Waliofariki kwa mafuriko kuzikwa Novemba 28

Tarime. Wakati Serikali ikijitayarisha kwa maziko ya watu wanane wa familia moja waliofariki dunia kwa kusombwa na maji wilayani Tarime, Mkoa wa Mara yaliyopangwa kufanyika Novemba 28, 2024, tayari watu 15 wamejitokeza na kujitambulisha kama ndugu wa marehemu hao.

Watu hao wameonyesha nia ya kushirikiana na Serikali katika maandalizi ya shughuli hiyo ya maziko.

Watu wa familia hiyo walifariki dunia usiku wa kuamkia  Jumatatu Novemba 25, 2024 katika Mtaa wa Bugosi wilayani Tarime, baada ya mto Mori uliopo jirani na makazi yao kujaa maji kufuatia mvua zinazoendelea kunyesha wilayani humo.

Katika tukio hilo, jumla ya watu tisa walisombwa na maji na maiti za watu wanane ziliopolewa na mtu mmoja ambaye ni mtoto wa mwaka mmoja bado anatafutwa.

Akizungumza na Mwananchi leo Jumanne Novemba 26,2024, Mkuu wa Wilaya ya Tarime, Edward Gowele, amesema tayari ameelekeza uongozi wa kata na mtaa kutafuta ndugu wa familia hiyo ili waweze kueleza ni wapi miili hiyo itakakozikwa.

“Ingawa familia imepoteza karibia watu wote, lakini tunaamini wapo ndugu na jamaa zao, sasa badala ya sisi kuamua tuzike wapi hii miili tunataka ndugu zao waseme wapi wangependa wapendwa wao wazikwe, ila maziko yao tumepanga yafanyike Novemba 28, 2024” amesema mkuu huyo wa wilaya.

Kufuatia agizo hilo, uongozi wa Kata ya Nyamisangura kwa kushirikiana na Mtaa wa Bugosi ulianza mchakato wa kuwatafuta ndugu hao na tayari watu 15 wamejitokoza  wakidai ni ndugu wa marehemu hao.

Ofisa Mtendaji wa Kata ya Nyamisangura, John Wankyo amesema baada ya watu hao kujitokeza, walipelekwa ofisini kwa mkuu wa wilaya kwa ajili ya taratibu zingine.

“Bado wako kule, kwa sasa naweza kusema tumefikia hatua hiyo hadi baadaye tutakapoambiwa nini cha kufanya,” amesema Wankyo.

Tayari miili minane imeopolewa huku jitihada za kutafuta mwili mwingine zikiwa bado zinaendelea kwa siku ya pili leo, katika shughuli ya utafutaji ambao unashirikisha vyombo vya uokozi na wenyeji wa eneo hilo.

Akizungumzia utaratibu wa maziko, Gowele amesema yatagharamiwa na Serikali na kama ndugu hawatapatikana au kushindwa kupendekeza wapi pa kuwazika, Serikali itaamua miili hiyo iagwe na kuzikwa sehemu itakayoamriwa na ofisi ya mtendaji.

Amesema wakati wanasubiri mapendekezo ya ndugu wa marehemu, shughuli ya kumtafuta mtoto Ochola Joel (1) bado inaendelea, huku matumaini ya kumpata akiwa hai yakizidi kufifia.

Jana Kaimu Kamanda wa Jeshi la Zimamoto na Uokoaji Mkoa wa Mara, Agostino Magere aliwataja waliofariki dunia ni pamoja na Florence Okoth (55), Rebecca Ngari (24), Winfrida Otieno (22), Salome Akinyi (15), Stella Joel (25), Danny Joel (4), Toto Akinyi (12) na Fadhi Ngari (1).

Katika tukio hilo la mafuriko, familia mbili zilihusika, ikiwamo ya kwanza ambayo watu 11 walisombwa na maji na  wawili wamenusurika, wanane wakifariki dunia na mtoto mmoja bado hajapatika.

Familia ya pili ilikuwa na watu tisa na wote wamenusurika, huku ikipoteza mali zote ikiwamo nyumba yao ambayo imesombwa na maji.

Related Posts