Dar es Salaam. Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora, George Simbachawene amewasisitiza watumishi wa umma na Watanzania wote waliojiandikisha kupiga kura kujitokeza kufanya uchaguzi wa viongozi wa Serikali za mitaa utakaofanyika kesho Novemba 27, 2024 Tanzania Bara.
Simbachawene ametoa rai hiyo leo Novemba 26, 2024 akiwa ofisini kwake katika Mji wa Serikali, Mtumba, Jijini Dodoma.
Simbachawene amesema kila Mtanzania mwenye sifa wakiwamo watumishi wa umma ni muhimu wakashiriki katika kuwachagua wenyeviti wa Serikali za mitaa, wenyeviti wa vijiji na vitongoji.
“Kwa kuwa zoezi hili ni la Kikatiba, nikiwa ndiye waziri mwenye dhamana ya kusimamia masuala ya utumishi wa umma na utawala bora, ninatoa rai kwa watumishi wote wa umma na wananchi wote waliojiandikisha kujitokeza kupiga kura ili kuchagua viongozi bora kwa maendeleo ya Taifa letu,” amesisitiza Simbachawene.
Amesema Rais Samia Suluhu Hassan ametangaza kesho kuwa ni siku ya mapumziko ili kutoa nafasi kwa watumishi wote kwenda kupiga kura.