, haki na kwa kuzingatia kanuni zilizopo.
Amewataka wadau wa uchaguzi kutoa ushirikiano ili kufanikisha azma ya kuwa na uchaguzi wa amani unaoakisi heshima ya Taifa lenye mshikamano na demokrasia imara.
Rais Samia amesema kesho ni siku ambayo Watanzania wataendeleza utamaduni wa kuwapata viongozi kwa njia ya uchaguzi kwa kuwachagua viongozi wa mitaa, vijiji na vitongoji watakaohudumu kwa kipindi cha miaka mitano ijayo.
“Hii ni fursa muhimu kwa kila Mtanzania mwenye sifa ya kupiga kura kuchangia maendeleo ya nchi kwa njia ya kidemokrasia kwa kuchagua kiongozi mwenye sifa. Serikali za mitaa ni msingi wa ujenzi wa Taifa imara lenye maendeleo endelevu,” amesema.
Amesema kupitia viongozi watakaochaguliwa katika uchaguzi huo, watahakikisha wanaweka misingi mizuri ya uwajibikaji katika utoaji wa huduma bora kwa wananchi na usimamizi wa rasilimali za umma.
“Hii ni fursa kwetu ya kuhakikisha uamuzi unaohusu jamii utakaotolewa na mahitaji halisi ya wananchi. Kila kura itakayopigwa ina maana na itasaidia kufanikisha azma yetu ya kujenga jamii yenye haki, usawa na maendeleo kwa wote.
“Uchaguzi ni haki yetu na jukumu letu kuhakikisha tunatumia jukumu letu hilo, kwa amani na utulivu. Niwasihi wananchi tujiepushe na vitendo vya uchochezi, vurugu na uvunjifu wa sheria, amani ni urithi wetu wa thamani na wajibu wetu kuilinda kwa gharama yoyote ile,” amesema.
Amewahisi Watanzania kutumia fursa hiyo kuchagua viongozi waadilifu, wabunifu na wenye maono ya kuendeleza jamii za Kitanzania.
Samia amesema kila kura ina umuhimu mkubwa katika kuamua mustakabali wa maendeleo na Taifa.
Amesema vituo vya kupiga kura vipo katika mitaani, majengo ya umma na maeneo ya wazi yaliyokubaliwa ambavyo vitafunguliwa kuanzia saa mbili asubuhi na kufungwa saa 10 jioni.
“Napenda kuwahakikishia kuwa uamuzi wenu katika sanduku la kura utaheshimiwa,” amesema.