Caravans haishikiki Ligi ya Mabingwa T20

Timu ya Caravans inaonekana kuwa ni moto wa kuotea mbali kwa kriketi ya mizunguko 20 baada ya kuwafunga vigogo wa Upanga kwa wiketi 6 katika mchezo uliopigwa jijini mwishoni mwa juma.

Siku moja kabla, Caravans waliwafunga vigogo wa Agakhan SC pia kwa wiketi sita.

Katika mchezo wa pili dhidi ya Upanga, Caravans waliwazidi sana wapinzani wao hasa katika utengenezaji wa mikimbio na uangushaji wiketi.

Upanga SC ndiyo walioanza kubeti na kufanikiwa kutengeneza mikimbio   83 baada ya wapigaji wote 10 kutolewa wakiwa wametumia mizunguko 19.5 kati ya 20 iliyokwekwa.

 Iliwachukua vijana wa Caravans mizunguko 14 kutengeneza mikimbio     86 huku wakiangusha wiketi 4 na hivyo kuondoka na ushindi mnono wa wiketi 6.

Johnson Nyambo alikuwa shujaa mechi  kwa timu ya Caravans baada ya kutengeneza mikimbio  21 huku akiangusha wiketi 3 za  wapinzani. Alisaidiana na Jitin Pratap Singh ambaye alitengeneza mikimbio 17 na kuangusha wiketi 2 za wapinzani.

Katika mchezo mwingine wa Ligi ya Mabingwa, timu ya Lions iliwaadhibu Agakhan Sports kwa ushindi wa wiketi 7 katika mchezo ulipigwa katika uwanja wa Anadil Burhan jijini mwishoni mwa juma.

Agakhan ndiyo walioanza kubeti na kumaliza mizunguko yote 20 na mikimbio  131 huku wakipoteza wiketi 9.

Ilibidi vijana wa Lions wakaze mkono sana na waliweza kuwafunga wapinzani wao baada ya kupiga mikimbio 136 kwa kutumia mizunguko 18 huku wakipoteza wiketi 3, na mwisho kuibuka na ushindi wa wiketi saba.

Nyota wa mchezo katika mechi hiyo alikuwa Shamim Ali aliyetengeneza mikimbio 36 na kuangusha wiketi 3 za wapinzani.

Kashif Ahmed aliyetengeneza mikimbio 27 na kupata wiketi 1, na Umar Sheikh aliyetengeneza mikimbio 11 na kupata wiketi 2,  pia walichangia sana timu yao kushinda mchezo huo.

Related Posts