KATIKA michezo mitano iliyopita, Simba imeonyesha kiwango bora kwa kushinda zote dhidi ya Tanzania Prisons (1-0), Namungo (3-0), Mashujaa (1-0), KMC (4-0) na Pamba Jiji (1-0). Mafanikio hayo yanaiweka timu hiyo kwenye hali nzuri kuelekea mchezo wa kwanza wa hatua ya makundi ya Kombe la Shirikisho Afrika dhidi ya Bravos do Maquis ya Angola, mechi itakayofanyika kesho Jumatano, kwenye Uwanja wa Benjamin Mkapa, Dar es Salaam.
Bravos ambao ni wapinzani wa Simba, wana rekodi tofauti. Katika michezo yao mitano ya mwisho, wameshinda mara moja tu dhidi ya C.R.D. Libolo kwa bao 1-0, huku wakitoka sare mara tatu dhidi ya Academica (0-0), CD Lunda Sul (0-0) na Sagrada (0-0). Walipoteza mchezo mmoja dhidi ya Interclube kwa mabao 3-1.
Kwa mujibu wa takwimu, Simba chini ya kocha Fadlu Davids imeonyesha uimara mkubwa. Timu hiyo imefunga mabao 10 katika michezo mitano ya mwisho na haijaruhusu nyavu zake kuguswa. Wakati huohuo, Bravos imefunga mabao mawili tu na kuruhusu matatu. Hali hii inawapa Simba faida ya kimkakati, hasa kwa kuzingatia mgawanyo wa mabao ambao umebeba uzito mkubwa katika kuamua michezo yao.
Simba imeonyesha uwezo wa kugawa nguvu vizuri katika vipindi vyote vya mchezo. Mabao sita kati ya 10 waliyofunga katika mechi za hivi karibuni yalifungwa kipindi cha kwanza, huku manne yakifungwa kipindi cha pili. Kwa upande mwingine, Bravos wanaonekana kuwa na udhaifu mkubwa katika kipindi cha pili. Katika mchezo waliopoteza dhidi ya Interclube, waliruhusu mabao mawili kipindi cha kwanza. Kwa jumla, wamefungwa mabao 10 katika michezo 12 ya msimu huu, ambapo asilimia 70 ya mabao hayo (mabao saba) yamefungwa kipindi cha pili.
Licha ya Bravos kufanya vizuri wakati wa hatua za kufuzu kwa kuishinda Coastal Union ya Tanzania na St Eloi Lupopo ya DR Congo huku wakiruhusu bao moja tu, inaonekana wazi kuwa timu hiyo ina changamoto ya kupoteza udhibiti wa mchezo, hasa katika dakika za mwisho.
Hali hii inatoa nafasi kwa Simba kutumia udhaifu huo kwa kuimarisha mashambulizi kipindi cha pili, jambo ambalo linaweza kuwa mwamuzi wa matokeo ya mchezo huo muhimu. Ushindi kwa Simba si tu utaanzisha safari yao ya hatua ya robo fainali kwa mafanikio, bali pia utaimarisha nafasi yao katika Kundi A lenye timu zenye ushindani mkubwa kama CS Sfaxien na CS Constantine.
Nyota wa Coastal Union, Mbaraka Yusuph, ambaye alikabiliana na Bravos katika raundi ya kwanza ya kufuzu, alisema: “Bravos ni timu nzuri, lakini wana udhaifu wa kuhimili presha hasa wanapocheza ugenini. Simba wanapaswa kutumia nafasi hiyo kwa kushambulia kwa kasi ni vile tu tulishindwa kutumia nafasi ambazo tulizitengeneza katika mchezo wetu wa marudiano.”
Kocha wa zamani wa Simba, Dylan Kerr, pia alilitakia mafanikio chama lake hilo la zamani katika mchezo huo wa kimataifa, akisema: “Simba ni timu kubwa yenye historia ya mafanikio Afrika. Naamini watafanya vizuri.”
Kwa hali ilivyo, Simba inapewa nafasi kubwa ya kuanza safari yao ya hatua ya makundi kwa ushindi kulingana na takwimu zinachosema. Mashabiki wanatarajia kuona mbinu za kiufundi kutoka kwa Fadlu ambaye hesabu zake zote zipo kwenye mchezo huo kuhakikisha Mnyama anavuna alama tatu muhimu katika mchezo huu wa nyumbani.