Tigo yabadili tena jina, yaeleza sababu

Dar es Salaam. Chapa ya kampuni ya huduma za simu ya Tigo Tanzania imebadilishwa  na sasa itakujulikana kwaa jina la Yas.

Kampuni hiyo ambayo wakati inaingia nchini miongo mitatu iliyopita ilianza kwa jina la Mobitel kabla ya kuitwa Tigo, imetambulisha jina hilo jipya leo Novemba 26, 2024 jijini Dar es Salaam.

Katika tulio hilo lililohusisha wadau mbalimbali wa huduma, mawasiliano na fedha kidijitali, Waziri wa Habari, Mawasiliano na Teknolojia ya Habari, Jerry Silaa ndiye aliyekuwa mgeni rasmi.

Mbali ya kubadilika chapa ya kampuni, jina la huduma zake za miamala ambazo awali zilijulikana kwa jina la Tigo Pesa limebadilika na sasa litaitwa Mixx by yas.

Yas (zamani Tigo) inamilikiwa na kampuni ya Honora Tanzania Public Limited ambayo ni sehemu ya kampuni mama ya Axian Telecom Group.

Katika uzinduzi wa jina jipya,  imeelezwa ni hatua muhimu ya kuonyesha dhamira ya kuongoza katika ubunifu wa kidijitali na uwezeshaji wa wananchi kiuchumi Tanzania nzima.

Kubadilishwa majina ya Tigo na Tigo Pesa hakujafanyika Tanzania pekee bali ni mpango wa Kampuni ya Axian Telecom Group kuwa na jina moja katika kampuni zake tanzu zote barani Afrika,  ili kuwa  na chapa ya kiuanamajumui yenye nguvu Afrika.

Nchi zingine zaidi ya Tanzania ni Togo, Madagascar, Senegal na Comoro.

Kuhusu mabadiliko hayo, Mwenyekiti wa Bodi wa kampuni hiyo, Rostam Aziz amesema: “Mabadiliko haya ni ishara ya dhamira ya kuendelea kuwekeza na kuendeleza mabadiliko ya kidijitali Tanzania Bara na Visiwani. Kwa pamoja na Axian Telecom Group tupo tayari kuendelea kufungua fursa mpya, kuhamasisha ubunifu, kujenga kesho iliyo bora na kuunganisha watu zaidi.”

Amesema Yas na Mixx by Yas zinadhamiria kubeba maono ya kampuni ya kuwa kiungo muhimu cha ubunifu wa kidijitali barani Afrika kwa kutengeneza fursa zisizo na kikomo, kuboresha maisha kupitia huduma za kidijitali na huduma za kifedha kwa mamilioni ya Watanzania.

Mwenyekiti wa Axian Telecom, Hassanein Hiridjee amesema: “Kampuni imekuwa kwenye safari thabiti ya kuunganisha Waafrika kupitia chapa zao zinazokua. Kuweza kuwezesha kizazi kijacho hatuna budi kuwa  na chapa inayotoa huduma katika mataifa tofauti na chapa hii inaiunganisha Afrika.”

Ofisa Mtendaji Mkuu wa mpito wa Kampuni ya Honora Tanzania, Jerome Albou amesema mabadiliko ya chapa ni mpango wa kampuni mama wa zaidi ya miaka miwili iliyopita na yamefanyika katika nchi tano ambazo wanatoa huduma.

“Tumekuwa tukiongoza katika ubunifu, tutaendelea kufanya hivyo, watu watarajie mambo mazuri. Kila siku tunaangalia mteja anataka nini nasi tunaboresha zaidi na zaidi,” amesema.

Katika uzinduzi huo, Waziri Silaa amesema tangu enzi za Mobitel kampuni hiyo imekuwa ikitoa huduma vizuri na kuchangia kwa sehemu kubwa katika maendeleo ya huduma za mawasiliano nchini.

“Uwekezaji wa Honora umechangia maendeleo ya huduma za mawasiliano nchini kwa kuongeza idadi ya watumiaji wa huduma za intaneti na miamala ya simu,” amesema Silaa.

Related Posts