Chadema walalamikia mawakala wao kuzuiwa vituoni

Arusha. Wakati kazi ya upigaji kura ikielekea ukingoni, Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema), kimelalamikia mawakala wao kuzuiwa kuingia katika vituo vingi, na kudai kuwa waliopewa nakala zao za viapo wamekataliwa.

Akizungumza na waandishi wa habari leo Jumatano Novemba 27, 2024, Katibu wa Chadema Kanda ya Kaskazini, Amani Golugwa amedai kuwa mawakala wao waliopewa nakala za viapo wameambiwa havitambuliki kwa kuwa havina muhuri.

“Jana mawakala wetu hawakupewa nakala za viapo vyao ambavyo ndivyo vitambulisho vinavyoweza kuwaruhusu kuingia kwenye vituo, tulikaa ofisi ya Mkurugenzi wa Jiji, toka asubuhi  hawajapewa na suala hili lipo majimbo karibu yote 35 ya Kaskazini,” amedai Golugwa.

Amesema maeneo mengine mawakala wao waliopewa nakala zao za viapo, lakini walipofika vituoni leo asubuhi wameambiwa hazitambuliki kwa sababu hazina muhuri.

Golugwa amesema wanaendelea kufuatilia kwenye  kanda nzima kisha watatoa taarifa zaidi.

Hata hivyo, Msimamizi wa Uchaguzi katika Halmashauri ya Jiji la Arusha, John Kayombo amesema hajapokea malalamiko yoyote kuhusu mawakala katika vituo vyote 462.

“Changamoto kadhaa tulizokutana nazo ni kwenye baadhi ya vituo, Chadema wanatengeneza changamoto, sijajua wana shida gani, wanapeleka mawakala wawili hadi watatu tumeendelea kuwaelimisha lakini hawataki kuelewa,” amesema Kayombo.

Amesema maeneo mengine mgombea wa mtaa anataka kwenda kuwa wakala kwenye kituo cha kupiga kura wakati kanuni hazimruhusu.

Msimamizi huyo wa uchaguzi amesema wagombea wakishapiga kura wanapaswa kurudi nyumbani kusubiri kutangazwa kwa matokeo.

“Lakini wao wanataka kubaki vituoni kama mawakala, hatuendi hivyo,” amesema Kayombo.

Hata hivyo amesisitiza kwamba mpaka muda huu hajapokea malalamiko. “Na hapa unaniona niko bize na simu nawapigia kila kituo kujua wanaendeleaje, maeneo yote ambayo mawakala tuliwaapisha jana wamepokelewa vituoni,” amesema.

Akizungumzia malalamiko ya majina kutoonekana, mkurugenzi huyo amesema ambao hawajayaona majina yao huenda hawakujiandikisha Arusha.

“Wasome vizuri jiji la Arusha tumeandikisha watu zaidi ya 389,000 watulie wasome vizuri kuna kitabu cha majina kiko ndani tuna orodha ya majina ya mwanzo ipo imebandikwa na mpya imebandikwa leo asubuhi,”amesema msimamizi huyo.

Related Posts