BARAZA LA SALIM: Majengo ya Mji Mkongwe bomu linalosubiri kulipuka

Watanzania wapo katika majonzi ya kuomboleza maafa yaliyotokea Kariakoo, Dar es Salaam, ya kuporomoka kwa jengo na kuua watu zaidi ya 20 na wengine kujeruhiwa, baadhi yao vibaya.

Hii siyo mara ya kwanza kutokea ajali kama hii, Bara na Zanzibar na kila inapotokea tunazungumzia umuhimu wa kuchukua tahadhari na hatua mbalimbali za kujiepusha na janga kama hili.

Kwa kweli kazi kubwa ilifanywa na wananchi waliokuwepo karibu na eneo la tukio, walisaidia kuokoa baadhi ya watu na baadaye vikosi vya ulinzi na juhudi zilizoonyeshwa na taasisi mbalimbali za serikali na kiraia palipotokea msiba huu zinafaa kupongezwa.

Huu ndio aina ya mshikamano na udugu ambao Watanzania wanapswa kujivunia na ambao unahitaji kuenziwa na kuendelezwa.

Lakini wakati bado tuna majonzi ya kupoteza ndugu zetu, ni vizuri kwa mara nyingine tukauchukulia huu msiba kama somo la kutaka kufanya juhudi zaidi za kujiepusha na maafa ya aina hii.

Tukio la Kariakoo linafaa kuwa somo la kuwaamsha watu wa Zanzibar kuhusu hatari iliyopo kutokana na majengo mengi ya Mji Mkongwe kuwa mabovu na yasiyofaa kuishi watu.

Baadhi ya majengo hayo yamewekewa mwege wa miti mikubwa hadi sita kuzuia kuta zisiporomoke kwa zaidi ya miongo miwili hivi sasa na hakuna dalili wala ishara ya majumba hayo kubomolewa ili yasije kuporomoka na kusababisha maafa.

Mara kadha baadhi ya majengo haya, pamoja na lile la kihistoria la Beit el Ajaib lililopo karibu na bandari kuu ya Zanzibar, yameporomoka na kusababisha vifo vya watu kadha.

Hivi sasa Serikali ya Zanzibar inaendeleza miradi mikubwa ya ujenzi wa hospitali za mikoa na wilaya, masoko na vituo vya mabasi Unguja na Pemba.

Laiti juhudi za mwendo kasi kama hizi zingefanyika kwa kuyakarabati majumba ya Mji Mkongwe na kuyaangusha yale ambayo hayawezi tena kufanyiwa ukarabati, lingekuwa jambo jema.

Kwa kweli inasikitisha kuona urithi mkubwa wa majengo ya Mji Mkongwe walioachiwa Wazanzibari na wazee wao unalia na kusikitika na hakuna wa kuunyamazisha.

Laiti sehemu ndogo ya fedha zinazotumika kila mwaka kwa sherehe mbalimbali za kitaifa au mbio za mwenge kila mwaka zingepelekwa kuyaliwaza majengo haya makongwe, nadhani kilio chao kingepungua.

Hivi sasa yapo majengo zaidi ya 20 ambayo yapo katika hali mbaya na huenda, Mungu aepushe mbali, yasije kusababisha maafa, hasa wakati huu ambao mvua zinanyesha.

Mengi ya majumba ya Mji Mkongwe yalijengwa zaidi ya karne moja iliyopita na yamekuwa yakiporomoka moja baada ya jingine, huku tukiambiwa hatua zipo mbioni kuyakarabati.

Familia nyingi zilihamishwa katika baadhi ya majengo haya ambayo ni hatari kwa binadamu kukaa humo kwa vile hata bila ya vishindo yanaweza kuporomoka wakati wowote.

Ukichunguza utaona hata hayo magogo yanayozuia hayo majengo mabovu yasiporomoke nayo yameanza kuonekana yamechoka na huenda yakawa yamepungukiwa uwezo wa kuzuia vema kuta nzito za hizi nyumba ambazo nyingi zina upana za zaidi ya inchi 12, zisianguke na kusababisha maafa.

Kwa kweli kupita chini ya majengo haya katika vichochoro vyembamba vya Mji Mkongwe ni kuhatarisha maisha.

Lakini siyo hayo tu, hivi sasa yapo majengo makubwa yanayojengwa ndani ya miji na pembezoni na baadhi ya nyumba zilizojengwa zaidi ya miaka 20 au 25 iliyopita zinaongezwa ghorofa mbili hadi tatu.

Ni vizuri ukafanyika utafiti na ukaguzi wa majengo haya ili kuelewa kama misingi yake inaweza kuhimili uzito unaoongezwa na kama vifaa vya ujenzi vinavyotumika vinakidhi viwango vinavyohitajika.

Tatizo kubwa liliojitokeza kwa baadhi ya watu na hasa wafanyabiashara ni kuweka mbele tamaa ya fedha na siyo maisha ya watu.

Hili jambo halifai kufanyiwa ajizi wala muhali, kwani tahadhari ina umuhimu mkubwa katika maisha ya kila siku ya binadamu.

Kuporomoka kwa majengo kadha Zanzibar siku za nyuma na tukio la kusikitisha la kuporomoka kwa jumba la ghorofa Kariakoo, kunapaswa kuwa funzo la kutukumbusha umuhimu wa kuhakikisha majengo yetu ya ghorofa ni salama kwa wakazi na wapitanjia.

Tusisubiri maafa ndio tutishike na kuunda tume au kamati za kuchunguzi.

Related Posts