KOCHA Mkuu wa Azam FC, Rachid Taoussi amesema kikosi hicho kwa sasa kipo katika mwenendo mzuri ingawa bado anaendelea kupambana na changamoto ya umaliziaji, kutokana na timu hiyo kutengeneza nafasi nyingi lakini wanafunga mabao machache.
Katika kikosi cha Azam, Nassor Saadun ndiye mshambuliaji tegemeo mwenye mabao matatu ya Ligi Kuu akisaidiana na Jhonier Blanco mwenye bao moja, huku Adam Adam akiwa hajafunga.
Akizungumza na Mwanaspoti, Taoussi alisema maendeleo yao sio mabaya hadi sasa katika Ligi Kuu Bara japo anaendelea kupambana na changamoto hizo, akiamini zitachukua muda kidogo kuisha ingawa muhimu ni kupata ushindi.
“Jambo nzuri na muhimu kwetu ni kuona tunapata matokeo mazuri ya ushindi huku tukiendelea kutengeneza kikosi bora cha ushindani, tutaendelea kupambana na hali iliyopo ili tusitoke nje ya malengo tuliyojiwekea kwa msimu huu,” alisema Taoussi.
Tangu kocha Taoussi ateuliwe kukiongoza kikosi hicho Septemba 7 mwaka huu akichukua nafasi ya Msenegali, Yousouph Dabo, ameiongoza Azam FC katika michezo 10 ya Ligi Kuu Bara ambapo ameshinda saba, sare mbili na kupoteza mmoja tu.
Kiujumla Azam FC imecheza michezo 11 ya Ligi Kuu Bara msimu huu, ikishinda saba, sare mitatu na kupoteza mmoja, ambapo kikosi hicho kimefunga jumla ya mabao 14 na kuruhusu matatu jambo ambalo bado halijamridhisha Taoussi.
Katika mabao 14 yaliyofungwa na Azam kwenye ligi msimu huu, mbali na manne kutoka kwa washambuliaji, Saadun (3) na Blanco (1), mengine ni kutoka kwa beki Lusajo Mwaikenda (2) na viungo washambuliaji Idd Seleman ‘Nado’, Feisal Salum ‘Fei Toto’ na Gibril Sillah ambao kila mmoja amefunga mabao mawili, huku jingine ni nyota wa KMC, Fredy Tangalo akijifunga.