Dar es Salaam. Baada ya pilikapilika za kampeni kesho Watanzania watafanya uamuzi wa kuwachagua viongozi wa mitaa, vijiji na vitongoji watakaohudumu kwa miaka mitano ijayo.
Siku saba za kampeni zilizohitimishwa leo Novemba 26, 2024, zilikuwa za hekaheka za wagombea na vyama vyao kujinadi, kuomba kura kabla ya uchaguzi unafanyika Jumatano siku ambayo ni mapumziko.
Ni uchaguzi wa aina yake kutokana na ‘amshaamsha’ zilizoonekana wakati wa kampeni za kuwanadi wagombea, huku vyama vitatu vya CCM, Chadema na ACT Wazalendo vikionekana zaidi zaidi.
Viongozi waandamizi wa vyama hivyo, wameonekana maeneo mbalimbali nchini wakinadi sera na kuwauza wagombea wao kwa wananchi huku vyama vingine vikionekana kwa nadra kwenye maeneo machache.
Kiingine kinachofanya uchaguzi huo kuwa aina wa aina yake ni ushiriki wa vyama 18, tofauti na mwaka 2019, ambao CCM ilichukua nafasi kubwa na hatimaye kushinda mitaa, vijiji na vitongaji kwa zaidi ya asilimia 95, baada ya baadhi ya vyama kususia mchakato huo katika hatua za mwisho vikidai wagombea wao walienguliwa na mawalaka wao kunyimwa nafasi.
Hata hivyo, uchaguzi wa safari hii, licha ya kutokea kasoro kadhaa kwenye uandikishaji na uteuzi wa wagombea, vyama vyote vya siasa vimeendelea hadi hatua ya upigaji kura.
Pamoja na uchaguzi kuwa muhimu kwa Watanzania, pia una maana kubwa kwa vyama vya siasa kwa sababu vinajenga msingi mzuri wa kuviwezesha kushinda katika Uchaguzi Mkuu mwaka 2025 wa wabunge, madiwani na Rais.
Baada ya hekaheka hizo za kampeni, sasa ni zamu ya Watanzania kutumia haki yao ya msingi ya kupiga kura ili kuwachagua viongozi hao ambao ni kiungo muhimu katika maisha yao ya siku.
Viongozi hao – wenyeviti wa serikali za mitaa, vijiji, vitongoji pamoja na wajumbe wao wanayo kazi muhimu ya kuwaunganisha wananchi na Serikali Kuu kuhakikisha sauti zao zinasikika na mahitaji yao yanashughulikiwa ipasavyo.
Kwa mujibu wa Sheria ya Serikali za Mitaa (Mamlaka za Wilaya) ya mwaka 1982 na marekebisho yake, mwenyekiti wa serikali za mitaa anawajibika kwa uongozi wa kijiji, mtaa au kitongoji.
Mwenyekiti atakayechaguliwa Jumatano, ndiye anayewajibika kusimamia mikutano ya kijiji au mtaa, ambayo ni jukwaa la wananchi kujadili masuala ya muhimu ya maendeleo, usalama na ustawi wa jamii.
Pia kiongozi huyo anawajibika kusimamia mapato na kuhakikisha yanatumika kwa mujibu wa sheria.
Kuhusu maandalizi ya uchaguzi huo, Katibu Mkuu wa Ofisi ya Rais, Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (Tamisemi), Adolf Ndunguru ameliambia Mwananchi kuwa maandalizi ya mchakato huo yanakwenda vizuri na amewataka Watanzania kujitokeza kwa wingi kupiga kura.
“Maandalizi yamefanyika leo (Jumanne) kampeni zinafungwa, kesho (Jumatano) ni uchaguzi. Kuna vifaa vinachakatwa serikali kuu na vingine ngazi ya chini, kwa hiyo vifaa vipo na kesho (Jumatano) ni uchaguzi, Watanzania wajitokeze,” amesema Ndunguru.
Akiuangazia uchaguzi huo, Mhadhiri Chuo Kikuu cha Dar es Salaam, Dk Faraja Kristomus amesema matokeo ya uchaguzi huu yatakuwa picha halisi ya kukubalika au kutokubalika kwa chama tawala na kukubalika au kutokubalika kwa vyama vya upinzani.
Amesema mwaka 2019 vyama vya upinzani havikupata nafasi ya kujipima kwa wananchi. Na kwa sasa vitakuwa na nafasi ya kujipima kama bado viko mioyoni mwa wanananchi. Lakini ni wakati mwingine kwa chama tawala kujipima.
“Lakini pia kwa wanasiasa wanaojenga ngome zao kwa ajili ya uchaguzi mkuu mwakani watajua mwelekeo wao wa kujenga himaya ukoje. Endapo watu wao watapenya kesho, basi watakuwa na kicheko na kama watapoteza basi watatakiwa kuanzisha ushirikiano na wale watakaoshinda ili waweze kujiimarisha,” amesema Dk Kristomus.
Mhadhiri huyo amesema, “lakini jambo la msingi zaidi ni uchaguzi wa kuamua mwelekeo wa siasa za mwakani. Kuanzia Januari mwaka 2025 Watanzania tutarajie pilikapilika nyingi zaidi huko mashinani na vinara wa pilikapilika hizo ni hawa wanaochaguliwa Jumatano.”
Novemba 16, 2024, akitoa takwimu za wagombea, Waziri wa Tamisemi, Mohamed Mchengerwa alisema nafasi za wenyeviti (mitaa, vijiji na vitongozi) zinazowaniwa ni 80,430 na kati ya hizo upinzani una wagombea kwenye nafasi 30,977 sawa na asilimia 38.
Alisema kwa kuzingatia maeneo ya utawala yaliyotangazwa katika gazeti la Serikali, Tangazo Na.796 na 797 ya Septemba 6, 2024, vijiji vilivyopo ni 12,333, mitaa 4,269 na vitongoji 64,274.
Alisema hata hivyo, kutokana na Halmashauri za Wilaya za Kaliua, Nsimbo na Tanganyika kuwa na makazi ya wakimbizi ya Ulyankulu, Katumba na Mishamo na wananchi kuhama kwenye baadhi ya vitongoji kutokana na sababu mbalimbali, maeneo yatakayofanya uchaguzi kwa sasa ni vijiji 12,280, mitaa 4,264 na vitongoji 63,886.
Nafasi zitakazogombewa ni 12,280 za mwenyekiti wa kijiji, 4,264 mwenyekiti wa mtaa na 63,886 za mwenyekiti wa kitongoji. Wajumbe wa Serikali ya kijijiwatagombea 230,834 na 21,320 wa kamati ya mtaa.
Idadi ya wananchi waliojiandikisha kupiga kura kwenye uchaguzi huo ni milioni 31.
Msemaji wa Jeshi la Polisi, David Misime anasema jeshi hilo limejipanga vizuri kuhakikisha upigaji wa kura unafanyika katika mazingira ya amani, utulivu na usalama.
“Mtaona askari mitaani na nje ya vituo vya kupiga kura, lengo ni kuhakikisha usalama unakuwepo wakati wote wa kupiga kura, kuhesabu hadi kutangaza matokeo.
“Tunatoa wito kwa kila Mtanzania kuhakikisha anadumisha amani, utulivu, upendo na usalama kipindi chote cha kupiga kura, kutangaza matokeo na baada ya uchaguzi. Kamwe usiwe chanzo cha uvunjifu wa amani, hautaonewa muhali utachukuliwa hatua za kisheria,” amesema Misime katika taarifa yake kwa umma.
Wakati Watanzania wanapiga kura wanapaswa kuzingatia masuala mbalimbali ikiwemo kuepuka kupiga kura kwa mgombea zaidi ya mmoja katika nafasi moja.
Kuhakikisha wanaweka alama ya vema katika kisanduku cha mgombea, kuepuka kuharibu karatasi ya kupigia kura, kuepuka kutumia simu ya kiganjani ndani ya kituo cha kupigia kura isipokua kwa wasimamizi wa uchaguzi kwa kazi maalumu ya uchaguzi.
Jambo jingine ni Watanzania kujiepusha kuvaa mavazi yanayoshabikia chama chochote cha siasa kwenye kituo cha kupigia kura.
Katika hatua nyingine, Serikali imetoa muongozo kwa waandishi wa habari kuchukua matukio kwenye uchaguzi huo.
Mkurugenzi wa Idara ya Habari Maelezo, Thobias Makoba amesema wametoa muongozo kwa kila mwanahabari atakayejitambulisha kwa kazi yake aruhusiwe kufanya kazi kwa uhuru akizingatia miongozo ya taaluma yake.
Akizungumza na waandishi wa habari jijini Dar es salaam, Makoba amesema kitu cha kwanza kitakachomtambulisha mwanahabari na kumpa uhuru wa kutekeleza makujumu yake ni kitambulisho chake cha kazi.
“Hii haina mjadala, mwandishi mwenye kitambulisho cha kazini kwake atakuwa huru kutekeleza majukumu yake au mwenye press card,” amesema Makoba.
Pia ameshauri wanahabari kuwa na jaketi maalumu na kuwa Serikali imetoa maagizo wakijitambulisha, waruhusiwe kuendelea na majukumu yao.